Kamati
ya Jumuiya ya Madaktari Nchini , kwanza inapenda kutoa pole kwa
Wanahabari wote nchini kwa kitendo cha kinyama ambacho Mwanaharakati na
Mwandishi wa habari, Marehemu David Mwangosi alifanyiwa, hii ni ishara
kuwa Jeshi la Polisi wameamua kutumia njia ya kuua raia ili kujenga hofu
na woga miongoni mwa wapenda demokrasia na maendeleo nchini.
Pia
tunapenda kulaani kitendo cha Serikali kupitia Wizara ya Michezo,
Habari na Utamaduni kulifungia gezeti makini la Mwanahalisi kwa sababu
ya kutoa taarifa za ukweli juu ya waliotaka kukatiza uhai wa Dr.Ulimboka
Stephen, Jamii ya Madaktari na watanzania wengi bado wanaamini kuwa
waliotajwa na gazeti la Mwanahalisi ni miongoni mwa waliohusika na
kutekwa, kuteswa na kutelekezwa kwake na si yule anayesemekana kuwa na
matatizo ya akili aliyedaiwa kukamatwa na Suleimani Kova. Hivyo
tunalitaka Jeshi la Polisi litoe ripoti yake ya Uchunguzi ili kubaini
ukweli wa taarifa hii.
Pia,
tunachukua nafasi hii kupongeza mshikamano ambao Madaktari wameendelea
kuuonyesha licha ya changamoto nyingi tunazopitia, ni vema ikafaamika
kuwa ni katika kipindi hiki ambacho Mwenyekiti wa MAT na MAT
imefunguliwa kesi 2 mahakamani, Ni katika kipindi hiki ambacho zaidi ya
interns 300 wanasubiri kuitwa kuhojiwa na MCT bila kujua ni lini hilo
litafanyika, Ni katika kipindi hiki ambacho Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Madaktari anapata mapumziko baada ya kutoka katika Matibabu nchini
Afrika Kusini, lakini ni katika kipindi hiki ambacho mpaka sasa hakuna
hata hoja moja ya Madaktari imefanyiwa kazi na Serikali.
Tunapenda
ieleweke kuwa suala la madai ya Madaktari si tukio, ni mchakato ambao
utaendelea kwa vizazi vya sasa na vijavyo, ndio maana tumeshuhudia
migomo hii katika nyakati tofauti pamoja na kujitokeza kikundi au mtu
kutumiwa kuomba msamaha kwa lengo la kudhalilisha taaluma na kurudisha
nyuma jitihada za kuboresha hali ya afya nchini na maslai ya watumishi
kwa ujumla.
Kuhusu
suala la interns, Ikumbukwe kwamba mnamo tarehe 10, Julai 2012, Baraza
la Madaktari Nchini lilitoa taarifa kwa umma kuwa imesitisha leseni za
muda kwa Madaktari waliochini ya mafunzo kwa vitendo, pia waliahidi
kuwaita kwa nia ya kuwahoji mmoja mmoja pindi wakatapokamilisha
uchunguzi wao, cha kushangaza ni kwamba miezi 2 sasa imepita bila hilo
kufanyika.
Katika
vikao mbalimbali ambavyo Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Naibu wake,
Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, na Kaimu Katibu Mkuu wameshiriki,
wamekuwa wakisisitiza kuwa hili lipo kisheria na interns wasuburi kuitwa
kwa ajili ya kuhojiwa. Hivyo tunapenda kutumia nafasi hii kuitaka MCT
itekeleze kwa haraka majukumu yake kwa lengo la kuharakisha upatikanaji
wa haki.
Hivyo
basi Kamati ya Jumuiya ya Madaktari imejiandaa vya kutosha na taratibu
za kisheria na itahakikisha inaweka wakili pale interns watakapoanza
kuhojiwa kwa kuwa sheria inayounda MCT inatoa hiyo nafasi.
Mwisho
kabisa tunapenda kutoa wito kwa interns kutumia hekima na busara katika
kipindi hiki kigumu, waepuke kutumiwa na kikundi cha watu ambao
wanatumika au wanajitumia kwa maslai ya kustarehesha watawala.
IMETOLEWA NA; KAMATI YA JUMUIYA YA MADAKTARI TANZANIA.
No comments:
Post a Comment