WAZIRI wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo ameivunja Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC), wakati ambao bodi hiyo ilikuwa ikisubiri kupokea ripoti ya ukaguzi uliofanywa na Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ukilenga kubaini tuhuma za kuwapo kwa ufisadi katika shirika hilo.
Msingi wa uchunguzi ndani ya CHC, ni maombi ya Bodi ya shirika hilo hodhi kwa CAG, kufuatia kuwapo kwa tuhuma kwamba menejimenti yake ilihusika na vitendo vya ufisadi, hivyo kusababisha kusimamishwa kwa Kaimu Mkurugenzi wake, Methusela Mbajo.
Ofisi ya CAG ilifanya uchunguzi kwa kutumia kampuni ya kimataifa ya ukaguzi wa hesabu ya Ernst&Young, ukaguzi ambao pia ulilenga kubaini tuhuma dhidi ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), inayoongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
Katika Mkutano wa Nne wa Bunge, Mkulo aliingia katika mvutano na Zitto baada ya waziri huyo kumtuhumu mbunge huyo na Kamati yake kwamba walihongwa ili kutetea nyongeza ya muda wa CHC, tofauti na mawazo ya Serikali ya kutaka kufutwa kwa shirika hilo.
Baada ya tuhuma hizo, Zitto aliapa bungeni kwamba kama uchunguzi utathibitisha yeye au wajumbe wa POAC wamehongwa, angejiuzulu uenyekiti na ubunge na kumtaka Waziri Mkulo nae atoe kiapo chake bungeni kama atajiuzulu akibainika amefanya ufisadi ndani ya CHC.
Mkulo akijibu swali hilo alishindwa kula kiapo na Spika wa Bunge, Anne Makinda akamkumbusha kuhusu kula kiapo kama atajiuzulu, lakini waziri huyo aligoma kufanya hivyo.
Lakini wakati CAG akiwa katika hatua za mwisho kukamilisha ripoti yake ambayo kimsingi ilipaswa kukabidhiwa kwa bodi ya CHC, uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa Mkulo amevunja bodi hiyo kabla ya kumaliza muda wake wa nyongeza ambao ulipaswa kumalizika Desemba 31, mwaka huu.
Uhai wa Bodi ya CHC
Awali bodi ya CHC ilikuwa imalize muda wake Juni 30 mwaka huu, lakini Mkulo aliiongezea muda hadi Desemba 31, mwaka huu na barua ya hatua hiyo ilitumwa kwa wajumbe wa bodi hiyo kuwajulisha hatua hiyo ya waziri Julai 29, 2011.
Hata hivyo, ghafla Mkulo alibadili uamuzi wake Oktoba 10, 2011, kwa kumwandikia Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CHC kwamba awaarifu wajumbe wa bodi kuhusu uamuzi huo.
Sehemu ya barua kutoka Wizara ya Fedha kwenda CHC ambayo Mwananchi imeiona inaeleza: “Nimeelekezwa nikuarifu kwamba Waziri wa Fedha, Mh. Mustafa H. Mkulo (Mb), ametengua uamuzi wake wa kuongeza muda wa Bodi ya CHC hadi tarehe 31 Desemba, 2011 au hapo Rais atakapoteua Mwenyekiti wa Bodi hiyo kuanzia tarehe ya barua hii (10, Oktoba, 2011).”
Barua hiyo iliyosainiwa kwa niaba ya Katibu Mkuu Hazina na Geoffrey Msella pia inasema; “Kwa barua hii unatakiwa kuwaandikia barua waliokuwa Wajumbe wa Bodi ukiwashukuru kwa michango yao kwa Shirika hili katika kipindi walichotumikia CHC.”
Kufuatia barua hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CHC, Dome Malosha siku hiyo hiyo ya Oktoba 10, 2011 aliwaandikia barua wajumbe hao wa Bodi akiwaarifu kuhusu uamuzi wa Waziri Mkulo kuvunja bodi hiyo.
Ukaguzi wa CAG
Uchunguzi wa Mwananchi umebiani kuwa hatua ya Mkulo kuvunja bodi ya CHC ilifanyika muda mfupi tu, tangu alipojibu hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utuoh kuhusu kile ambacho kinaonekana kuwa ni matokeo ya awali ya ukaguzi uliofanywa na Ernst & Young.
Uchunguzi wetu unaonyesha kuwa kulikuwa na mawasiliano baina ya Mkulo na Utouh kati ya Oktoba 6 na 8, 2011, na baadaye kuvunjwa kwa bodi Oktoba 10.
Oktoba 8, 2011, Mkulo alimwandikia barua Utouh akikanusha kwamba hahusiki na ufisadi wowote ndani ya CHC, kauli inayothibitisha kwamba alitajwa katika taarifa yake hiyo.
Katika barua hiyo ambayo pia Mwananchi imeiona, Mkulo anakanusha kile alichosema kuwa ni tuhuma za kuhusishwa na uuzwaji wa mali za CHC kinyume cha sheria.
