JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO
TAMKO LA SERIKALI
GAZETI LA MWANAHALISI LAFUNGIWA
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imelifungia kutochapishwa gazeti la
MwanaHalisi kuanzia 30 Julai, 2012 kwa muda usiojulikana kutokana na
mwenendo wake wa kuandika habari na makala za uchochezi, uhasama na
uzushi likiwa na nia ya kusababisha wananchi kukosa imani na vyombo vya
dola hali inayoweza kuhatarisha amani na mshikamano uliopo nchini.
Katika
matoleo yake hivi karibuni, gazeti la MwanaHalisi toleo Na. 302 la
Jumatano Julai, 11 – 18, 2012 na toleo Na. 303 la Jumatano Julai 18 –
24, 2012 na toleo Na. 304 la Jumatano Julai 25 hadi 01 Agosti, 2012 na
mengine yaliyotangulia yamekuwa yakichapisha habari na makala zenye
kueneza na kujenga hofu kwa jamii.
Mhariri
wa gazeti la MwanaHalisi, ameitwa na kuonywa mara nyingi, lakini hataki
kukiri kuwa maudhui ya makala zake hazina tija kwa jamii, pia hazifuati
weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.
Mhariri,
mara zote katika utetezi wake amekuwa akinukuu kifungu cha 18 cha
Katiba ya nchi yetu ambacho kinatoa uhuru wa kutoa maoni na kwa makusudi
kutonukuu kifungu cha 30 cha Katiba hiyo kinachoweka ukomo wa uhuru.
Uamuzi wa Serikali
Serikali
imeamua kulifungia kutochapishwa kwa muda usiojulikana gazeti la
MwanaHalisi, kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, kifungu Na.
(25) (i), adhabu hiyo itaanza tarehe 30 Julai, 2012 kwa mujibu wa
Tangazo la Serikali (Government Notice) Na. 258 lililochapishwa katika
Gazeti la Serikali na kutolewa jijini Dar Es Salaam tarehe 27 Julai,
2012.
Serikali
inawataka wamiliki, wahariri na wanahabari kuzingatia sheria, uzalendo,
weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari katika kutekeleza
wajibu wa kuhabarisha, kuelimisha na kutoa burudani kwa wananchi.
Kama
ilivyoelezwa Bungeni wakati wa kuwasilisha Bajeti ya Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo hivi karibuni waandishi na watangazaji wa
habari wanatakiwa kuhakikisha kuwa habari wanazoziandika na vipindi
wanavyoandaa vinazingatia taaluma na kuweka mbele maslahi ya Taifa letu na uzalendo. Uhuru na haki ya vyombo vya habari uendane na wajibu.
Kuanzia
sasa Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya vyombo vya habari
ambavyo kwa maksudi vitatoa taarifa za uchochezi ambazo zitahatarisha
hali ya amani na utulivu uliopo nchini mwetu.
Imetolewa na
OFISI YA MSAJILI WA MAGAZETI
WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO
30 Julai, 2012
No comments:
Post a Comment