Monday 2 May 2011

MZIGO WA MADENI WAWAELEMEA WATANZANIA

MZIGO  wa madeni umeendelea kuwaelemea Watanzania  hususan walalahoi  kutokana na kuendelea kuongezeka kwa deni la Taifa ambalo limefikia zaidi ya Sh10.5 trilioni.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Ludovick Utouh, deni la taifa limeongezeka kwa asilimia 38 kutoka Sh7.6 trilioni katika mwaka wa fedha 2008/09 hadi Sh 10.5 trilioni  mwaka 2009/2010.
Ongezeko hilo limebainika wakati wa ukaguzi wa Fedha za Serikali Kuu katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2009/2010, kilichoishia Juni 30/2010.Kuongezeka kwa deni hilo ni mzigo mkubwa kwa walalahoi kwa kuwa ndio walipaji wakubwa wa kodi mbalimbali licha ya kuwa fukara.
Utouh alibainisha hayo katika taarifa hiyo kwamba jumla ya deni la Taifa kwa kipindi cha mwaka mmoja, limeongezeka kwa zaidi ya Sh2.8 trilioni.Alisema katika kipindi hicho deni la nje liliongezeka kwa zaidi ya Sh2.5 trilioni sawa na asilimia 44, huku deni la ndani likiongezeka kwa zaidi ya Sh521.2 bilioni sawa na asilimia 23.

Mchanganuo huo ulionyesha kuwa Serikali ilikopa kiasi kikubwa cha fedha kutoka taasisi mbalimbali za nje kuliko kiasi kilichokopwa katika taasisi za ndani ya nchi.

“Hii inamaanisha kuwa Serikali ina dhima kubwa katika kuwalipa wadai wa nje kuliko wadai wa ndani, na hii kiuchumi ina maana kuwa kiasi kikubwa cha mtaji katika fedha za kigeni kitalipwa nje ya nchi,” inasema taarifa ya CAG.Taarifa hiyo ilifafanu kuwa uchumi wa taifa, umekuwa kwa asilimia  6.5 tu kutoka mwaka 2008/09 hadi 2009/10. “Hali hii ni ya kutisha kama haitaendana na ukuaji wa hali ya uchumi wa nchi,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Mbali na deni hilo la fedha ilizokopa serikali, taarifa ya CAG pia imebaini kuwapo kwa deni lisilotarajiwa la Sh26 bilioni yaliyozihusisha Wizara tisa na Mikoa mitatu, huku CAG akibainisha kwamba madeni kama hayo ni mzigo mkubwa kwa serikali. 

“Hata hivyo, chanzo cha madeni haya hakikuonyeshwa. Madeni yasiyotarajiwa kama haya ni mzigo mkubwa kwa Serikali hasa pale yanapoiva na kutakiwa kulipwa.“Hivyo ningependa kuishauri Serikali  kujiepusha katika kufanya maamuzi ambayo yatasababisha kushamiri kwa madeni yasiyotarajiwa,”alisemaUtouh katika taarifa yake.
Wakati deni la taifa likizidi kukua kwa kiasi hicho, taarifa CAG ilibaini kuwapo kwa  mikopo isiyorejeshwa ya Sh424 bilioni katika kipindi hicho, ikiwa ni ongezeko la Sh7.6 bilioni sawa na asilimia 2 ikilinganishwa na mwaka 2008/09.

Ukaguzi huo umebaini kuwa madeni yamekaa bila kulipwa kwa muda wa zaidi ya miaka mitatu, huku taarifa ya  Msajili wa Hazina ikionyesha kwamba Serikali imeshindwa kuokoa Sh281.8 milioni  kutoka kwa kampuni ya Ginaac Industries Ltd na Sh44 milioni kutoka kwa Mansoons Ltd.

Deni lingine ambalo CAG amelibaini katika ukaguzi wake ni Sh2 bilioni katika  mfuko wa kubadilisha Madeni na Benki, ambalo lilionekana kupotea.

chanzo:mwananchi

yale yalee,pesa inayokopwa haieleweki inaenda wapi na wala inafanya nini,deni linazidi kupanda hela iliyokopwa haionekana,kilio cha watz sijui lini kitasikilizwa tuondokane na huyu luba wa ufisadi aliyetuganda.

No comments:

Post a Comment