Tuesday 19 July 2011

Rushwa yatikisa Nishati na Madini

KATIBU MKUU ADAIWA KUENGA SH1 BILIONI KUWAHONGA WABUNGE
Leon Bahati, Dodoma, Furaha Maugo, Dar
MBUNGE wa Kilindi (CCM), Beatrice Shellukindo amelipua bomu Bungeni akimtuhumu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, kwa kutumia zaidi ya Sh 1 bilioni kwa ajili ya kutoa rushwa kwa watu mbalimbali ili bajeti ya wizara hiyo iweze kupitishwa na Bunge.
Tuhuma hizo nzito zinakuja kipindi ambacho tayari Wabunge wa Kamati ya Nishati na Madini wakiwa wameibua tuhuma kama hizo za baadhi ya wajumbe kutaka kuhongwa na maofisa wa wizara hiyo, ili kurahisisha upitishaji wa bajeti ndani ya kamati.

Takriban wiki tatu tangu wabunge wa kamati hiyo kuibua tuhuma hizo ambazo zilifika hadi kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, jana Shellukindo alikoleza moto huo wakati akichangia bajeti ya wizara.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda jana alikubaliana na tuhuma hizo. Akitoa hoja ya kuondoa bungeni hotuba ya makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini, Pinda alisema alikuwa akisubiri Rais Jakaya Kikwete afike Afrika ya Kusini alikokwenda katika ziara ya kiserikali ili aweze "kumshtaki" Katibu Mkuu huyo kutokana na tuhuma zilizotolewa dhidi yake. Pinda alisema hawezi kuchukua hatua dhidi ya Jairo kwani kwa mujibu wa sheria, mamlaka ya uteuzi ndiyo inayoweza kuchukulia hatua dhidi yake.

"Kwa jinsi jambo hili lilivyokaa, hakuna jinsi mtu unavyoweza kulitetea hata kidogo, nilitamani sana kwamba nije hapa niseme kwamba uamuzi wangu mimi ni huu, lakini haikuwezekana," alisema Pinda na kuongeza: "Kwa dhati kabisa naomba wabunge tuwe na subira, mara tu mheshimiwa Rais atakapotua South Africa (Afrika Kusini) jioni ya leo  (jana), nitamuarifu na ninaamini tutaelewana kuhusu hatua za kuchukua."

Shinikizo la kutaka Jairo kuondolewa katika nafasi yake lilitolewa ndani ya kikao cha wabunge wa CCM waliokutana jana mchana wakitaka Katibu huyo wa zamani wa Rais Kikwete afukuzwe kazi, huku wakiitaka Serikali iiamuru Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru) imchunguze.

Awali, akichangia bajeti hiyo bungeni jana huku akianza kwa kumwomba Mungu msaidie katika kauli zake, alisema alifanikiwa kuipata barua iliyoandikwa na Jairo kwenda kwa taasisi na idara zaidi ya 20, ikiagiza zitoe Sh50 milioni kila moja.

Shellukindo alisema barua hiyo inaonyesha idara na taasisi hizo ziliagizwa fedha hizo ziwekwe kwenye akaunti namba 5051000068 inayomilikiwa na Geological Survey of Tanzania (GST) kwenye Benki ya NMB, Tawi la Dodoma."Tena inaagiza kwamba fedha hizo zikishatumwa kwenye akaunti hiyo, wizara ipewe taarifa kupitia Ofisi ya DP kwa ajili ya utaratibu," alisema.

Alisema barua hiyo yenye kichwa cha habari: "Yahusu kuchangia gharama za kukamilisha maandalizi na uwasilishaji wa hotuba ya bajeti ya wizara ya 2011/12 bungeni Dodoma, Jairo alisema wizara imefanikisha maandalizi ya mpango wa bajeti kwa mwaka 2011/12 na imekwishapitishwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na hivyo aliinukuu barua hiyo: "Katika kukamilisha mchakato huo, hotuba ya bajeti inatarajiwa kuwasilishwa Bungeni tarehe 15 na 18, Julai 2011."

"Kama ilivyo kawaida wakati wa kuwasilisha hotuba ya Bajeti Dodoma, maofisa mbalimbali wa wizara na taasisi zilizo chini yake huambatana na viongozi waandamizi kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa masuala yanayojitokeza wakati wa mjadala wa hotuba hiyo. Ili kufanikisha mawasilisho ya hotuba hiyo ya bajeti, unaombwa kuchangia jumla ya Sh50 milioni.

Katika uchunguzi wake, Shellukindo alisema amebaini fedha hizo tayari zimetolewa na Jairo kwenye benki hiyo hivyo akahoji; "Naomba kufahamu fedha hizo zimekwenda wapi?"