Barua hiyo ya Mkulo kwenda kwa CAG ina kumbukumbu Namba TYC/B/70/03 na kichwa cha habari, YAH: UKAGUZI WA CONSOLIDATED HOLDING CORPORATION ikirejea mazungumzo ya simu baina ya viongozi hao wawili Oktoba 7, mwaka huu, pia ujumbe mfupi wa simu kutoka kwa Utouh kwenda kwa Mkulo Oktoba 6, 2011.
Waziri Mkulo katika barua huyo alisema: "Napenda kuthibitisha niliyosema kwenye simu, kwa maandishi kwamba, mimi kama Waziri wa Fedha sijawahi kutoa kibali kwa mwenyekiti wa Bodi ya CHC, kumpa madaraka ya kuuza ama kiwanja au nyumba zinazomilikiwa au kutunzwa na CHC bila kufuata taratibu za zabuni au Sheria ya Manunuzi".
Aliendelea Mkulo akisema, "Kama mwenyekiti wa bodi aliamuru Kaimu Mkurugenzi Mkuu na Bodi ya Wakurugenzi kuuza kiwanja cha shirika bila kufuata taratibu za zabuni, alifanya hivyo kwa ridhaa yake mwenyewe na si kwa maagizo ya Waziri wa Fedha".
Waziri Mkulo alifafanua," Wizara ina utaratibu maalum wa kushughulikia masuala yote yanayohusu mashirika ya umma. Kisheria, huanzia kwa Msajili wa Hazina, kupitia kwa Katibu Mkuu-Hazina (PST/PMG) hadi kumfikia waziri wa fedha kwa uamuzi".
Aliongeza, "Hivyo, utaratibu uliotumiwa na mwenyekiti wa Bodi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CHC ni kinyume na kanuni za utendaji kazi ndani ya Wizara ya Fedha na pia ni kinyume na kanuni za manunuzi".
Katika aya ya mwisho ya barua hiyo, Mkulo anasisitiza:, "Nakushukuru sana kwa kunijulisha jambo zito ambalo sikuwa nalifahamu. Natumaini kwa maelezo haya ya maandishi, ofisi yako sasa inaweza kuendelea kukamilisha ukaguzi wa CHC".
Nakala ya barua hiyo, kwa mujibu wa uchunguzi huo zimekwenda kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo na Mwenyekiti wa Bodi ya CHC iliyovunjwa, Profesa Hamis Kahigi ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
Pia nakala imekwenda kwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Ramadhani Khijjah na Geofrey Msella ambaye ni Msajili wa Hazina.
Kauli ya Mkulo
Uamuzi wa Mkulo kuvunja bodi hiyo umezuai hisia kwamba umesukumwa na taarifa za CAG zinazomuhusisha na uuzaji wa mali za CHC.
Lakini, Mkulo alijitetea akisema uamuzi huo ulitokana na ukweli kwamba tayari alikwishamwandikia barua Rais Rais Jakaya Kikwete kuhusu kuisha kwa muda wa bodi tangu Juni 30, hivyo kinachosubiriwa ni mkuu huyo wa nchi kuteua mwenyekiti mpya wa bodi.
Mkulo alisema hakuvunja bodi na kusisitiza kwamba, tayari yenyewe ilikwishamaliza muda hivyo haikuwa sahihi iendelee kukaa madarakani.
Mmoja wa wajumbe wa bodi hiyo iliyomaliza muda wake alikiri bodi yao kumaliza muda, lakini akahoji mantiki ya Mkulo kuivunja wakati huu ambao ripoti ya ukaguzi inakaribia kutoka.
"Nikweli lazima tumtendee haki waziri. Hakuvunja bodi bali muda ulikuwa umekwisha na sisi tulipaswa kuondoka tangu Juni 30, lakini swali ni moja tu, kwanini waziri kavunja bodi juzi badala ya kusubiri tukabidhiwe ripoti?," alihoji mjumbe huyo kwa shariti la kutotajwa jina.
CAG astuka
CAG Utouh alipoulizwa jana kwa njia ya simu kuhusu suala hilo, alistuka na kusema hadi sasa ripoti haijakamilika kwani bado zinakusanywa taarifa nyingi muhimu ili matokeo yake yasiwe na shaka yoyote.
Utouh ambaye anasifika kwa utendaji makini, alisema hadi sasa uchunguzi huo umekamilika kwa asilimia 90 na kusisitiza, "Tunachokifanya ni kukusanya data zote muhimu kwa umakini".
Aliongeza, "Unajua hili jambo ni zito sana, hivyo tunalifanya kwa umakini mkubwa. Tunataka ripoti yetu ikija kutoka iwe iko based on facts. Sasa, ni suala tu la kuwa wavumulivu ripoti itatoka tu".
Utouh alipoulizwa kuhusu barua ya Mkulo ya kujitetea alicheka kidogo, "Haaahaa!" Kisha akahoji:, "Wewe umeiona wapi? Subirini matokeo, kuweni wavumilivu".
Alipoulizwa Zitto kuhusiana na sakala la CHC, alisema : Kwa sasa siwezi kuzungumza hadi kesho (leo) nitakapokutana na waandishi wa habari Dar es Salaam,” alisema.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment