Ghana siku ya Jumapili ilifuzu kuingia nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa kuishinda Tunisia magoli 2-1, katika muda wa ziada.
Kipindi cha kawaida cha dakika 90 kilipokwisha, timu hizo zilikuwa sare ya 1-1.
Bao la ushindi la Ghana lilifungwa na Andre 'Dede' Ayew.
Katika historia ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, Tunisia haijawahi kuishinda Ghana.
Black Stars sasa wana matumaini ya kuendelea katika mashindano hayo na kupata ubingwa baada ya subira ya miaka 30, na watakutana na Zambia katika nusu fainali itakayochezwa uwanja wa Bata, siku ya Jumatano, tarehe 8 Februari, na ikiwa ni nusu fainali ya kwanza.
Mali na Ivory Coast nao watapambana katika nusu fainali ya pili siku ya Jumatano, katika uwanja wa Libreville.
Mali ilifuzu kuingia nusu fainali baada ya kuwashinda wenyeji Gabon 5-4 katika kupiga mikwaju ya penalti, baada ya mechi kumalizika kwa sare ya 1-1, na mabao kukosekana hata katika muda wa ziada.
Bao la Eric Mouloungui lilikuwa limewatia matumaini wenyeji Gabon, ambao mwaka huu wamekuwa wakishirikiana na Equatorial Guinea kuandaa mashindano ya mwaka huu.
Lakini kutangulia sio kufika, na Tidiane Diabate aliweza kuisawazishia Mali, zikiwa zimesalia dakika tano tu kabla ya mechi kumalizika.
Kwa kushindwa kufungana katika muda wa ziada, ilikuwa ni pigo kubwa wakati wa mikwaju ya penalti, Pierre-Emerick Aubameyang aliposhindwa kuifungia Gabon bao.
Gabon hawajawahi kufuzu kufika nusu fainali za mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.
Idhaa ya Kiswahili ya BBC, ikishirikiana na redio washirika, itakutangazia nusu fainali kati ya Mali na Ivory Coast kutoka mjini Libreville, Gabon, katika matangazo maalum ya Ulimwengu wa Soka.
Charles Hilary vile vile atakutangazia mechi ya fainali ya mashindano hayo.
chanzo:bbcswahili
No comments:
Post a Comment