Kutokana na hali hiyo, Shellukindo alishauri bajeti hiyo isiendelee kujadiliwa Bungeni na badala yake Ngeleja arejeshewe ili akaifanyie marekebisho na aiwasilishe upya Bungeni baada ya wiki mbili... "Nakusudia kutoa hoja kwamba bajeti hii irudishwe na baada ya wiki mbili irudishwe hapa.”

Habari kutoka ndani ya Kikao cha Kamati ya Wabunge wa CCM zinasema kuwa wabunge hao walikuwa wametoa muda kwa Serikali kwamba hadi saa 11:00 jioni jana Jairo awe amefukuzwa kazi. Kwa mujibu wa habari hizo, wabunge hao pia waliitaka Serikali kuielekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru) kuanza uchunguzi wa jinsi fedha hizo zilivyotolewa na matumizi yake, ili ikibainika vinginevyo wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

Chanzo chetu ndani ya kikao hicho cha wabunge wa CCM kiliwataja waliotaka Jairo afukuzwe kazi kuwa ni pamoja na Christopher Ole Sendeka (Simanjiro), Esther Bulaya (Viti Maalumu), George Simbachawene (Kibakwe), Godfrey Zambi (Mbozi Mashariki), Henry Shekifu (Lushoto), Murtaza Mangungu (Kilwa Kaskazini), Alphaxard Lugora (Mwibara), Shellukindo (Kilindi) na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, January Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli.

"Wabunge wamegeuka wamekuwa wakali sana na hawataki kusikia cha mtu, wamesema lazima leo (jana) ikifika saa 11 Jairo awe amefukuzwa kazi, hawataki kumuona kabisa," alisema mmoja wa wabunge waliohudhuria kikao hicho.Mbunge huyo alisema Waziri Ngeleja na Naibu wake, Adam Malima pia walitakiwa wajiuzulu kwa maelezo kwamba: "Haiwezekani wasiwe wanafahamu chochote kuhusu mkakati huo wa katibu wao mkuu katika wizara wanayoiongoza."

"Hawawezi kujivua lawama, hata hao tumewataka wajiuzulu, ina maana gani kama barua nzito namna hiyo Waziri na Naibu wake hawazifahamu, haiingii akilini kabisa," alisema mbunge huyo.

Wabunge walivyoikataa Bajeti ya Ngeleja
Wakichangia mjadala wa bajeti hiyo jana, wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na upinzani walisimama imara na kueleza bayana kwamba hawako tayari kuipitisha bajeti hiyo. Hali hiyo ilisababisha baada ya mjadala huo uliomalizika mchana, wabunge wa CCM kuitwa kwenye kikao maalumu cha kichama.

Wakati wa mjadala, wabunge wengi walikuwa na shauku ya kuchangia lakini Spika Anne Makinda alisema wote wasingeweza kupata nafasi hiyo kutokana na muda.

"Nataka nianze kwa kusema siungi mkono hoja ya kupitishwa kwa bajeti hii na nawaomba wabunge wenzangu msipitishe bajeti hii kwa sababu tupo gizani," alisema Dk Hamis Kigwangala (Nzega-CCM) alipoanza kuchangia mjadala wa bajeti hiyo. Mbali na tatizo la umeme, alitaja sababu nyingine za kutaka bajeti hiyo isipitishwe kuwa ni mikataba mibovu ya sekta ya madini na nishati, ambayo imesababisha rasilimali za nchi kuibwa na wageni huku Watanzania walio wengi wakiendelea kuogelea kwenye umasikini.

"Waliosababisha hayo wanajulikana lakini hawachukuliwi hatua. Wengine wapo hapa bungeni na wengine wako serikalini. Hii ni mikataba kandamizi. Watu hao wapo kwenye 'system' (mfumo wa Serikali). Nchi inauzwa, wachache wanashibisha matumbo yao," alisema.

Alisema watu hao wamelifikisha taifa kwenye mazingira hayo ya kifisadi kwa sababu ya kutumia nafasi zao kujinufaisha na kuweka kando maslahi ya umma wa Watanzania... "Hawa watu kama hawafikirii kwa matumbo wanafikiria kwa kutumia 'spinal cord' (uti wa mgongo) badala ya ubongo."

Alisema watendaji hao walioliingiza taifa kwenye mikataba hiyo mibovu wanapokwenda kuisaini wanajali kile watakachopata ili kufanikisha malengo yao binafsi kama vile kujenga majumba ya kifahari. "Wanaruhusu ardhi ya Watanzania kuuzwa nao wanafaidi kwa kwenda kujenga Mbezi Beach (Dar es Salaam)," alilalamika Dk Kigwangala na kusema ni jambo ambalo halipaswi kufumbiwa macho.

Alisema miongoni mwa mikataba ya kifisadi kuwa ni ule kati ya Pan African na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuhusiana na uzalishaji na usafirishaji wa gesi asilia. Katika mpango huo alisema Serikali imepoteza kodi ya Sh100 bilioni kwa udanganyifu kiasi ambacho alisema kingeweza kutatua tatizo la umeme nchini.Kwa sababu hiyo, Dk Kigwangala alitaka mikataba yote ya madini na nishati ivunjwe ili uandaliwe utaratibu mzuri wa kufaidisha umma wa Watanzania.

