katibu mkuu wa wizara ya nishati na madini bw david jairo
SIKU moja baada ya Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, kumrejesha kazini Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, Rais Jakaya Kikwete, amemsimamisha tena kazi ili kupisha uchunguzi zaidi juu ya tuhuma zinazomkabili kuhusiana na matumizi mabaya ya madaraka yake.
Jairo ambaye juzi aliingia ofisini na kupokelewa kwa shangwe na wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini, ikiwa ni pamoja na gari lake kusukumwa na watendaji wakuu wa wizara hiyo, jana hakuwapo ofisini kuashiria kwamba alipewa taarifa ya kuendelea na likizo mapema.
Juzi, Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe, alishawishi wabunge kusimamisha shughuli zote za Serikali katika Bunge hilo hadi hapo taarifa ya uchunguzi wa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), iliyomsafisha Jairo iwasilishwe na kujadiliwa na Bunge.
Hata hivyo, kikao cha Kamati ya Uongozi kilichoitishwa na Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, baada ya hoja hiyo ya Zitto kukubaliwa na nusu ya wabunge kilikubali hoja hiyo na kiliirejesha bungeni na hatimaye kujadiliwa na Bunge kisha kuridhia kuundwa kwa Kamati teule ya kuchunguza suala hilo.
Pinda atangaza uamuzi wa Rais
Jana, wakati Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akijibu maswali ya papo kwa hapo bungeni, alitangaza hatua hiyo ya mkuu wa nchi akisema: “Suala la Jairo limefika kwa Rais na tayari amekwishalitolea uamuzi”. Kiongozi wa Kambi rasmi ya upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, akimuuliza swali la kwanza katika siku ya maswali kwa Waziri Mkuu, alisimama na kutaka kauli ya Serikali kuhusiana na jambo hilo.
“Mheshimiwa Spika, naomba kujua kuhusu kauli iliyotolewa kuhusu uamuzi wa Katibu Mkuu Kiongozi kuhusiana na Katibu wa Wizara ya Nishati na Madini ambayo imeleta utata mkubwa; na kwa sababu Bunge jana liliridhia kuunda kamati ya kuchunguza sakata hilo; na kwa sababu Katibu Mkuu Kiongozi alimrudisha Bwana Jairo ofisini je, Serikali haioni kuwa kuna umuhimu wa Bwana Jairo kuendele na likizo wakati uchunguzi wa jambo hilo utakapofanyika?,’’ Aliuliza Mbowe.
Akijibu swali hilo Pinda alisema: “Mheshimiwa Spika, naomba niliarifu Bunge lako tukufu kwamba, hatua hiyo tayari imeshachukuliwa na Rais na ninachoweza kuliarifu Bunge lako ni kwamba, kwa kuwa jambo lenyewe limefanyika kwa utaratibu unaofaa, Serikali itatoa ushirikiano wa kutosha ili tuweze kubaini mazingira na mambo yote yanayoendana na jambo hilo,’’
Baada ya taarifa hiyo ya Waziri Mkuu, Bunge lililipuka kwa kelele za shangwe kuonyesha kuwa wamekubaliana na uamuzi wa Rais.
“Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri Mkuu kwa majibu yake ambayo ni ya kuridhisha. Pia ningependa kujua kwamba ilikuwaje Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ilikuwa na bajeti kubwa kuliko wizara nyingine zote ilitumia jumla ya Sh174.5 milioni kuwezesha bajeti kupita na Wizara ya Madini na Nishati ilitumia Sh578 milioni?" Aliuliza Mbowe na kuongeza:
"Je, pamoja na kuwa Bunge linazungumza, Serikali itakuwa tayari kuwachukulia hatua wote waliohusika na itakuwa tayari kutoa tamko kwamba, kitendo cha kukusanya fedha siyo utaratibu mzuri wa Serikali.’’
Akijibu swali hilo, Pinda alisema hawezi kulizungumzia zaidi jambo hilo na kwamba, ripoti itakayopelekwa bungeni na Kamati teule ndiyo itakayotoa maoni yake juu ya jambo hilo pamoja na kueleza nini kifanyike.“Siwezi kusema kitu chochote juu ya jambo hilo, lakini kamati itakayoundwa itatoa majibu na mapendekezo ya nini kifanyike ikiwa fedha hizo zilikuwa zikikusanywa kwa nia njema basi ni sawa, lakini kama ni kwa njia nyingine yoyote, basi hatua kamili zitachukuliwa,’’ alisema Pinda.
