Askari
wa Bunge wakiwa wamebeba jeneza la aliyekuwa mbunge wa viti maalum
(Chadema), Regia Mtema, wakati wa salamu na rambirambi za kumuaga rasmi
kiserikali zilizofanyika viwanja vya karimjee jijini Dar es Salaam
jana.Mbunge huyo anatarajiwa kuzikwa leo alasiri nyumbani kwao Ifakara
mkoani Morogoro.Picha na Silvan Kiwale
MAKUNDI
mawili yanayopinga ya wanachama wa Chadema jana nusura yazichape
kavukavu yalipokuwa katika msiba wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu kwa
tiketi ya chama hicho, Regia Mtema huko Ifakara, kutokana na chuki na
makovu ya uchaguzi wa wa ndani wa chama hicho wa mwaka 2010.
Wakati
hayo yakitokea huko Ifakara, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe alitumia fursa aliyopewa wakati wa kuaga mwili wa
mbunge huyo kuipiga vijembe Serikali huku Mwenyekiti Mstaafu wa chama
hicho, Bob Makani akianguka ghafla.
Marehemu Regia ambaye
alifariki dunia Jumamosi iliyopita kwa ajali ya gari iliyotokea Ruvu,
Pwani, unatarajiwa kuzikwa leo Ifakara.
Katika tukio la Ifakara,
mgogoro baina ya kambi mbili zilizotokana na makovu ya uchaguzi huo wa
ndani kati ya wafuasi wa marehemu na ya Mbunge wa Viti Maalumu, Susan
Kiwanga ulisababisha kutimuliwa msibani hapo kwa Mwenyekiti wa Chadema
Wilaya ya Kilombero, Salum Ngozi.
Ilielezwa kwamba baada ya Ngozi
kufika msibani hapo juzi majira ya saa moja usiku na kusalimiana na
viongozi wa Serikali, alifuatwa na baadhi ya makada wa chama hicho
wakimtaka aondoke eneo hilo jambo ambalo aliligomea. Wafuasi hao wa
Chadema waliamua kutumia nguvu kumwondoa hali iliyowalazimu polisi
waliokuwa eneo hilo kuingilia kati. Askari walimtoa mwenyekiti huyo na
kumpeleka katika Kituo cha Polisi Wilaya.
Hiyo ilikuwa mara ya
pili kwa Ngozi kutimuliwa katika msiba huo. Mara ya kwanza ilikuwa juzi
na kumlazimu Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Francis Miti kuingilia
kati.
Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Ngozi alikiri kutokea vurugu
hizo msibani na kudai kwamba, alifanyiwa fujo na kikundi cha watu
aliowaita wahuni na kwamba amefungua kesi ya kufanyiwa vurugu katika
Kituo cha Polisi Wilaya ya Kilombero na kwamba baada ya kumalizika kwa
mazishi atasimamia suala hilo ili haki itendeke.
Naibu Katibu
Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe mbali na kukiri kuufahamu mgogoro huo,
alisema asingependa kuzungumzia suala hilo sasa wakati watu bado
wanaendelea na msiba.
Mbowe aipiga vijembe Serikali Jijini Dar es Salaam, tukio la kuaga mwili wa marehemu Regia liligeuka jukwaa la siasa baada ya Mbowe na Makinda kupiga siasa.Mbowe
alitumia msiba huo kutoa dukuduku lake juu ya shughuli za chama chake
kisiasa na kiutendaji wakati akitoa salaam za rambirambi kwa
marehemu.Mbowe aliirushia kombora Serikali na vyama vingine vya upinzani
kuhusu mwenendo wa Chadema kuendesha siasa katika vyuo vya elimu ya juu
akisema ni mpango maalumu kuwanoa wanasiasa mahiri.
Aliishauri
Serikali na vyama vingine vya siasa kuiga utaratibu huo wa Chadema
akisema unasaidia kukuza vipaji na kuwaandaa viongozi makini kwa kuwapa
nafasi vijana kushiriki katika uongozi.
“Kuna jambo moja ambalo
ningependa Serikali, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vingine
walitafakari na wasilibeze hili. Viongozi huandaliwa na viongozi makini
hawazuki tu,” alisema na kuongeza;
“Naeleza hivyo maana mara
nyingi tumekuwa hatueleweki na tumekuwa tukibezwa. Sisi tunatambua
viongozi wa baadaye kisha tunakuza vipaji na kutoa fursa za nafasi za
uongozi kwa vijana.”
“Vijana lazima waandaliwe kimaadili na ndiyo
maana tuliingia vyuo vikuu lakini tukatafsiriwa kuwa ni wakorofi na
wachochezi wa vurugu. Lakini leo tumepata viongozi wazuri vijana kwa
njia hiyo kutoka vyuoni kama vile Mheshimiwa Zitto (Zuberi Kabwe, Mbunge
wa Kigoma Kaskazini), Mnyika (John Mbunge wa Ubungo, Mdee
(Halima-Mbunge wa Kawe), Silinde (David Mbunge wa Mbozi) na Mtema (Regia
Marehemu).
“Hawa tuliwaandaa, hawakuzuka. Rai yangu kwa Serikali
na kwa wazazi ni kwamba vijana hawa wakifanya siasa tusiwakwaze na
kuwafukuza, bali tuwalee.”
Spika Makinda katika kile
kilichoonekana kama ni kumjibu Mbowe, alitumia fursa hiyo kufafanua
uendeshaji wa shughuli za Bunge akisisitiza kwamba linaendeshwa kwa
kanuni na wala si kufurahisha watu. Alimsifia marehemu Mtema kwamba
alikuwa akizijua vyema kanuni za Bunge: “Bunge huendeshwa kwa kanuni na
si kwa matakwa tu ya kufurahisha watu. Yeye marehemu alizijua kanuni
ndiyo maana hata wakati alipokuwa akikosea alikuwa tayari kuomba radhi.”
Mzee Makani aanguka Hata
hivyo hafla hiyo iliingia dosari baada ya Makani kuanguka muda mfupi
baada ya kuuaga mwili wa marehemu. Baada ya tukio hilo, alibebwa na
kupelekwa pembeni ambako alipepewa kwa takriban dakika tano kisha
kurejea katika hali yake ya kawaida na kurudi kwenye kiti chake.
Baadaye
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia ambaye alikuwa mmoja wa watu
waliokuwa wakimpatia Mzee Makani huduma ya kwanza aliwaambia waandishi
wa habari kuwa alianguka baada ya kuishiwa nguvu ghafla.
“Sasa anaendelea vizuri na amerudi kushiriki kumuaga mpendwa wetu katika safari yake hii ya mwisho,” alisema Mbatia.
Kafulila ashangiliwa Mbunge
wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila jana alishangiliwa kwa
makofi baada ya kutangazwa kuwa mmoja wa wabunge walioteuliwa na Ofisi
ya Bunge kuwamo katika msafara kusindikiza msiba huo akiwakilisha chama
chake.
Baada ya kiongozi wa shughuli hiyo, Ofisa Mwandamizi wa
Ofisi ya Bunge, Saidi Yakub kumtaja Kafulila baadhi ya waombolezaji
walishangilia kwa makofi, vicheko vya chini kwa chini na minong’ono ya
hapa na pale.
Hatua hiyo ya waombolezaji inatokana na hali ya
kisiasa ilivyo kati ya Kafulila na chama chake hicho ambacho mwishoni
mwa mwaka jana kilitangaza kumvua uanachama hatua ambayo ameipinga
mahakamani. Kama ikitekelezwa, itamvua ubunge.
mwananchi |
|
No comments:
Post a Comment