Monday 31 October 2011

SWALI TOKA MWANANCHI

Wanyamapori wetu wataendelea kusafirishwa nje mpaka lini?

GAZETI hili katika ukurasa wake wa kwanza, limechapisha habari inayoeleza uovu wa baadhi ya wafanyabiashara kusafirisha nje ya nchi kinyemela wanyamapori hai kutoka Hifadhi ya Wanyamapori ya Saunyi wilayani Kilindi.

Habari hiyo inaeleza kuwa wanyama hao wamekuwa wakiwindwa na kukamatwa kwa njia ya wizi kisha kusafirishwa kwa magari wakiwa hai, wakisaidiwa na baadhi ya maofisa wa wanyamapori wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Tayari vitendo hivyo vimewashtua baadhi ya viongozi wilayani humo akiwamo Mbunge wa Wilaya hiyo, Beatrice Shelukindo ambaye amelalamikia kuwa vitendo hivyo vinafanywa na maofisa wanyamapori wasiokuwa na uzalendo na nchi yao.

Katika Kikao cha Madiwani wa Wilaya ya Kilindi kilichofanyika juzi, suala hili pia lilibuka na Diwani wa Kata ya Saunyi, Michael Lesindiyo Yeiyoo, alisema ni jambo la kusikitisha kuona kuwa wanyamapori mbalimbali waliokuwa katika Mbuga ya Saunyi, hivi sasa wapo hatarini kutoweka kutokana na kasi ya uwindaji wa kijangili na kusafirishwa nje ya nchi.

Diwani huyo, alisema jambo la kushangaza ni kuwa wawindaji wanapohojiwa na walinzi wa vijiji vya Kata ya Saunyi wamekuwa wakidai kwamba wanavyo vibali vilivyotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii ambavyo vinawaruhusu kuwinda mnyama yeyote bila kubughudhiwa na mtu wa ngazi ya wilaya, kata na hata kijiji.

Kashfa hii inakuja wakati Agosti mwaka huu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipiga marufuku biashara ya kukamata na kusafirisha wanyamapori kwenda nje ya nchi.

Pinda alisema eneo la wanyamapori utaratibu, usimamizi na hata namna biashara yenyewe inavyofanyika, linahitaji kutazamwa upya.

Katika Bunge hilo la Bajeti, serikali ilitangaza kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Wanyamapori nchini, Obed Mbangwa na watumishi wengine wawili wa Wizara ya Maliasili na Utalii ili kuruhusu kufanyika kwa uchunguzi wa tuhuma za kutoroshwa kwa wanyamapori 116 na ndege 16 kwenda nje ya nchi.

Wanyamapori hao wanadaiwa walikamatwa katika hifadhi za taifa na kutoroshewa nje ya nchi Novemba 26 mwaka 2010 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Tunachukua nafasi hii kulaani vikali vitendo vya wanyamapori kusafirishwa nje ya nchi wakati tayari serikali ilishapiga marufuku.

Tunaamini kuwa wanaofanya mchezo huu ni watu wanaofahamika na maofisa wa wanyamapori na pengine ni viongozi wa juu serikalini.

Ni wazi kutokana na tukio hili la Kilindi, Wizara ya Maliasili na Utalii, inatakiwa kufanya mabadiliko makubwa ikiwamo kuwaondoa haraka maofisa wake wa wanyamapori wasiokuwa waaminifu.

Inaonyesha kwamba Idara ya Wanyamapori haina tena uwezo wa kulinda wanyamapori dhidi ya majangili. Tunayo mifano hai ni hivi karibuni tulishuhudia faru walioingizwa nchini kutoka Afrika Kusini mmoja aliuawa wakati Rais Jakaya Kikwete alishaagiza wapewe ulinzi wa kutosha.

Tunahoji, Waziri wa Maliasili na utalii na timu yake ya watumishi wako wapi katika kuhakikisha kuwa wanazui mchezo huu mchafu


No comments:

Post a Comment