Wednesday 8 February 2012

Bungeleo- Tusipojadili mgomo watu watatushangaa

BUNGE limesema, kama litaendelea kukaa kimya kuhusu mgomo wa madaktari wakiwemo madaktari bingwa, litaonekana ni la ajabu na watu watalishangaa.

Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, amekiri leo bungeni mjini Dodoma kuwa, jambo hilo ni la dharura na muhimu kwa umma.

Ametoa msimamo huo baada ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM) kuomba Bunge lijadili jambo hilo kama jambo la dharura.

Tangu kuanza kwa Mkutano wa Sita wa Bunge Januari 31, Serukamba ni Mbunge wa sita kuomba Bunge liujadili mgomo wa madaktari unaoendelea nchini.

Kwa mujibu wa Ndugai, mgomo wa madaktari ni jambo la dharura kwa vigezo vyote, na kwamba, ukiacha vita, kwa suala la dharura hilo linafuatia.

Amesema, kwa hali ilivyo, wabunge wakimaliza Mkutano wa Bunge unaoendelea na kuondoka Dodoma bila kuzungumzia mgomo huo, wananchi watalishangaa.

“Ni vigumu sasa meza kukaa kimya kwa suala hili” amesema Ndugai na kuitaka Kamati ya Uongozi ya Bunge ikutane kwenye ukumbi wa Spika ili kuona namna ya kuishauri Serikali kuhusu mgomo huo unaoathiri afya za wananchi.

Spika wa Bunge, Anne Makinda jana alizuia wabunge kujadili mgomo wa madaktari wakiwemo madaktari bingwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Makinda alikuwa anamjibu Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM) aliyeomba Bunge lisitishe shughuli nyingine na kujadili mgomo wa madaktari bingwa Muhimbili kwa kuwa unaathiri afya za wananchi.

Zambi alitumia kifungu cha 47 na 48 cha Kanuni za Bunge fasili ya pili na tatu na kunukuu taarifa ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwamba madaktari bingwa wamegoma hivyo afya za wagonjwa ni mbaya sana.

Mbunge huyo aliomba Bunge lijadili hali hiyo kama jambo la dharura kwa kuwa haliwezi kuendelea na shughuli nyingine wakati hali ya afya za Watanzania inazidi kuwa mbaya.

Aliomba wabunge wamuunge mkono, Serikali itoe tamko, na akahoji kwa nini kuna kigugumizi kuwalipa madaktari.

Makinda alisema, wabunge wanalishughulikia vibaya suala hilo na akawataka wawe watulivu wanaposhughulikia mambo makubwa kama hayo.

“Waheshimiwa wabunge tuwe watulivu tunaposhughulikia mambo makubwa…hili ni suala kubwa sana, sana, sana” amesema Makinda.

“Kwa kutumia busara ya kiti, hili suala siruhusu mpaka kamati yangu irudi” amesema.

Baada ya Makinda kutoa uamuzi huo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), aliomba mwongozo wa Spika, na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, aliomba kutoa taarifa, Spika alikataa.

Jumapili iliyopita Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii ilianza kuzungumza na wadau wa sekta ya afya ili kutafuta namna ya kumaliza mgomo wa madaktari.

Februari tatu mwaka huu, Bunge liliiagiza kamati hiyo izungumze na Serikali na madaktari ili kumaliza mgogoro huo.

Naibu Spika wa Bunge, Ndugai ameitaka kamati hiyo ifanye kazi hiyo haraka na itoe taarifa kuhusu yaliyojiri kwenye mazungumzo hayo na ushauri wa Bunge kwa pande husika.

Kwa mujibu wa Ndugai kamati hiyo ilitarajiwa kukutana na Katibu Mkuu Utumishi, na itakutana pia na Baraza la Madaktari, Baraza la Wafamasia, Uongozi wa madaktari walio katika mafunzo kwa vitendo, na Jumuiya ya Madaktari.

Wabunge wameelezwa kuwa, kamati hiyo pia itakutana na Umoja wa Madaktari, Kamati ya Madaktari Bingwa, Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Uongozi wa Kitengo cha Mifupa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI), na uongozi wa hospitali za rufaa KCMC, Mbeya.

Kwa mujibu wa Ndugai, kamati hiyo pia itakutana na uongozi wa hospitali za Ocean Road, Temeke, Mwananyamala, Amana za Dar es Salaam, uongozi wa madaktari mbadala kutoka jeshini, chama cha wauguzi, uongozi wa Tughe, na wadau wengine wa sekta ya afya.

Bunge limewaruhusu wabunge wengine ambao si wajumbe wa kamati hiyo kuhudhuria vikao vya kamati na pande husika, na kuchangia.

Ndugai alisema , baada ya kamati ya Bunge kuwasilisha taarifa kuhusu mazungumzo na pande husika, Mbunge yeyote ambaye atahitaji mjadala ataruhusiwa kuwasilisha hoja mahsusi.

Kiongozi huyo wa Bunge ameiomba Serikali na madaktari watoe ushirikiano kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii.

toka:habarileo

No comments:

Post a Comment