Monday 4 July 2011

KASHFA YA RUSHWA WIZARA YA NGELEJA



MAOFISA WA JUU WATUHUMIWA KUIHONGA KAMATI YA MAKAMBA
Mwandishi Wetu
WIZARA ya Nishati na Madini imeingia katika kashfa nzito ambapo baadhi ya maofisa wa wizara hiyo wanatuhumiwa kuwahonga baadhi ya wabunge katika Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kwa kile kinachodaiwa kutaka bajeti ya wizara hiyo kupita kwa urahisi, Mwananchi limebaini.
Habari zilizopatikana kutoka Dodoma na Dar es Salaam zimedokeza kuwa taarifa za uovu huo tayari zimefikishwa mezani kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye amesema atalishughulikia baada ya kuwa amewasiliana na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Kwa mujibu wa habari hizo suala hilo pia tayari limefikishwa kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda na kwamba kamati ya uongozi ya bunge anayoiongoza pia imearifiwa kuhusu suala hilo.
Kashfa hiyo imeikumba wizara hiyo katika kipindi kigumu ambacho nchi iko gizani huku wizara hiyo ikilaumiwa kutokana na uhaba wa nishati ya umeme kiasi cha Waziri Ngeleja kutangaza mgawo wa saa 10 wakati wa mchana na saa sita wakati wa usiku "ni janga la kitaifa".
Habari zaidi zinasema miongoni mwa mambo muhimu ambayo kamati hiyo ilikuwa ikitaka maelezo ni mapendekezo ya wizara hiyo kutaka kujenga jeno la makao yake makuu jijini Dar es Salaam kinyume cha ilani ya CCM ambayo inaweka wazi kwamba hakutakuwa na ujenzi wa makao makuu ya wizara jijini humo katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Habari zilizolifikia Mwananchi zilidai kwamba, Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini ya Bunge, January Makamba ndiye aliyewasilisha malalamiko kwa Pinda na Makinda baada ya kubaini 'ulegevu' miongoni mwa wajumbe wa kamati yake wakati wa mchakato wa kujadili mapendekezo ya bajeti ya Wizara hiyo na kwamba mapema alikuwa ameishapokea taarifa kuhusu baadhi ya wajumbe wake kuhongwa.
"Mwenyekiti (January) alipewa taarifa za wajumbe wawili wa kamati yake ambao walikataa hongo hiyo, na baada ya kufanya uchunguzi alibaini kwamba kuna kila dalili kwamba baadhi ya wabunge katika kamati yake walikuwa wamebadili msimamo katika baadhi ya mambo," kilieleza chanzo chetu mjini Dodoma.
Habari zaidi zilidai kuwa kufuatia hali hiyo, January aliitisha kikao cha wabunge ambao ni wajumbe wa kamati yake na kugeuka mbogo, huku akiweka bayana kuchukizwa kwake na taarifa za wajumbe wake kuhongwa na kwamba alikwenda mbali zaidi akitishia kujiuzulu nafasi ya uenyekiti ili kutoa nafasi kwa wabunge hao kuchagua mwenyekiti mwingine ambaye atakuwa tayari kuvumilia uovu huo.
"Yule kijana (January) alikasirika sana, alichukizwa kweli kweli na hali hiyo kwa sababu ni kama wajumbe waliopokea hizo bahasha walikuwa wakimzunguka kwani tayari walikuwa wanajua nini wanachopaswa kufanya ili kuziokoa sekta za nishati na madini,"kilieleza chanzo hicho.
Kadhalika suala hilo la hongo lilijadiliwa katika kikao cha pamoja baina ya wajumbe wa kamati hiyo na viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini, ambapo Waziri Ngeleja na Naibu wake, Adam Malima waliomba radhi kutokana na tukio hilo, hivyo kamati hiyo kuagiza maofisa wa wizara waliohusika wachukuliwe hatua.
"Ni kama Ngeleja na Malima walimalizana na kamati, si unajua maana ni kama January alikuwa peke yake, kama kulikuwa na wanaomsapoti (wanaomuunga mkono) walikuwa ni wachache, hivyo kama waziri na naibu wake waliomba radhi hakukuwa jinsi zaidi ya kumalizana nao," zilidai taarifa hizo na kuongeza:
"Hata hivyo Mwenyekiti na baadhi ya wajumbe walimwagiza Ngeleja na Malima kuwachukulia hatua maofisa waliohusika na ugawaji wa fedha hizo kwa baadhi ya wabunge".
Kauli za viongozi
Mwananchi liliwasiliana na January ili kufahamu undani wa suala hilo, lakini mbunge huyo wa Bumbuli hakukanusha wala kukubali kuhusu baadhi ya wajumbe wake kupokea rushwa.
"Nani kakwambia bwana, mimi siwezi kuzungumza lolote, mambo ya kamati jamani si yote tunayoweza kuweka wazi, lakini siku hizi hatufanyi vikao bila kuwaruhusu waandishi wa habari, kama hayo yangetokea si yangeonekana wakati huo?,"alihoji January.
Waziri Ngeleja kama ilivyo kwa January naye hakukubali wala kukanusha kuwepo kwa tuhuma hizo na badala yake alisisitiza kwamba anayeweza kuzizungumzia ni mwenyekiti wa kamati akimaanisha January.
"Unasikia, kama jambo limetokea kwenye kamati mimi sina mamlaka ya kulizungumzia hata kidogo maana nitakuwa navunja kanuni, kama wengine nilivyowaambia maana naona leo wengi wananitafuta kwa habari hii, mpigieni mwenyekiti wa kamati yeye ana mamlaka, mimi kwangu no comment (siwezi kusema chochote),"alisema Ngeleja kwa simu.
Spika wa Bunge, Makinda kwa upande wake pia alikanusha kupokea taarifa hizo. "Mimi ndiyo nazisikia kutoka kwako, pengine kama zimeletwa kwa barua sijaiona, lakini sifahamu kitu kama hicho," alisema Makinda alipozungumza kwa simu na Mwananchi.
Kwa upande wake Naibu Spika Job Ndugai alisema kuwa hana taarifa hizo kwa kuwa yeye alikuwa nje ya nchi kikazi. "Ndugu yangu, pengine ukimpata Spika anaweza kukusaidia, mimi nimerudi jioni hii (jana jioni) ndio naingia hapa Dodoma najiandaa kwa ajili ya kesho,"alisema Ndugai.

mwananchi 

No comments:

Post a Comment