SERIKALI YA KENYA: imesema inazifanyia kazi taarifa za raia wake kukamatwa na kufikishwa kortini nchini kwa tuhuma za kumteka na kufanya jaribio la kumuua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka.
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Jeshi la Polisi kutangaza kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa raia wa Kenya, Joshua Mulundi anayetuhumiwa kuhusika na tukio la kumteka, kumpiga na kumtupa Dk Ulimboka katika Pori la Akiba la Pande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam hivi karibuni.
Balozi wa Kenya nchini, Mutinda Mutiso, alisema kwa njia ya simu jijini Dar es Salaam jana kuwa Serikali yake itachunguza uraia na tuhuma zinazomkabili mtu huyo ili kubaini ukweli.
“Ndiyo kwanza nimewasili kutoka nje ya nchi…, nitafuatilia kwa makini kupata taarifa sahihi kutoka kwenye vyanzo sahihi na mamlaka husika za hapa Tanzania na Kenya ili kupata taarifa ya kweli,” alisema Balozi Mutiso na kuongeza: “Siwezi kueleza zaidi kwa sasa kwani itakuwa naeleza uvumi.”
MAT wadai kutoridhishwa
Wakati Balozi wa Kenya akisema hayo, Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), kimeelezea kutoridhishwa na hatua hiyo kikisisitiza msimamo wake wa kutaka kuundwa kwa tume huru ya uchunguzi kwa lengo la kuwabaini wahusika na kuchukuliwa hatua stahiki.
MAT pia imesema kwamba, inaendelea na mpango wake wa kuandamana, ikibainisha kuwa kesho itawasilisha barua ya kuomba kibali cha kufanya maandamano ya amani Polisi.
Imefafanua kuwa malengo ya maandamano hayo yaliyopigwa 'stop' na polisi kwa kile walichoeleza ni sababu mbalimbali za kiusalama na kwamba, madai mengi ya madaktari yamefanyiwa kazi na Serikali.
"Nisingependa kuingilia suala la kipolisi kwa ujumla wake, lakini moja ya madai yetu ni kuundwa kwa tume huru ya kuchunguza tukio la kutekwa, kupigwa na kutupwa katika Msitu wa Pande kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Dk Ulimboka," Katibu Mkuu wa (MAT) Dk Rodrick Kabangila aliliambia Mwananchi Jumapili jana.
TUCTA nao wamo
Katika hatua nyingine, Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi (Tucta) limelipongeza Jeshi la Polisi kwa kumkamata mtu anayedaiwa kumteka na kumpiga kiongozi wa mgomo wa madaktari, Dk Steven Ulimboka.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Tucta, Nicolaus Mgaya alisema kuwa, hatua ya kumkamata mtuhumiwa huyo inaleta matumaini ya kuwabaini watu wengine waliohusika na vitendo hivyo, jambo ambalo linaweza kurahisisha uchunguzi.
Alisema kutokana na hali hiyo, jeshi hilo linatakiwa kuendelea na uchunguzi ili waweze kuwabaini wahusika wengine na kubaini ukweli kuhusu tukio hilo ambalo limesababisha kutokea kwa hisia tofauti katika jamii.
“Tunaliomba Jeshi la Polisi liendelee na uchunguzi ili waweze kuwabaini watuhumiwa wengine na kuwachukulia hatua za kisheria,” alisema Mgaya.
Mkenya kukamatwa
Joshua Mulundi, ambaye anatuhumiwa kumteka na kumtesa Dk Ulimboka alikamatwa na kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam juzi alasiri na kusomewa mashtaka mawili na Wakili wa Serikali, Ladslaus Komanya.
Wakili Komanya alidai mahakamani hapo kuwa, Mulundi ambaye makazi yake ni Murang'a nchini Kenya mnamo Juni 26, mwaka huu akiwa eneo la Leaders Club alimteka Dk Ulimboka.
Hata hivyo, kumetokea utata wa jina, umri wake na makazi ya mtuhumiwa huyo.
Wakati hati ya mashtaka mahakamani inasema ni Joshua Mulundi mwenye umri wa miaka 21, mkazi wa Murang’a nchini Kenya, taarifa ya Jeshi la Polisi imesema anaitwa Joshua Mahindi mwenye miaka 31 na mkazi wa Namanga nchini Kenya.
Katika shtaka la pili, Wakili Komanya alidai kuwa tarehe hiyohiyo mshtakiwa alifanya jaribio la kumsababishia kifo Dk Ulimboka kwa kumpiga katika eneo la Msitu wa Pande eneo la Tegeta jijini Dar es Salaam, kinyume cha sheria.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo alikana mashtaka hayo akidai kuwa makosa aliyoshtakiwa nayo siyo sahihi.
Hakimu Mkazi, Agnes Mchome alimwambia kuwa hatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, isipokuwa Mahakama Kuu pekee.
Afya ya Dk Ulimboka yazidi kuimarika
Akizungumzia hali ya Afya ya Dk Ulimboka anayeendelea na matibabu nchini Afrika Kusini, Katibu Mkuu huyo wa MAT alisema kuwa, Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania anaendelea vizuri na sasa ameanza kufanya mazoezi ya kutembea.
"Taarifa tulizonazo sasa ni kwamba, hali ya Dk Ulimboka inaendelea vizuri. Ameanza kufanya mazoezi ya kutembea mwenyewe, anakula na pia anaweza kuzungumza vizuri. Amekuwa akifanya mawasiliano yeye mwenyewe na madaktari wenzake wa hapa nchini ingawa bado kuna matibabu anayoendelea nayo," alisema Dk Kabangila.
Mmoja wa Madaktari wa karibu wa Dk Ulimboka aliyepo nchini, alisema Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania amewatumia ujumbe wa kuwashukuru wanataaluma wenzake na Watanzania wote waliomchangia na kumwezesha kupata matibabu nchini humo.
Hata hivyo alisema kuwa, Dk Ulimboka ameomba suala la tukio lake la kutekwa na kuumizwa lisiwe hoja ya kujadili, badala yake madaktari na wananchi wote wajielekeze kudai haki zao, ambazo Serikali haijazipa kipaumbele.
Dk Ulimboka alisafirishwa nje ya nchi Juni 30 kwa ajili ya matibabu kufuatia jopo la madaktari lililokuwa likimtibu likiongozwa na Profesa Joseph Kahamba kudai afya yake imebadilika ghafla na pia angestahili kupelekwa nje ya nchi kwa ajili ya vipimo na matibabu zaidi ambayo hayapatikani hapa nchini.
Chanzo: www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment