Friday 20 April 2012

ZITO ATAKA SAINI 70 KUMNG"OA PINDA

Thursday, 19 April 2012 23:27
0digg
Waziri Mkuu,Mizengo Pinda.
ZITTO ATAKA SAINI ZA WABUNGE 70 KUMNG'OA,MAWAZIRI WATANO WATAKIWA KUJIUZURU, FILIKUNJOMBE ADAI MKULO MWIZI
Na Waandishi wetu, Dodoma na Dar
BUNGE jana lilichafuka baada ya wabunge kuishambulia Serikali kwa kukumbatia ufisadi, huku baadhi yao wakiandaa mkakati wa kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Akifanya majumuisho ya hoja zilizotolewa na wabunge pamoja na mawaziri, Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (PAC) Zitto Kabwe, alisema kuwa wanachohitaji kukamilisha mchakato huo ni kupata saini za wabunge 70.

Kwa sababu hiyo, akasema inabidi wabunge wenye uchungu na jinsi fedha za Serikali zinavyofujwa na watendaji mbalimbali wasaini kwenye karatasi hiyo ili hoja hiyo iwasilishwe bungeni Jumatatu.

Fukuto la kutaka Waziri Mkuu ajiuzulu lilianza katika kikao cha faragha cha  wabunge wa CCM kilichofanyika mchana, baada ya wabunge kutaka Serikali iwawajibishe mawaziri wezi vingine Pinda ajiuzulu.

Iwapo kura za kutokuwa na imani zitapigwa, huenda Pinda akalazimika kujiuzulu na matokeo yake Rais Jakaya Kikwete itambidi kulivunja Baraza la Mawaziri na kuunda jipya.

Zitto alisema mpango huo unapaswa kufanyika ili kuweka msingi wa uwajibikaji kwa viongozi wa nchi kwa sababu limekuwa ni tatizo sugu.

“Misingi ya uwajibikaji lazima iwekwe,” Zitto alisema akisisitiza kuwa ni moja ya jambo ambalo kama lingekuwa linatekelezwa nchini ama kuwekewa mkakati maalumu wa utekelezaji,Tanzania ingepiga hatua kimaendeleo.

Awali Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) amewaomba wabunge wote kuungana bila kujali itikadi za vyama vyao na kupiga kura ya kutokuwa na imani na Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kuhusu uendeshaji wa nchi.

Akichangia mjadala kuhusu taarifa hizo za kamati, Lissu ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Upinzani Bungeni, alisema wakati CAG, Ludovick Utouh amekuwa akitoa taarifa ya wizi wa kutisha, hakuna hatua zozote zilichochukuliwa na serikali.

Alisema tatizo linaloikabili nchi hivi sasa ni kuwa na mfumo wa utawala wa wizi ambao unalinda wezi na unaoadhibu watu wanaosema ukweli na kutoa mfano kuwa ukitaka ‘kushughulikiwa’ fuatilia wizi ndani ya halmashauri za wilaya.


“…wabunge tuache kulalamika tu- move a motion (tulete hoja) ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na serikali,”alisisitiza Lissu.



Filikunjombe
Awali, Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe jana alichachamaa bungeni na kumlipua Waziri wa Fedha, Mustapha Mkulo kwa madai kuwa ni mwongo na anaongoza kundi la mwaziri 19 wa Serikali aliodai, wanatafuna fedha za umma na kulifilisi taifa.

Filikunjombe alifikia hatua hiyo baada ya kutakiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uratibu na Bunge William  Lukuvi kuomba mwangozo wa Spika, ukimtaka mbunge huyo kijana kuthibitisha madai aliyoyatoa wakati wa  mjadala wa kuchangia Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, ambapo aliwashambulia mawaziri huku akiweka bayana kuwa ana ushahidi na majina 19 ya mawaziri,mchwa wanaolitafuna taifa.

"Mimi nina ushahidi wa mawaziri 19 na nikipata fursa nitamtaja mmoja kwa jina leo (jana) jioni," alisema.

Akizungumza kwa hisia, Filikunjombe alimtaja Mkulo akisema kuwa siyo mwaminifu na mwongo huku akionesha ripoti aliyodai imeanika madhambi yote ya Mkulo.

Alisema kuwa anashangaa kwanini tangu ripoti hiyo iwasilishwe, hakuna hata waziri mmoja aliyejiuzulu na kuongeza kuwa mawaziri hao wamekuwa na tabia ya kulindana.

