NI KATIKA KUONYESHA ALIVYOMPA MAELEKEZO KUNUNUA JENGO LA UBALOZI NCHINI ITALIA | Send to a friend |
Wednesday, 29 February 2012 21:21
|
Na Mwandishi Wetu
ALIYEKUWA Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Rais Jakaya Kikwete alitia saini kuidhinisha bei ya jengo la ubalozi wa Tanzania huko Italia hivyo kumpa nguvu ya kisheria ya uwakilishi katika ununuzi wake. Mahalu alidai mahakamani hapo jana kuwa Kikwete alikubali bei ya Euro 3,098,741.58 kwa ajili ya ununuzi wa jengo hilo na alitetea uamuzi wake huo alipoliambia Bunge Agosti 3, 2004.
“Wakati wa Mkutano wa 16 wa Bunge, Kikao cha 39 kilichofanyika Agosti 3, 2004, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Jakaya Kikwete alithibitisha kuwa jengo hilo liligharimu Euro 3,098,741.58 kwa kuanzia,” alisema Mahalu na kuendelea:
“Mheshimiwa hili linaweza kuthibitika ukisoma kumbukumbu za Bunge za Kitabu cha mwaka 2004 ukurasa wa 169 aya ya pili. Mwaka 2001/2002 Wizara ilinunua jengo Roma kuondokana na adha ya kupanga nyumba za watu na kulipa kila mwaka. Wizara ya Ujenzi kila mwezi. Machi 16, 2002 ilitoa hundi ya kwanza ya Euro700 milioni kati ya Euro 3,098,741.58,” alisema.
Profesa Mahalu ambaye alitinga mahakamani huku akiwa na kabrasha kubwa la vielelezo, aliyaeleza hayo mbele ya Hakimu Mfawidhi, Ilvin Mgeta wakati akiendelea kutoa utetezi wake dhidi ya kesi inayomkabili ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2,065,827.60.
Mahalu ambaye alikuwa akiongozwa na Wakili wake, Mabere Marando alitoa nyaraka mbalimbali zilizokuwa zimejaa kwenye kabrasha hilo zikionyesha hatua mbalimbali za mchakato wa ununuzi wa jengo hilo la ubalozi ikiwemo barua ya kwanza iliyokuwa ikionyesha mchanganuo wa ununuzi wa jengo alizozipeleka serikalini.
Profesa Mahalu alidai kuwa Septemba 2001, akiwa Balozi wa Tanzania, Italia alipewa nguvu ya kisheria ya uwakilishi (Special power of Attorney) ya ununuzi wa jengo hilo la ubalozi na Kikwete ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. “Aliniagiza kununua jengo hilo la ubalozi lililopendekezwa na Serikali na Machi 24, 2004, nilimwandikia barua Kikwete na kwenye barua hiyo niliambatanisha nyaraka za ununuzi wa jengo hilo baada ya kulinunua,” alisema Balozi Mahalu. Profesa Mahalu alidai kuwa licha ya kumwandikia Kikwete, pia aliipeleka barua hiyo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Mhasibu Mkuu wa Serikali, Waziri wa Ujenzi, pamoja na kwa Waziri wa Fedha. Aliendelea kudai kuwa baada ya kuandika barua hiyo na kuiambatanisha na nyaraka hizo za ununuzi wa jengo hilo, hakuwahi kuhojiwa juu ya ununuzi huo. Wakili Marando akimwongoza Mahalu, alimwuliza juu ya ushahidi uliotolewa na shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka, Steward Migwano Aprili 23, 2008 pamoja na vielelezo vya ushahidi kuhusu ununuzi wa jengo hilo kama unalingana au haulingani na wake. Akijibu swali hilo, Profesa Mahalu alisema unalingana. Wakili Marando aliendelea kumwuliza Profesa Mahalu kama ushahidi wa shahidi wa tano wa upande wa mashtaka, Isdory Kyando uliohusu gharama za bei ya ununuzi wa jengo hilo la ubalozi kama zilikuwa zinaoana au zinatofautiana na za