Ndege za kivita za NATO zimeshambulia mji wa Sirte, moja ya maeneo ya mwisho yaliyo ngome za Gaddafi, wakati wanajeshi wa serikali ya Libya wakiendelea kuushambulia mji huo.
Wanajeshi wa Baraza la Mpito la Taifa la Libya (NTC) wanakabiliwa na upinzani mkali na wamepeleka vifaru kukabiliana na mashambulio ya kuvizia yanayoendeshwa na wapiganaji watiifu kwa Gaddafi.
Wanajeshi wa NTC wanadhibiti bandari wakati wakisonga mbele kuelekea katikati ya mji wa Sirte - mahali alikozaliwa kiongozi wa Libya aliyeondolewa madarakani.
Raia wamekuwa wakiondoka kutoka mji huo, wakati ambapo kuna uhaba wa maji, chakula na dawa.
Makabiliano makali
Wizara ya ulinzi ya Uingereza imesema majeshi yake ya anga na yale ya NATO yalipata mafanikio katika mashambulio ya siku ya Jumanne katika mji wa Sirte, kwa kuharibu maeneo ya kijeshi, yaliyolengwa yakiwemo maghala ya silaha na risasi.
Pia wameendesha mashambulio katika ghala la magari ya kijeshi ambalo limekuwa likitumika kama moja ya vituo vikuu vya shughuli za kijeshi kwa askari wanaomuunga mkono Gaddafi. Mashambulio ya anga yaliendelea siku ya Jumatano.
Sirte pamoja na mji wa Bani Walid ni maeneo ya mwisho yaliyo chini ya udhibiti wa wanajeshi watiifu kwa Gaddafi. Miji yote miwili imekuwa kitovu cha mapigano makali katika wiki za hivi karibuni.
Maafa
Kwa mujibu wa taarifa moja, wapiganaji 11 wa NTC waliuawa katika mji wa Bani Walid, kufuatia makombora yaliyofyatuliwa Jumatano na wanajeshi wanaomtii Gaddafi.
Raia wengi wameukimbia mji huo, lakini watu wameendelea kuripoti hatari ya kujikuta katikati ya mapigano ya kuwania kuutwaa mji wa Sirte.
Kamanda mmoja katika uwanja wa mapigano amesema upinzani unaoonyeshwa na wapiganaji wa Kanali Gaddafi umekwamisha harakati za wanajeshi wa NTC kusonga mbele kuudhibiti mji wa Sirte.
"Daima kumekuwa na mashambulio ya mizinga na makombora, tunajibu mashambulio hayo kwa silaha nzito lakini hatuwatumii askari wa miguu," Kepteni Walid Khaimej ameliambia shirika la habari la AFP.
"NATO ipo hapa lakini bado haijatosheleza. Wanarusha makombora , lakini tunajibu haraka. Tunahitaji msaada zaidi kutoka NATO."
Hali mbaya ya maisha
Chama cha Msalaba Mwekundu kimeonya kuwa hali ya maisha ya watu katika miji ya Sirte na Bani Walid inazidi kuwa mbaya.
"Hakuna chakula, hakuna umeme. Tunakula mikate tu," Mkaazi mmoja wa Sirte Saraj al-Tuweish ameiambia AFP wakati akiondoka mjini Sirte Jumanne.
"Kwa muda wa siku 10 nimekuwa nikijaribu kutoroka na kila wakati jeshi linatulazimisha kubaki. Leo, mapema asubuhi tulitumia barabara mbaya na tukaweza kutoroka."
chanzo:bbcswahili
No comments:
Post a Comment