SERIKALI
ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema operesheni ya kuwasaka wahalifu
walihusika na vurugu za wiki iiliyopita inaendelea na Serikali haitakuwa
na msalia mtume kwa yeyote aliyehusika na vurugu hizo.
Akizungumza
katika mkutano na viongozi wa dini katika ukumbi wa Kanisa la
Pentekoste Tanzania lililopo Kariakoo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed alisema Serikali imesikitishwa na
kitendo kilichotokea cha vurugu na uchomaji wa nyumba za ibada,
Makanisa.
“Hizi
ni njama za makusudi, nataka nisemawazi kwamba watu hawa wametangaza
mapambano na Serikali,tutawashughulikia ipasavyo,” alionya Waziri Aboud.
Watu waliofanya vurugu Zanzibar sasa watakiona kwani wametangaza mapambano na Serikali, itawashughuliki popote walipo.
Waziri
Aboud alisema kwamba waumini wa dini zote wamekuwa wakiishi kwa upendo
na maelewano makubwa kwa miaka mingi ambapo ustahamilivu wa kidini upo
kwa hali ya juu katika Visiwa vya Unguja na Pemba.
“Mie
nakumbuka nilipokuwa nakaa kule Shangani kwa mfano Mwezi wa Ramadhani
utakuta tunapelekeana vyakula, waislamu wanapeleka kwa wakristo na hata
siku ya sikuuu ya Idd el Fitr tunasherehekea pamoja, huwezi kubagua yupi
mkristo yupi Muislam,” alisema waziri hyo.
Alisema
Serikali inawapo pole waumini wa makanisa yaliyochomwa moto na
kuwaahidi hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wale wote waliohusika.
Akizungumza
katika mkutano huo,Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Said
Mwema alisema Polisi imejipanga kimkakati kukabuiliana na wale wote
watakaofanya au kuchochea ghasia.
“Tunaendelea
kudhibiti hali,doria kama kawaida na pia tumeweka ulinzi maalum katika
nyumba za ibada tumezijumuisha katika sehemu muhimu za ulinzi kwa
kipindi hichi,” alisema IGP Mwema.
IGP
Mwema alisema pia ameunda timu maalum ya kikosi kazi ambacho
kinajumuisha maafisa kutoka Idara ya Upelelezi Makao Makuu Dar es Salaam
kuchunguza matukio ya vurugu hizo na kuwachukulia hatua watakaobainika.
Alisema
katika mkutano huo pia jumla ya watu 46 wamekamatwa jana (juzi) na kati
ya hao 43 wamefikishwa mahakamani jana Mjini Zanzibar wakikabiliwa na
tuhuma mbalimbali.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Abdallah Mwinyi
Khamis alisema Serikali ya Mkoa wake imesikitishwa mno na vitendo vya
ghasia na uchomaji wa makanisa moto.
Mkuu
huyo wa Mkoa alisema uvumilivu wa kidini ni jambo la msingi sana na
anaamini waliofanya vurugu na kuchoma baadhi ya makanisa moto sio
waumini wa dini ya Kiislamu bali ni wahalifu.
“Tujiulize
jamani, hivi kweli muumini wa kiislam anaweza kwenda kuvunja baa na
kasha kuanza kunywa pombe? Hawa sio Waislam …hapa kuna jambo,
tutawachunguza kubaini chanzo na wanaohusika na kadhiaa hii,” alisema
Mkuu huyo wa Mkoa.
Akithibitisha
uvumilivu wa kidini uliokuwepo Zanzibar tangu enzi na enzi, Mkuu wa
Mkoa alitoa Stempu ya Serikali ya Kikoloni iliyopambwa kwa picha za
misikiti na makanisa wakati wa utawala wa Kisultani chini ya himaya ya
Uingereza yenye ujumbe wa uvumilivu wa kidini Zanzibar.
“Stempu
hii iliyokuwa imetolewa na Serikali ya Kiingereza wakati ule
inathibitisha kwamba Zanzibar hakuna tatizo la waislamu na wakristo,huu
jamani ni ushahidi tunashangaa leo wanatoka watu wanachoma moto kanisa,”
alisema.
Alitoa
mfano wa namna wananchi Zanzibar walivyokuwa wakiishi kwa upendo na
mshikamano wa maziko ya aliyekuwa Waziri Mwandamizi katika Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, marehemu Brigedia Jenerali Adam Mwakanjuki, idadi ya
Waislamu mazikoni ilikuwa kubwa kuliko ya dini nyingine.
“Mbali
na hili la mwenzetu Mwakanjuki, mimi mwenyewe niliombwa na Skuli ya
Kanisa St Joseph kusomesha, walikuwa na upungufu wa walimu, Wizara ya
Elimu ikaniteuwa mie nienda kusomesha, nimeishi nao vizuri,
hawakunitenga …mimi ndio mwalimu wa mwanzo muislam kusomesha skuli ya
wakristo hapa Zanzibar,” aliongeza Mkuu huyo wa Mkoa.
Katibu
Mkuu wa Makanisa ya Pentekoste Tanzania, Askofu David Mwasota
aliishukuru Serikali kwa kuwaunga mkono na kuwa pamoja nao kitendo
ambacho kinathibitisha dhamira njema ya Serikali na viongozi kwa ujumla.
Askofu
Mwasota alisema kesho (leo) watafanya mkutano wa madhehebu yote ya
kidini kuzungumzia kadhia hiyo mkutano ambao utafanyika katika Kanisa la
Pentekoste Kariakoo Unguja.
Mkuu
wa Dini ya Kiislam katika Ofisi ya Mufti Mkuu Zanzibar, SheikhThabit
Noman Jongo ameshangazwa na watu wanaochoma moto makanisa na
kuwafananisha watu hao kuwa ni wahalifu na Serikali iwachukuli hatua
kali kwani Waislam hawana ugomvi na Wakristo.
Na Juma Mohammed – MAELEZO, Zanzibar
No comments:
Post a Comment