Kwa wapenzi wa muziki wa enzi wa Tanzania jina la mpiga
gitaa Dekula Kahanga Vumbi si geni, lakini baba yake hakupenda kabisa apige
gitaa, lakini bahati nzuri alikulia kwa bibi yake katika mji wa Uvira, mkoa wa
Kivu, Jamhuri ya Kongo ambako alikuwa na uhuru zaidi na akaanza kwa kutengeneza
magitaa yake, ambalo lilikuwa likivunjwa kila baba yake alipokuwa akija
kumtembelea bibi yake.Jirani na alipokuwa akiishi kulikuweko na bar inaitwa
Sikiya sosi ambapo palikuweko na bendi ikiitwa Gramick Jazz, bendi
iliyopitiwa na wanamuziki wengi waliokuja Tanzania akiwemo Dr Remmy. Alikuwa
akisikiliza muziki ukipigwa katika hiyo bar na yeye akawa anafuatisha kwenye
gitaa la kutengeza mwenyewe la nyuzi tatu, hatimae bibi yake akamnunulia gitaa
dogo la nyuzi nne ambalo alikuwa naaenda nalo mpaka shule, ambapo mwalimu wake
siku nyingine alikuwa akimwita awatumbuize wanafunzi wenzie. Hatimae akakutana
na jamaa aliyekuwa akipiga katika bendi iliyokuwa ikimilikiwa na mapadri, akawa
anamnunulia sigara huyu jamaa nae akaanza kumfundisha chords mbalimbali za
kupiga gitaa. Aliendelea vizuri hatimae akajiunga na bendi hiyo ya mapadri
iliyoitwa Kyalalo Band akiwa mpiga rhythm. Wanamuziki wa Kyalalo hawakuruhusiwa
kujiunga na bendi zilizo kuwa zinapiga muziki kwenye bar, wala bendi yenyewe
kwenda kupiga kwenye bar, kulikuweko na ukumbi mkubwa wa kanisa na hapo ndipo
walipofanya mazoezi na maonyesho, lakini baadae Vumbi akajiunga na bendi Bavy
National tena kama mpiga rhythm,
na
hapo akakutana na mwimbaji Issa Nundu ambae alikuwa anafanya hospitali na jioni
kujiunga na bendi, hatimae Kyanga Songa ambaye kazi yake ilikuwa Bwana Shamba
nae alijiunga nao.
Katika kipindi hicho wakazi wa Kongo ya Mashariki,
ambako kunazungumzwa kiswahili, walikuwa wakisikiliza na kuzijua bendi nyingi
kutoka Afrika ya Mashariki, bendi kama Tabora Jazz, Mangelepa, Simba wa Nyika,
Mlimani Park zilisikilizwa sana, na nyimbo kama Kassim ilikuwa nyimbo maarufu
wakati huo na hivyo ikawa ndoto ya Vumbi kuwa lazima siku moja waende huko
unakotoka muziki mtamu huo ili nae aweze kushiriki. Katika kipindi hicho Kyanga
Songa na Issa Nundu waliondoka kwenye bendi yao ya Bavi National na kuelekea
Tanzania. Bendi ikatetereka sana, lakini nae wakati huo akawa anahamu sana ya
kuja Afrika Mashariki. Bahati nzuri mtu mmoja Alida Shanga akamjia akiwa
ametumwa na Marehemu Mzee John Luanda aliyekuwa anamiliki Chamwino Jazz kuja
kutafuta wanamuziki toka Kongo, nae akawachukua na wakatua Tandale jijini Dar es
Salaam, na siku waliofika tu na wakaanza mazoezi siku hiyo hiyo. Wakiwa vijana
bado yeye na wenzie watatu walikuja wakiwa na staili ya kuimba na steji show
ambayo wakati huo iliitwa sarakasi, na pia wao ndo kilikuwa kikundi cha kwanza
kuanza kurap katikati ya nyimbo. Waimbaji wakiwa ni Sisko Lunanga, Fanfan
Bwami, na mwenzao mmoja Baposta Kilosho ambae hatimae alirudi Kongo. Recording
ya kwanza ilimuacha Julius Nyaisanga akishangaa vituko vya vijana hawa. Katika
bendi ya Chamwino wakati huo wapiga magitaa walikuwa Vumbi Dekula, Kazembe wa
Kazembe (huyu alikuwa Msukuma ambaye aliishi kwa muda Kongo na alikuwa mpiga
gitaa hodari sana), na Mzee Albert, na hatimae wakamchukua Muhidin ambae alikuwa
mpiga bezi wa Dr Remmy. Siku moja walienda kuomba kupiga na Maquis
Original(lift), wakati huo wakipiga nyimbo za kopi, nyimbo kama Mario, Maze na
kadhalika, hivyo wakazipiga hizo na watu wakafurahi sana na kuwatuza fedha
nyingi, wakachanganyikiwa maana bendi yao ya Chamwino ilikuwa haina mshahara na
si mara moja walitembea kwa miguu toka Buguruni hadi Tandale kwa kukosa mapato.