"Uchungu wangu ni kwamba ardhi yote (nchini) yenye madini na gesi imenunuliwa na Wazungu," alisema Dk Kigwangala na kuitaka Serikali itoe majibu katika masuala matatu muhimu... "Serikali itamke mwisho wa wageni... Leseni zote zifutwe na itafute wabia wengine... Serikali ieleze imejipanga vipi kuchukua fedha za Pan African Energy na iweke wazi lini tatizo la umeme litapatiwa ufumbuzi."

Naomi Kaihula (Viti Masalumu-Chadema) aliunga mkono ushauri wa Dk Kigwangala kuwa wabunge wote wasipitishe bajeti hiyo akisema tatizo la umeme limesababisha maeneo mengi ya nchi kuwa na mgawo wa saa 12 linaangamiza uchumi wa nchi. Alisema athari hiyo imevikumba viwanda, kampuni na hata wajasiriamali wadogowadogo ambao wengine mitaji yao imetokana na kukopa.

"Tukipitisha bajeti hii Watanzania watatuona kuwa sisi ni watu tusio na akili. Tusiipitishe kwa sababu tunawapenda wananchi," alisema Kaihula akiwaomba wabunge kuweka kando tofauti zao za kiitikadi na badala yake kuwa na nguvu ya pamoja kuizuia bajeti hiyo.

Alisema kuwa serikali imeonekana kuwa dhaifu hata kwa wafanyabiashara wa hapa nchini akitoa mfano kuwa walishindwa kupambana na uchakachuaji wa mafuta na badala yake kupandisha gharama ya bei ya mafuta ya taa jambo ambalo limeongeza ugumu wa maisha kwa watu wa kipato cha chini.

Lolesia Bukwimba (Busanda-CCM) alilalamika wakazi wa jimboni kwake wengi wao ni masikini na wanachoambulia ni vumbi linalotimuliwa na misafara ya magari yaliyobeba madini kutoka ardhi yao.

Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole-Sendeka alisema licha ya taifa kukabiliwa na mgawo wa umeme, ratiba yake haiheshimiwi na kuongeza kuwa hiyo ndiyo inayosababisha wananchi kuchanganyikiwa zaidi kwa sababu wanaotegemea umeme kwa shughuli za ujasiriamali wanashindwa kujipanga ili kukabiliana na hali hiyo.
Alibeza mpango wa Serikali wa kununua mitambo miwili ya kuzalisha umeme; megawati 100 ambao utafungwa Ubungo, Dar es Salaam na megawati 60 mkoani Mwanza akisema hautakuwa na manufaa yoyote kwa sababu ya mgogoro uliopo wa gesi kidogo inayosafirishwa hadi Dar es Salaam kutotosheleza mahitaji.

Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed aliitaka serikali kuchukua uamuzi mgumu kama uliowahi kuchukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) wa kufuta mikataba yote ya madini na kuanza upya. Alisema Bunge lina madaraka ya kubadili mfumo wa uendeshaji wa sekta ya madini kupitia kamati zake, hivyo akahimiza hatua hiyo ichukuliwa haraka iwezekanavyo.

Kwa upande wake, Hussein Amar (Nyang'hwale-CCM) alisema yupo tayari kumpa somo Waziri Ngeleja la jinsi wawekezaji wa sekta ya madini wanavyofaidika huku wakidanganya kuwa wamekuwa wakipata hasara kwenye biashara hiyo. Alisema wizi huo umekuwa ukifanyika kwa ushirikiano kati ya wawekezaji na wataalamu wazalendo ambao wamesomeshwa kwa jasho la Watanzania kupitia kodi zao.

Akichangia bajeti hiyo, Eustace Katagira (Kyerwa-CCM) aliilaumu Wizara ya Nishati na Madini akisema katika jimbo lake hakuna mtandao wa umeme licha ya ahadi nyingi za miaka iliyopita.Silvestry Koka (Kibaha Mjini-CCM) alisema kuwa tatizo la umeme linalolikumba taifa kwa sasa linatokana na Serikali kutowekeza vya kutosha kwenye sekta ya nishati.

Kuhusu sekta ya madini alisema kuna migogoro mingi kwa sababu Watanzania hawafaidiki na rasilimali hiyo na badala yake wageni wanajipakulia wapendavyo. Alisema baadhi ya wawekezaji walikuja nchini wakiwa na timu kubwa ya wafanyakazi ambao utaalamu wao hautofautiani na ule wa Watanzania: "Sheria ipo lakini haitekelezwi... tunajenga chuki bila sababu, Watanzania wanazidi kudhalilika."

MWANANCHI

No comments:

Post a Comment