TAARIFA
YA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO
WA TANZANIA, KUFUATIA AJALI YA KUZAMA KWA MELI YA MV SKAGIT ILIYOTOKEA
TAREHE 18 JULAI, 2012, CHUMBE, ZANZIBAR
Jana
tarehe 18 Julai, 2012, majira ya alasiri kumetokea ajali ya kuzama kwa
meli ya MV SKAGIT katika eneo la Chumbe, Zanzibar. Meli hiyo iliyokuwa
ikitokea Dar es Salaam kueleka Zanzibar ilikuwa imebeba watu 290. Kati
yao watu wazima 250, watoto 31 na wafanyakazi wa meli 9.
Amiri
Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete aliagiza vyombo vya ulinzi
na usalama vya Serikali ya Muungano yaani JWTZ na Polisi waanze kazi ya
uokoaji mara moja.
Kazi
hiyo imefanywa kwa kushirikiana na vyombo vya usalama vya Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar na meli za makampuni binafsi. Mpaka giza lilipokuwa
limeingia na hivyo kazi ya uokoaji kusitishwa mpaka kutakapokucha tarehe
19 Julai, 2012, watu 136 walikuwa wameokolewa na maiti 31 zilikuwa
zimepatikana. Aidha, mali zilizokuwa kwenye meli hiyo hazikuweza
kuokolewa.
Kufuatia
ajali hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano alizungumza na Dkt. Ali Mohamed
Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi. Alimpa pole kwa ajali iliyotokea hasa kwa vifo na majeraha
waliyopata Watanzania wenzetu na watu wasiokuwa raia wa Tanzania.
Alimuomba afikishe salamu za rambirambi kwa ndugu zetu waliopotelewa na
jamaa zao na kuwapa pole waliopata majeraha na maumivu maungoni mwao.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano alisema kuwa huu ni msiba wetu sote na kwamba
majonzi yao ni majonzi yake na ya Watanzania wote. Kwa ndugu zetu
waliojeruhiwa tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awape ahueni na wapone
haraka ili waweze kuendelea na shughuli zao za kujiletea maendeleo na
kulijenga taifa letu.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amempongeza Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein na viongozi
wote wa ngazi mbalimbali kwa uongozi wao thabiti tangu taarifa ya
kutokea kwa ajali mpaka sasa.
Aidha,
amewapongeza maafisa na askari wa vyombo vya ulinzi na usalama na
wafanyakazi wa meli binafsi, kwa juhudi kubwa walizozifanya za uokoaji
wa ndugu zetu waliopatwa na maafa haya makubwa na ya aina yake.
Amewataka waendeleze juhudi hizo leo na siku zijazo.
Rais
amewataka wananchi wawe na moyo wa subira na uvumilivu wakati kazi ya
uokoaji inaendelea. Kama ilivyofanyika katika ajali ya MV Spice Islander
miezi 10 iliyopita, uchunguzi wa kina utafanyika kubaini chanzo cha
ajali.
Kutokana
na ajali hiyo na msiba huu mkubwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ametangaza maombolezo
ya taifa ya siku tatu ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kuanzia
leo, tarehe 19 Julai, 2012.
Asanteni sana.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
19 Julai, 2012
No comments:
Post a Comment