Mtuhumiwa akiwa hoi baada ya kichapo.
Mama aliyebakwa.
MAUAJI ya kinyama yametokea Iringa baada ya kijana Ambokile Mbwanji (28), mkazi wa Mkwawa katika Manispaa ya Iringa, kumchoma kisu na kusababisha kifo cha Costantino Matatala (50), mchana wa Jumatano iliyopita.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, Mzee Matatala aliuawa alipokuwa akijaribu kusaidia kuamulia ugomvi kati ya muuaji huyo na dada yake, Anna Mbwanji, mama yake na pamoja na watu wengine wawili.
Wanafamilia hao walikuwa katika mgogoro mzito ambapo mtuhumiwa alikuwa akiwatuhumu kumzuia kumrithi mama yake mzazi baada ya baba yao kufariki dunia.
Imeelezwa kuwa kijana huyo aliyekuwa akiishi Sumbawanga, alirejea mjini Iringa mwaka 2009 ambapo alikuta taarifa za kifo cha baba yake mzazi lakini hakuonesha kuguswa na msiba huo.
Baada ya siku chache alianza vituko na kujigeuza kuwa yeye ndiyo baba katika nyumba hiyo huku akitoa amri mbalimbali kama alivyokuwa akianya marehemu baba yake enzi za uhai wake.
Akizungumza na gazeti hili, mmoja kati ya wanafamilia ambaye ni dada wa mtuhumiwa, Anna alisema kuwa mdogo wake Ambokile alijigeuza kuwa baba wa familia kwa kumshurutisha mama yao mzazi ampe ‘huduma’ kama alivyokuwa akimpa baba yao, hali iliyosababisha familia kumkalisha kikao na kumkanya juu ya tabia hiyo chafu.
Hata hivyo, alisema katika tukio la wiki iliyopita, kijana huyo alivuta bangi na kunywa pombe kupita kiasi tangu asubuhi hadi saa 8 mchana ambapo alifika sehemu mama yake anayofanyia biashara na kuanza na kutamka wazi uhusiano anaotaka kati yake na mama yake.
Akasema asipokubali basi aanze kusali mara ya mwisho kabla hajamuua na ndipo alipomvamia mama huyo.
Anna aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, alilazimika kukimbilia kituo cha polisi kwenda kutoa taarifa lakini wakati anarejea, akapata habari kuwa mdogo wake tayari amemuua kwa kisu mzee Matatala.
Naye mama mzazi wa kijana huyo (Jina tunalihifadhi) alisema: “Kabla ya kumuua mzee huyo, alitaka kumuua kwa kisu mdogo wake wa kike na wakati akimfukuza ili amchome kisu, alianguka na kisu kuvunjika.
“Akarudi na kwenda dukani kununua kingine kisha kurudi eneo la tukio akitaka kufanya mauaji lakini shemeji yake aliokota mawe na kuanza kumrushia hadi alipokimbia.”
Alifafanua kuwa kutokana na vurugu alizomfanyia na kelele nyingi zilizokuwepo sehemu hiyo, wakazi wa eneo hilo walijitokeza kutoa msaada, akiwemo Matatala na kuanza kumfukuza kijana huyo ambaye alikuwa na kisu mkononi huku wananchi wakipiga kelele za ‘mwizi’ na ndipo alipomchoma kisu mzee huyo.
Aliongeza kuwa, licha ya mzee huyo kuchomwa kisu, alimng’ang’ania kijana huyo hadi wananchi walipofika na kuanza kumshambulia kwa mawe na fimbo hadi alipopoteza fahamu na kuja kuchukuliwa na polisi.
Akithibitisha kutokea kwa mauaji hayo, Diwani wa Kata ya Mkwawa, Thobias Kikula amesema kuwa licha ya kijana huyo kumuua mzee huyo, bado alitaka kusababisha mauaji kwa ndugu zake zaidi ya watatu, akiwemo mama yake mzazi na kuwa ushirikiano wa wananchi wa eneo hilo na jeshi la polisi ulifanikiwa kunusuru damu zaidi kumwagika.
Ofisa mmoja wa polisi mkoa wa Iringa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na akasema wanamshikilia mtuhumiwa licha ya kuwa amelazwa katika hospitali ya mkoa.
toka:amani
No comments:
Post a Comment