Monday 19 September 2011

WABUNDE CHADEMA WAFIKISHWA MAHAKAMANI









WASOMEWA MASHTAKA MATATU LIKIWAMO LA WIZI, WAACHIWA KWA DHAMANA
Waandishi Wetu, Tabora na Igunga
WABUNGE wawili wa Chadema na kiongozi mmoja wa chama hicho wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora kujibu mashtaka matatu kwa pamoja likiwamo la kumshambulia Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario.Mbali na mashtaka hayo kuwakabili watuhumiwa wote, watatu ambao ni Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Kiwanga, Sylvester Mhoja Kasulumbayi (Maswa Mashariki ) na Anwar Kashaga, Kasulumbayi ameongezewa shtaka moja; kumtukana matusi ya nguoni mkuu huyo wa wilaya.

Watuhumiwa hao kwa pamoja, walifikishwa mahakamani hapo jana chini ya ulinzi mkali wa polisi na kusomewa mashtaka hayo, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Thomas Simba.

Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Juma Massanda aliieleza mahakama kuwa katika shtaka la kwanza, Kasumbayi alimtukana matusi ya nguoni mkuu huyo wa wilaya. Alisema alitenda kosa hilo Septemba 15, mwaka huu katika Ofisi ya Ofisa Mtendaji wa Kata ya Isakamaliwa wilayani Igunga.

Alidai mahakamani hapo kuwa siku ya tukio hilo, mbunge huyo wa Jimbo la Maswa Mashariki, alimwambia Fatuma 



Kimario kuwa 'malaya mkubwa, huyu ndiye ningetaka kuzaa naye, mpumbavu mkubwa na DC gani huyu hana akili.' Alisema, jambo hilo lingeweza kusababisha uvunjifu wa amani katika eneo hilo.

Mwendesha mashtaka huyo aliendelea kuieleza mahakama kuwa shtaka la pili hadi la nne linawakabili watuhumiwa wote kwa pamoja. Alieleza kuwa katika shtaka la pili, watuhumiwa hao kwa pamoja walimshambulia mkuu huyo wa wilaya na kumsababishia maumivu kichwani, shingoni na kifuani.

Shitaka la tatu, alisema: “Ni washtakiwa wote kwa pamoja siku hiyo, walimweka chini ya ulinzi, Kimario pasipo halali kwa muda, kosa ambalo ni la jinai.”

Katika shitaka la nne ilielezwa kuwa washtakiwa wote watatu kwa pamoja walifanya kosa la wizi wa maungoni. Alisema kwa pamoja walimwibia Kimario simu ya mkononi yenye thamani ya Sh400,000.

Hata hivyo, washtakiwa wote walikana mashtaka hayo na wako nje kwa dhamana ya Sh5 milioni kila mmoja hadi Oktoba 10, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa gari la polisi saa 3:55 asubuhi na kupelekwa chumba cha mahabusu kabla ya dakika chache baadaye, kupandishwa kizimbani baada ya Hakimu Simba kuingia mahakamani hapo.

Washtakiwa hao kwa pamoja katika kesi hiyo, wanatetewa na wakili Tundu Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki kupitia Chadema.

Baada ya upande wa mshataka kukamilisha kusoma maelezo ya awali, upande wa utetezi uliokuwa ukiongozwa Lissu ulitoa maombi mawili.

Uliiomba mahakama hiyo kuwaruhusu washtakiwa hao kujidhamini wenyewe kwa kuwa wao ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano hivyo hawawezi kukimbia, jingine ni kudhaminiwa na wadhamini lakini wasipewe masharti magumu ya dhamana.

Alisema hilo linatokana na mashtaka hayo kutokuwa makubwa na hayajakataliwa kupewa dhamana kwa mujibu wa Sheria namba 148 ya kanuni za Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Lissu alisema kuwa mashtaka mawili ya kwanza ambayo ni kutumia lugha ya matusi na shambulio adhabu yake ni mwaka mmoja jela, shtaka la kumweka chini ya ulinzi adhabu yake ni kifungo cha miezi sita jela wakati la wizi wa maungoni ni miaka 10 jela.