“Nitamtaja Waziri mmoja ambaye anahusika na ubadhirifu huu. Waziri Mkulo siyo mwaminifu. Kila mbunge anayoripoti hii inayoeleza ubadhirifu huu,” alisema Filikunjombe na kuongeza;
“Alitaka kuifuta CHC, waheshimiwa wabunge tukapigana humu Bungeni tukashinda, …alipoona Mkurugenzi wake anamfuatilia, alimsimamisha kazi na kuisimamisha kazi bodi ya shirika hilo. Waziri Mkulo ni mwongo!”

Alitoa mfano wa jinsi fedha za Serikali zinavyopotea akiitaja Taasisi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kwamba licha ya fedha nyingi kupelekwa huko, zimekuwa zikiliwa na wakuu wa vyuo.
Alimtaja Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki  cha Mkwawa akisema kuwa anahusika moja kwa moja na wizi wa fedha hizo.

Filikunjombe pia alimtaja Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami kuwa amekuwa akilinda uozo wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa maslahi yake binafsi.

“Kuhusu hili la Shirika la Viwango (TBS) ambalo halina viwango….Waziri Chami amekuwa akilinda TBS kwa nguvu zake zote… najua ulinzi huo siyo wa bure, mnakumbatia mmoja. TBS hawafanyi ukaguzi wowote, kuna blueband mbovu, vyakula vibovu, mafuta ya ndege feki, matairi feki ndiyo maana hata ndege ilianguka kule. Maisha ya Watanzania yako hatarini” alisema Filikunjombe.

Huku akimkazia macho Waziri Mkuu, Filikunjombe alisema kuwa baadhi ya mawaziri wake si waaminifu na kuongeza kuwa nchi hii sio ya CCM wala hivyo haipaswi kusubiri hadi wapinzani waseme au waandamane.


Wabunge wa CCM
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Pinda jana alijikuta katika wakati mgumu baada ya wabunge wa CCM kumtaka ama ajiuzulu au awafukuze kazi mawaziri wake watano wanaohusishwa na tuhuma mbalimbali zikiwamo za kushindwa kuwajibika na kuruhusu ufisadi wa kutisha kufanyika.

Huo utakuwa ndio mtihani wa kwanza mkubwa kuwahi kumkumbua Waziri Mkuu huyo tangu ashike wadhifa huo Februari 2008,  huku akiwa na kumbukumbu ya mtangulizi wake, Edward Lowassa aliyelazimika kujiuzulu kwa shinikizo la wabunge.

Shinikizo la Waziri Mkuu kutakiwa ama kujiuzulu ama kuwatosa mawaziri wake hao lilianzia ndani ya Bunge na baadaye kuhamia katika kikao cha faragha cha Wabunge wa CCM kilichoitishwa kujaribu kupunguza makali ya Wabunge hao dhidi ya serikali.

Mawaziri waliomponza Waziri Mkuu Pinda ni pamoja na Waziri wa Fedha, Mkulo, Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (Tamisemi), George Mkuchika, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami na Naibu wake, Lazaro Nyalandu.

Hasira ya Wabunge hao ilitokana na ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na taarifa za wenyeviti wa kamati tatu za kudumu, zote zikionyesha wizi na ufisadi wa mabilioni ya shilingi katika serikali kuu, mashirika ya umma na Halmashauri mbalimbali za wilaya na majiji.

Taarifa zilizovuja kutoka ndani ya kikao hicho kilichoanza saa 7.10 mchana hadi saa 11:08 mchana zilieleza wabunge walimshambulia waziwazi Waziri Mkuu Pinda kuwa amekuwa na kigugumizi kisicho cha kawaida na mzito wa kuchukua maamuzi dhidi ya wale wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali kutoka ndani ya kikao hicho, wabunge hao walimtuhumu Waziri Mkuu kuwa amekuwa akimshauri vibaya rais na hivyo kushindwa kuwafukuza mawaziri hao wanaonekana kuwa ni mzigo kwa Serikali na kuifanya iboronge katika utendaji.

“Kwa ujumla Pinda hana hatia, lakini kikubwa kinachomfanya asulubiwe ni kitendo chake cha kuwa na kigugumizi kwa kushindwa kufikisha majibu sahihi ya wabunge kwa rais na kutufanya tuendelee kuwa na hii mizigo,’’kilisema chanzo hicho kimoja cha kuaminika.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa huyo, wabunge waliokuwa msumari wa moto kwa serikali ni pamoja na Livingston Lusinde, Zainab Kawawa, Godfrey Zambi,Michael Laizer pamoja na Peter Serukamba ambao kila mmoja alitoboa hadharani kuwa Serikali imeoza.

Zainabu aliwaeleza wabunge kuwa kwa hali ilikofikia sasa,kama waasisi wa Taifa hili wangefufuka na kupata hata dakika moja tu ya na kushuhudia madudu yanayofanyika,wangeamua kujiondoa tena kutoka ndani ya CCM na tena wangeondoka kutokana na aibu hizi.
“Kwa ujumla ninyi wazee hamfai, tena hamfai kabisa mnakotupeleka ni kubaya kulikooza hebu tuondoleeni aibu hiyo,’’alisema Kawawa.

Kwa upande wake Lusinde alimueleza Waziri Mkuu Pinda kuwa anafanya kila namna ya kuhakikisha kuwa kila kitakacholetwa katika kipindi cha bajeti kinakwamishwa kutokana na yeye kuwa na zaidi ya vijiji 71, lakini havina maji hata kidogo huku baadhi ya mawaziri wakibeba kila kitu cha nchi hii na kupeleka katika majimbo yao.

Lusinde alisema yuko tayari kujiuzulu ubunge pamoja na nafasi zake ndani ya chama kwani hakuna faida ya yeye kuwa mbunge huku mawaziri wakiendelea kumdanganya.

Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi alimtaka Waziri Mkuu kufikisha kwa Rais Jakaya Kikwete mara moja hoja ya kuwafukuza Mawaziri mzigo na kusema kuwa kama hatafanya hivyo bunge halitakalika.

“Kikubwa unachotakiwa kumfikishia rais ni kuwa hawa mawaziri ni mzigo, wameoza tafadhali sana bila ya hivyo bunge halitakalika hapa tunakwambia maana hata akibadilisha Waziri Mkuu lakini bila ya hawa jamaa kuondoka ni sawa na kazi bure,’’alisema Zambi.

Mbunge wa Longido, Michael Lekule Laizer alimtaka Pinda kufikisha ombi lake kwa rais na kumueleza kuwa kama ameshindwa kuwafukuza mawaziri hao basi ni lazima avunje Serikali na nchi irudi katika uchaguzi.
Lazier alisema mahali ilipofikia sasa ni pabaya ambapo kila mmoja anatakiwa kubeba msalaba wake mwenyewe na kufa nao vinginevyo shimo hilo litawatumbukiza wengi hata wale ambao hawakuhusika.
Chanzo kingine cha habari kilisema wabunge hao walifikia maazimio ya kumpa muda Waziri Mkuu kwenda kuwasiliana na Rais juu ya kuwawajibisha mawaziri hao na kama hatafanya hivyo watapiga kura ya kutokuwa na imani na serikali katika Bunge lijalo.

Ole Sendeka azomewa
Katika kikao hicho wabunge walimzomea Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole-Sendeka baada ya kusimama na kuonyesha wazi kuwa anawatetea mawaziri hao walioonekana kuchafua hali ya hewa.

Inadaiwa Ole Sendeka aliwataka wabunge wenzake kupunguza hasira na kuwasamehe mawaziri akisema kuwa nao ni binadamu ambao kwa vyovyote lazima wawe na mapungufu.

Kauli hiyo iliufanya ukumbi huo wa Msekwa kulipuka kwa kumzomea kabla ya Mbunge wa Kigoma, Mjini Peter Serukamba kumueleza mbunge huyo kuwa “ huna sera kwa leo kaa chini”.

Wakati hayo yote yakitokea, hakuna Waziri aliyepewa nafasi ya kueleza jambo lolote au kujitetea kwani hata Waziri Mkuu alijibu kwa ufupi kuwa wameyasikia na wanakenda kuyafanyia kazi.

Mbowe
Naye kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alionyesha kushangazwa na kutokuwepo kwa wabunge wengi wa CCM akisema kuwa wamekwenda kwenye mkutano na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ili kuinusuru Serikali ya CCM.

Mbowe aliyekuwa wa kwanza kuchangia katika kipindi cha jioni, alisema atahamasisha wananchi kote nchini kuandamana ili kuiondoa madarakani Serikali iliyoshindwa kuwajibika.

“Katika historia ya Bunge hili tangu lilipoanza kuonyeshwa moja kwa moja, sijawahi kuona wabunge wakitoka bungeni ili kuinusuru Serikali na kuacha watu sita tu wa kukaba nafasi,” alisema Mbowe.
Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa Chadema, alisema kuwa licha ya wabunge wa upinzani ukupiga kelele kuhusu ubadhirifu serikalini bado hawasikilizwi.