ushahidi wake. Profesa Mahalu akijibu swali hilo, alidai kuwa zinatofautiana kwenye bei rasmi yaani na kwamba kulikuwepo na mikataba miwili ambayo Serikali iliridhia yaani mmoja wa bei rasmi na mwingine wa bei isiyo rasmi. Alidai kwamba mikataba hiyo yote ipo mikononi mwa Serikali kwa muda mrefu. Alidai kuwa kauli yake na ya Kikwete akiwa Waziri juu ya ununuzi wa jengo hilo unaonyesha kuwa bei zinalinga na kwamba hakuwahi kupata malalamiko yoyote wala kuhojiwa juu ya uhalali wa matumizi hayo ya fedha. Balozi Mahalu pia alidai kuwa hakuwahi kuona upande wa mashtaka ukipeleka kesi mahakamani hapo kama mama mwenye jengo hilo la ubalozi lililonunuliwa alikuwa amelipwa fedha pungufu ya bei iliyokubaliwa na katika mgogoro huo pia, hakuwahi kuona mama huyo akipeleka malalamiko kuwa hakuwahi kulipwa malipo yake. Akimalizia kutoa utetezi wake, Profesa Mahalu alidai yeye si mbadhirifu kama anavyoshtakiwa na kwa kuithibitishia Mahakama na kwa kuthibitisha hilo, alitoa nishani na tuzo mbalimbali alizowahi kutunukiwa nchini Italia kutokana na uaminifu na utendaji kazi mzuri wa kuboresha uhusiano kati ya Tanzania na nchi hiyo. Wakili wa Serikali, Ponziano Lukosi aliiomba Mahakama iwape muda ili waweze kujiandaa kufanya madodoso juu ya ushahidi wa mshtakiwa. Hakimu Mgeta alikubaliana na ombi hilo na kuiahirisha kesi hiyo hadi Machi 21, mwaka huu. Mwendelezo wa juzi Juzi, akitoa utetezi wake, Profesa Mahalu aliiambia Mahakama hiyo kuwa Kikwete wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alifahamu kuwepo kwa rasimu mbili za mikataba ya ununuzi wa jengo la Ubalozi wa Tanzania nchini Italia. Mahalu aliitambua barua ya Februari 20,2002 ambayo ilikuwa ikieleza kuwa matayarisho yote ya ununuzi wa jengo la ubalozi huo yamekamilika ikiwa ni pamoja na rasimu mbili za mikataba. Mahalu alidai kuwa katika mchakato wa ununuzi wa jengo hilo la ubalozi wakati yeye akiwa Balozi chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kulikuwa na rasimu mbili za mikataba na kwamba aliwahi kuwasiliana na wizara hiyo juu ya mikataba hiyo. Alidai kuwa Desemba 2001, Kikwete alikwenda Rome kwenye mkutano wa SADC na alipokuwa huko, ubalozi ulifanya mpango ili atembelee jengo hilo lililopendekezwa kununuliwa kama ofisi ya ubalozi. Alidai kuwa alikwenda kutembelea jengo hilo na kukutana na mama mwenye jengo na kwamba kabla ya mazungumzo yao Kikwete, mtoto wa mama huyo, Alberto alimzungusha kwenye jengo hilo ndani na nje na baadaye mazungumzo hayo yaliendelea. Balozi Mahalu alidai kuwa katika mazungumzo hayo Alberto alikuwa akitafsiri, kwa sababu mama yake hakufahamu lugha ya Kingereza. Mahalu alidai kuwa katika mazungumzo hayo, Kikwete alimuuliza mama huyo, “Hivi ni kwanini kunakuwa na mikataba miwili? na mama huyo alimjibu kuwa hiyo ni kawaida kwa Italia ukitaka kununua jengo kwa bei nafuu. Profesa Mahalu aliendelea kudai kuwa baada ya kupewa jibu hilo, Kikwete hakuzungumza tena zaidi ya kucheka na kwamba mwenye jengo alimkumbusha kuhusu malipo ya awali ya Dola za Marekani milioni moja ambapo aliafiki na kuahidi kuwa zingelipwa kabla ya mwisho wa mwaka.
chanzo;mwananchi
|
No comments:
Post a Comment