Katika ombi lake la pili Lissu aliyekuwa akisaidiwa na wakili, Mussa Kwikima aliiomba mahakama hiyo kuanza kusikiliza kesi hiyo kwa kuwa upande wa mashtaka umeshamaliza kupeleleza shauri hilo.

Alisema kwa sababu uchaguzi mdogo unaendelea katika jimbo la Igunga mkoani humo, anaiomba mahakama ianze kusikiliza shauri hilo ili kuepuka kupoteza muda.

Hata hivyo, upande wa mashtaka haukuwa na pingamizi juu ya dhamana kwa washtakiwa lakini ulipinga hoja iliyotolewa na Lissu ya kutaka washtakiwa hao kujidhamini wenyewe.

Masanja ambaye anasaidiana na Wakili wa Serikali, Mugisha Mombeko alisema ingawa Lissu anayaona makosa yanayowakabili washtakiwa hao kuwa ni madogo kulingana na adhabu zake zilizoainishwa katika sheria, alisema kosa la miaka 10 jela si dogo.

Aliitaka mahakama kutoa dhamana kwa washtakiwa hao lakini kwa kupitia wadhamini ili wasipohudhuria mahakamani kuwepo na watu wa kueleza watuhumiwa walipo.

Katika ombi la pili, Masanja aliiomba mahakama kutoanza kusikiliza kesi hiyo jana ingawa upelelezi umekamilika ili kutoa muda wa kuandaa maelezo kwa makini. Hoja hiyo iliungwa mkono na Wakili Mombeko akisema hakuna uhusiano kati ya kesi hiyo na uchaguzi mdogo wa Igunga na kwamba hata kama ingeanza kusikilizwa jana ingepangiwa tarehe nyingine ya kusikilizwa.

Baada ya maelezo ya pande hizo mbili, Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo kwa muda wa dakika 10 kabla ya kurejea tena na kisha kusema kuwa amekubaliana na upande wa mashtaka kuwa ni vizuri washtakiwa hao wakadhaminiwa na watu wengine kwa sababu wasipotokea mahakamani kwa sababu yoyote ile awepo na mtu wa kueleza waliko.

Kuhusu kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo, Simba alisema anakubaliana na upande wa mashtaka akisema kuanza kusikiliza shauri hilo jana, kungeushtukiza upande huo.

Washtakiwa wote walidhaminiwa na watu wawili kila mmoja na kesi hiyo itatajwa tena Oktoba 10, mwaka huu saa 3:00 kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.

Kwa muda wote tangu wawasili katika viwanja vya mahakama, kuingia mahakamani na wakati wa kutoka, washtakiwa hao walikuwa wakinyoosha vidole viwili juu huku wakipungiwa mikono na kushangiliwa na wafuasi wa Chadema waliojitokeza. Baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo wabunge hao waliondoka kuelekea Igunga kuendelea na kampeni.

Wapokewa Igunga kwa maandamano
Baada ya kuwasili Igunga, wabunge hao walipokewa kwa maandamano makubwa yaliyoanzia eneo la mnadani kilometa moja kutoka Igunga Mjini na kuelekea kwenye ofisi za chama hicho zilizoko Barabara ya Singida.

Mapokezi hayo yalitawaliwa na baiskeli, pikipiki na bajaji zilizokuwa zinaendeshwa na vijana ambazo zilitanda barabara nzima mjini hapa.Wabunge hao wakiongozwa na Lissu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Katiba na Sheria wa chama hicho waliwasili majira ya saa kumi na moja jioni.

Kuongeza nguvu ya kampeni
Chama hicho kinatarajia kuongeza kwa nguvu ya mapambano ya kulinyakua jimbo hilo na leo wabunge wake machachari, Halima Mdee, Godbless Lema na Susan Lyimo wanatarajiwa kuwasili hapa leo.

Tayari wabunge wengine wa chama hicho, Regia Mtema, Philipa Mturano, Rabecca Mngodo, Joyce Mukya na Dk Anthony Mbassa wapo hapa wakipiga kampeni.



chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment