Monday 28 March 2011

BABU ASITISHA KUPATA KIKOMBE KWA WIKI MOJA


HUDUMA za uponyaji wa magonjwa sugu, zinazotolewa na Mchungaji mstaafu wa KKKT, Ambilikile Mwaisapile, zimesitishwa kwa wiki moja,kufuatia matukio ya idadi kubwa ya watu wanaofuata tiba kufariki dunia kabla ya kupata huduma.
Mchungaji Mwaisapile maarufu Babu, aliwaambia waandishi wa habari jana hali katika Kijiji cha Samunge, sasa ni mbaya, yakiwa ni matokeo ya kuongezeka kwa idadi ya watu wanaofuata tiba.
Alisema hata hivyo, ongezeko la watu katika kijiji hicho limesababisha madhara makubwa ya kiafya kwa maelfu ya watu."Tumeelemewa na idadi ubwa ya watu, naomba halmashauri ya wilaya itusaidie ili tuweze kuwahudumia hawa watu ambao sasa wanakufa hata kabla ya kupata dawa," alisema.
Alisema yeye binafsi, bado ana nguvu, nia na uwezo wa kuendelea kutoa tiba kwa kadri mwenyezi Mungu alivyomjalia na kumwelekeza na kwamba anachohitaji ni ushirikiano katika kuboresha taratibu ili tiba ipatikane bila usumbufu na adha kwa wananchi.

Akisoma tamko la Mchungaji Mwaisapile, Ofisa Makazi wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Frederick Mwisagile, alisema linakuja baada ya kupewa taarifa kuhusu msururu wa magari uliokwama kilometa 55 kutoka nyumbani kwake.Habari zilisema msururu unakakadiriwa kuwa na zaidi ya magari 4,000 na mengine zaidi ya 100 yamekwama.

Mchungaji huyo aliiomba serikali isaidie kupunguza msongamano wa watu na magari yanaoendelea kwenda katika kijiji hicho yakitokea ndanni na nje ya nchi."Nimeambiwa watu wasiopungua 24,000 wapo ndani ya magari kwenye foleni. Najua itawachukua kati ya siku tatu hadi saba kufika kwangu, kwa kweli hali hii si nzuri na inahitaji hatua zichukuliwe haraka,"alisema.

Kwa mujibu wa mchungaji, njia ya kukabiliana na msongamano huo, ni kuhakikisha watu walioko kwenye msururu wanaisha kwanza."Naomba kuanzia leo tarehe 26 hadi Aprili mosi nishughulike na hawa waliopo kwenye foleni ili waishe kwanza,"alisitiza Mchungaji Mwaisapile.

Pia alipendekeza magari yanayokwenda Loliondo, yakaguliwe vizuri na mamlaka zinazohusika ili kuhakikisha kuwa a ni mazima na si malori.Alisema hiyo inatokana na ukweli kwamba   barabara ni mbaya na mvua zinaendelea kunyesha.

Babu pia alitaka wagonjwa mahututi walioko mahospitalini, wasitolewe na kupelekwa kwake.Hali kadhalika, aliwataka wale wanaotumia dawa, kubeba dawa za kutosha wakiwa safarini na kwamba ushauri huo unakuja baada ya kubainika kuwa idadi kubwa ya watu wanapoteza maisham walikuwa na ugonjwa wa sukari na hawakubeba dawa za kutosha, wakiamini kuwa wangepata dawa haraka na kuondoka.

Katika tamko lake, mchungaji huyo amependekeza pia barabara ikarabatiwe na kuweka utaratibu mzuri utakaowezesha watu 2,000 kupata tiba na kuondoka  kwa siku moja.Pia alitaka kuwepo kwa  vituo vya kukagua magari katika maeneo mbalimbali ya barabara na kusimamia utaratibu ili watu wasikae katika foleni zaidi ya siku moja.

Mchungaji pia alipendekeza mazingira ambayo sasa yamechafuliwa sana, yasafishwe na kujengwa  vyoo vya kutosha na kwamba hayo yafanyikw pamoja na kusogeza  karibu huduma za maji.

Aliishauri serikali itengeneze maeneo ya kuwawezesha wagonjwa kupumzika wakati wakisubiri kupata tiba.Halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro, imekuwa ikitoza kila gari linalokwenda Lolindo, ushuru wa Sh5,000 wakati helkopta zikilipiwa ushuru wa Sh 150,000 na inaelezwa kuwa fedha hizo ni za  kugharimia huduma mbalimbali zinazotolewa na halmashauri hiyo.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ngorongoro, Benjamini Maziku, alisema hadi Machi 24 mwaka huu, watu 52 walikuwa wamefariki dunia wakiwa hawajapata tiba kwa sababu ya misururu mirefu.
chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment