Monday 16 April 2012
Familia ya Kanumba yasita kuanika utajiri wake
Editha Majura
UTAJIRI wa aliyekuwa msanii maarufu katika tasnia ya filamu nchini, marehemu Steven Kanumba, mpaka sasa umeendelea kuwa siri baada ya familia yake kusita kuuzungumzia kwa maelezo kwamba ni mapema mno na bado wanamlilia mtoto wao.
Mdogo wa marehemu Kanumba, aliyekuwa akiishi naye Sinza Vatican, Dar es Salaam mpaka hadi mauti yalipomfika, Seth akizungumza na Mwananchi Jumapili nyumbani hapo juzi, alisema; “Mama hayuko tayari kuzungumzia masuala ya mali, ni mapema mno bado anamlilia mtoto wake.”
Seth alisema siyo rahisi katika muda mfupi kama huu kufahamu mali za marehemu, lakini familia ikitulia na kutekeleza jukumu hilo kwa ukamilifu, taarifa zitatolewa kwa jamii kama itaonekana kuna umuhimu wa kufanya hivyo.
Naye Gabriel Mtitu anayetajwa na wachungaji wa Kanisa la AIC, alilokuwa akisali Kanumba enzi za uhai wake, kuwa ndiye aliyemuingiza kwenye uigizaji, alisema imeundwa Kamati kumsaidia mama mzazi wa marehemu kufuatilia na kuweka salama mali zote alizokuwa akimiliki.
“Kamati itamsaidia mama kufuatilia mali za marehemu ikiwemo mikataba ya kazi aliyoiingia ndani na nje ya nchi, mashamba, nyumba, uendelezaji wa kampuni yake,” alibainisha Mtitu.
Alisema alifahamiana na Kanumba akiwa mwanafunzi wa Sekondari ya Jitegemee na muimbaji katika kwaya ya Neema Gospel, ya AIC - Chang’ombe.
Mchunguji Samweli Daudi wa Kanisa la AIC – Magomeni ambaye ndiye alimpokea Kanumba kwenye kanisa hilo – Chang’ombe mwaka 2004, anasema alipoingia kanisani alionekana kuwa na karama ya uimbaji, utunzi na upigaji wa gitaa.
“Nilimpokea mwaka 2004 kama msharika wa kawaida lakini akaonekana kuwa na kipaji cha kuimba na kutunga nyimbo baada ya kujiunga na kwaya ya Neema Gospal na pia alikuwa akipiga gitaa ya base,” alibainisha Mch. Samweli
Hata hivyo, alisema baada ya Kanumba kujiunga na shughuli za uigizaji, mwaka 2005 mahudhurio yake kanisani yalianza kutetereka, alikuwa akizungumza naye mara kwa mara akimuasa kutolegalega katika shughuli za kanisa kwa maana ndiyo chimbuko la mambo yote.
Alisema hakujua kwa uhakika hali ya kiimani aliyokuwa nayo muda mfupi kabla ya siku ya mauti yake, akashauri Mwananchi Jumapili liwasiliane na Mchugaji Charles Sweya, wa AIC-Chang’ombe, alikokuwa akisali.
Mch. Sweya alisema, alimfahamu Kanumba enzi za uhai wake kwa kuonana na kuzungumza naye wakati alipokuwa akihudhuria ibada siku za Jumapili, ingawa hakuwa akihudhuria mara kwa mara bila shaka kutokana na kuwa na shughuli nyingi.
Alisema mara ya mwisho kuhudhuria ibada ilikuwa majuma matatu kabla kifo chake. Kwa mujibu wa Mch. Sweya, mazungumzo mengi ya Kanumba yalihusu namna ya kuwasaidia watoto katika masuala mbalimbali, hata hivyo alisema mpaka anafikwa na mauti, alikuwa hajatekeleza azma yake hiyo.
“Kila alipofika kanisani, alikuwa mtu wa kukaa na watoto na kuwapigia hadithi mbalimbali na walimpenda sana. Kila nilipozungumza naye alipenda kudadisi ninachoona watoto wa kanisani wakifanyiwa kinaweza kuwa msaada kwao ingawa mpaka alipokutwa na kifo, hakuwa amefanikisha dhamira yake hiyo,” alisema Mch. Sweya
chanzo:mwananchi
No comments:
Post a Comment