Kigwangala ajitosa
Mbunge wa Nzega, Dk Khamis Kigwangala (CCM), wakati akimuuliza swali Waziri Mkuu, alimtaka atoe majibu kuhusiana na jambo hilo ambalo alidai kuwa ana ushahidi wa kutosha kwamba, mbali na fedha zilizoelezwa hapo awali, Jairo alikuwa amefanya ufisadi mwingine.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, mbali na ile iliyozungumzwa hapo awali ninao uthibitisho kuwa sio fedha hizo tu, bali Jairo alifanya madudu mengine na vielelezo ninavyo hapa naweza kukupa ukitaka sasa hivi,’’ alidai Kigwangala.
Mbunge huyo alisema anavyo vielelezo, ambavyo ni pamoja na kinachoonyesha kuwa Jairo alichangisha Sh22 milioni na Sh5.8 milioni katika mazingira tofauti ambavyo alidai kuwa, ni kuonyesha ni namna gani Jairo alivyokuwa akitumia vibaya fedha za walipa kodi.
Hata hivyo, Pinda alisema kwamba, mambo yote hayo pamoja na vielelezo alivyovitoa Kigwangwala vitafanyiwa kazi na Tume itakayoundwa kabla ya kuahirishwa kwa Bunge leo ili vifanyiwe kazi kwa pamoja.
Kamati Teule ambayo itaundwa kufuatia hoja ya Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka alipokuwa akichangia hoja ya awali iliyotolewa na Zitto, inatarajiwa kutangazwa leo na Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Wizarani kwazizima
Katika Wizara ya Nishati na Madini, hali ilikuwa tulivu na gazeti hili lilifika katika ofisi ya Jairo haikumkuta mtu yeyote. Msaidizi wa Jairo, ambaye alijitambulisha kwa jina la Elias Kayandabila, alisema yeye siyo msemaji.
"Kila eneo lina utaratibu wake na mimi si mzungumzaji, hivyo ni vizuri muende kwa Tesha (Ofisa Uhusiano wa Wizara)," alisema.
Msemaji wa wizara hiyo, Alyoce Tesha, alisema kuwa Jairo aliomba likizo na aliyekuwa anakaimu nafasi hiyo wakati hayupo, Eliakimu Maswi, ataendelea kushikilia nafasi hiyo."Serikali ina utaratibu wake na makatibu wakuu wanasimamiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, yeye ndiye anayejua atakuwa amempa likizo ya muda gani, hivyo kamuulizeni yeye," alisema Tesha.
NCCR yatoa neno
Kwa upande wake, Chama cha NCCR-Mageuzi kimesema kilichotokea kwa Jairo kinadhihirisha wazi kwamba mfumo mzima wa Serikali umechoka, haufai na ndiyo sababu ya kukithiri kwa ufisadi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia, alisema: “Iweje Rais Kikwete atoe maamuzi mengine ya kumpa likizo Jairo huku akimwacha Luhanjo aliyemrudisha kazini?”
Mbatia aliongeza: “Aliyoyafanya Katibu Mkuu huyo ni kama tone moja la maji ndani ya bahari”.
Mbatia alisema kwamba, ndio maana sakata la Richmond aliyewajibika alikuwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na si viongozi wengine.
Mbatia alifafanua majukumu ya mihimili ya Serikali akisema: “Serikali itatawala kwa kutekeleza sheria, Bunge litatunga sheria ili kuzifanya sera za nchi kutekelezeka na mahakama zitaamua mashauri na kutafsiri sheria na kutoa haki,”,
Mbatia alishangazwa na kauli ya Luhanjo kwamba, ni kawaida kwa wizara kuchangisha fedha kwa taasisi zilizo chini yake kwa ajili ya kuandaa na kupitisha bajeti.
“Tunataka wabunge wahoji kwamba, kwa nini hatuna kasma kwenye kila wizara ya kuandaa bajeti? Kwanini Katibu Mkuu awe anachangisha idara za wizara? Je, hakuna kiwango cha gharama za kuandaa bajeti,” alihoji Mbatia.
Alisema kama ni kweli imethibitika kwamba, fedha zilizochangishwa zilikuwa Sh578,599,100 ni wazi kuwa hoja ya wabunge imethibitika.
Mbatia alihoji zaidi akisema: “Kama ni hivyo Luhanjo alikuwa akichunguza nini?”.
Mbatia alisisitiza: “Hadidu za rejea za CAG zipanuliwe ili achunguze kama huo ndio utaratibu unaofuatwa na wizara zote… Luhanjo ametuhakikishia kuwa hilo ni sawa je, ni kweli na halali Serikali kutumia fedha za umma kifisadi kwa kisingizio cha kuandaa bajeti?”.
Alisema Bunge linatakiwa kufanya utafiti mpana ili kutambua ukweli jinsi watumishi wa wizara wanavyoandaa bajeti na kama ikibainika utaratibu unaotumika ni kama wa Jairo, itungwe sheria ya kuweka masharti mapya kuhusu jukumu hilo.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment