Muro alimfunga pingu Wage- Shahidi
SHAHIDI katika kesi ya kuomba rushwa ya sh. milioni 10, inayomkabili Mtangazaji wa Kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC1), Bw. Jerry Muro nawenzake, SSP Duwan Nyanda amedai kuwa mshtakiwa huyo alimfunga pingu Mhasibu wa Halmashauri ya Bagamoyo, Bw. Michael Karoli Wage wakati akimtisha na kumuomba rushwa.
SSP Nyanda ambaye ni shahidi wa sita, alidai hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi, Bw. Gabriel Mirumbe anayesikiliza kesi hiyo.
Alidai Bw. Wage alimueleza kuwa Bw. Muro alitumia pingu kumfunga wakati anamtishia na kumuomba rushwa.
Katika ushahidi wake, shahidi huyo alidai kuwa mnamo Januari 31,2010, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Bw. Charles Mkumbo alimtaka asimamie upekuzi katika gari aina ya Toyota Cresta nyeupe ya Bw.Muro lenye namba za usajili T 545 BEH ili kuthibitisha kama kweli ndani kulikuwa na vitu vilivyodaiwa na Bw. Wage ambapo pia alidai kusahau miwani katika gari hilo.
“Nilipofanya upekuzi nilipata pea moja ya miwani, ambayo Wage aliitambua kuwa ni ya kwake, pea moja ya pingu ambayo Wage alidai kuwa ilitumika kumfunga wakati akitishwa na Muro,”alidai SSP Nyanda.
Alidai kuwa baada ya kupata vitu hivyo aliviandika katika hati ya upekuzi ambayo Bw. Muro aliisaini, yeye mwenyewe pia aliisaini pamoja na askari Lugano.
Baada ya kueleza hayo, Nyanda aliiomba mahakama ipokee hati hiyo ya upekuzi, miwani na pingu kama sehemu ya vielelezo katika kesi hiyo kama upande wa utetezi utakuwa hauna pingamizi.
Mawakili wa utetezi wanaowatetea kina Muro, Bw. Richard Rweyongeza, Bw. Paschal Kamara na Bw. Majura Magafu walidai kuwa hawana pingamizi na hivyo mahakama ilivipokea kama vielelezo katika kesi hiyo.
Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake, Hakimu Mirumbe aliiahirisha kesi hiyo hadi Machi 7 na 8, mwaka 2011 itakapoendelea kusikilizwa tena.
Wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Bw. Deogratius Mgasa na Bw.Edmund Kapama.
SOURCE:MAJIRA
No comments:
Post a Comment