“Wananchi wajue kwamba wabunge wa upinzani hatusikilizwi bungeni, lakini tukiandamana ndiyo tutasikilizwa. Kama wabunge na mawaziri wa CCM wameondoka bungeni, basi watupishe na Ikulu na ofisi nyingine tuwaonyeshe nanma ya kufanya kazi,” alisema Mbowe.

Wabunge wengine
Naye Mbunge wa Kasulu Mjini Moses Machali aliitaka Serikali kuchukua hatua kali kwa wote waliohusika na ubadhirifu huo ikiwa ni pamoja na kuwanyonga,
“Unaweza kuwadanganya baadhi ya watu kwa wote na unaweza kuwadanganya watu wote kwa wakati fulani lakini huwezi kuwadanganya watu wote kwa wakati wote. Mambo haya yamesema mno…… Waliosababisha haya yote wakamatwe na wanyongwe hadharani ili iwe fundisho kwa wengine watakaohusika” alisema Machali.

Machali pia alimlaumu Waziri Lukuvi kwa kile alichosema kuwa ni kuchakachua kauli za wabunge.
Kwa upande wake Mbunge wa Musoma mjini Vincent Nyerere alikumbushia swali alilomuuliza juzi Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Chami kuhusu ukaguzi wa magari akikosoa kuwa waziri huyo hakusema kweli.
Alitaja kampuni alizoziita kuwa za kitapeli akisema kuwa zimekuwa zikijifanya kukagua magari wakati si kweli.

“Septemba 25, 2007 kuna wajanja walikutana pale hoteli ya Movenpick na kuanzisha kampuni za ukaguzi wa magari ili zionekane kuwa ni kampuni za nje. Hakuna magari yanayokaguliwa kama alivyosema Waziri” alisema Nyerere.

Aliongeza kuwa tangu ukaguzi huo feki ulipoanzishwa kampuni hizo zimepata dola za Marekani 18 milioni (zaidi ya Sh 23 bilioni) huku Serikali ikiambulia dola milioni mbili tu.


Mapema, wakati akichangia mjadala  wa taarifa za kamati tatu za kudumu za Bunge, Dk. Chami alisema wizara yake imetekeleza maazimio yote ya kamati kuhusiana na kashfa ya ufisadi katika Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Katika mchango wake, Dk. Chami aliliambia Bunge kuwa yupo tayari kujiuzulu wadhifa huo endapo itathibitika kuwa yeye au ndugu, rafiki zake wa karibu, wana maslahi yoyote katika kashfa hiyo ya TBS ya kuyapa kazi makampuni bandia  ya ukaguzi wa mizigo nje ya nchi.

“Mheshimiwa Naibu Spika, inaonekana kumejengeka hisia bungeni kuwa tunamlinda Ekelege kama mtu ana uthibitisho nina maslahi katika hili au ndugu yangu niko tayari kuuweka rehani uwaziri wangu…niko tayari kujiuzulu,”alisema.

Dk. Chami alijitetea kuhusu taarifa ya maalumu ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwamba ndiyo kwanza ilikuwa imemfikia juzi jioni, hivyo akawaomba wabunge waamini kuwa wizara yake ilikuwa haijapatiwa matokeo ya taarifa hiyo.

Mapema, Mbunge wa Lulindi, Jerome Bwanausi (CCM) alipendekeza kuwa kwa halmashauri ambazo zimekuwa na tuhuma nzito za ufisadi, wakurugenzi wake wasimamishwe kazi wakati uchunguzi wa tuhuma hizo ukiendelea.

Naye Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), alilitaka Bunge kutumia mamlaka yake ya kikatiba kuchukua hatua kwa vile kama ni kusema basi wametumia asilimia 70 ya muda wao kusema na sasa wanahitaji kuchukua hatua kwani hakuna mabadiliko.
 
Hali kadhalika, Mbunge wa Shinyanga Mjini, Steven Maselle (CCM) alitaka kufumuliwa kwa TBS akisema inasikitisha kuwa bidhaa feki zinaendelea kuzagaa nchini na mbaya zaidi ni kuingizwa nchini kwa maziwa feki ya watoto jambo ambalo ni la hatari zaidi.

Mbunge wa Viti Maalumu, Christowaja Mtinda(Chadema) alishangaa jina lake kuorodheshwa kuwa ni mtumishi wa Chuo Kikuu Huria nchini (OUT) wakati si mtumishi wa chuo hicho na kuhoji mshahara huo ni nani anayelipwa.

CHANZO:MWANANCHI

No comments:

Post a Comment