Japo wakati huo walikuwa wadogo kwa umri na hata umbo walifika mahala marehemu
Kasheba alikuwa anawaita ‘Vimario’, upigaji wao ulikuwa mzuri sana. Nguza
aliwashauri wawe wanakuja kupiga kabla Maquis hawajaanza kupiga. Hivyo wakaamua
kuacha Chamwino, na wakawa wanasindikizana na Maquis, hili lilimuudhi
aliyewaleta na siku moja wakiwa Silent Inn, maafisa wa Uhamiaji walikuja
kuwachukua wakalazwa Central Police na kisha kupelekwa gereza la Keko. Wakiwa
huko walimwandikia Mzee Luanda kuwa wanarudi Chamwino, basi wakaachiwa na kurudi
kusuka upya Chamwino Jazz. Lakini hawakukaa muda mrefu Mzee Makassy akaja
kuwaomba waingie katika bendi yake, wenzake waimbaji wakaenda yeye akabaki
Chamwino, lakini muda si mrefu Nguza akamwambia aandike barua ajiunge na Maquis.
Nae akafanya hivyo na ndio kujiunga rasmi na Maquis kama mpiga gitaa la second
solo. Aliwakuta wanamuziki kama Maneno Uvuruge, Omari Makuka, Keppy kiombile,
Ilunga Lubaba, William Maselenge na wengine wengi. Aliendelea kupiga second
solo hadi siku moja bendi ilikuwa inapiga maeneo ya Ukonga, kwa kawaida Mzee
Lubaba alikuwa anapiga kuanzia saa tatu mpaka saa sita, na kisha Nguza Viking
akiingia na kuendelea .
Wa pili toka kulia na shati jeusi Vumbi, wapili toka kushoto na suruali nyeusi Issa Nundu |
Siku hiyo Nguza hakuonekana Vumbi akaweza kupiga
nyimbo zote za Nguza, na kesho yake akaambiwa afike ofisini akasainishwa rasmi
mkataba wa kuwa mwanamuziki wa Maquis. Baada ya muda mfupi Nguza akaacha bendi.
Na baada ya hapo walirekodi ule
wimbo maarufu wa Makumbele, solo ya wimbo huu ilikuwa awali ikipigwa na Mzee
Lubaba, lakini afya ya mzee Lubaba ilianza kuzorota nae akawa anawafundisha
nyimbo zake wanamuziki wengine, wimbo wa Makumbele alifundishwa Makuka na akawa
anaupiga katika mahonyesho mbalimbali, lakini wakati wa kutaka kurekodi kamati
ya uongozi ya Maquis iliamua Vumbi aufanyie mazoezi na aurekodi. Kurekodi kwa
album ya Makumbele ilitokana na safari ndefu ya bendi ambayo ilichukua miezi
mitatu katika mikoa ya Ziwa, hivyo bendi iliporudi Dar ilikuta sifa ya bendi
imepungua, hivyo walirekodi album ya Makumbele iliyokuwa na nyimbo kama
Tipwatipwa, Ngalula na Makumbele, sifa ya bendi ikarudi juu tena kwa mara
nyingine. Na ni wakati huo ambapo bendi ilihamia katika ukumbi wa Lang’ata KINONDONI
habari yote kwa hisani ya kitineblog
No comments:
Post a Comment