BAADHI ya wafanyakazi wa kigeni kutoka mataifa mbalimbali
hususan barani Asia, wameendelea kuajiriwa katika nyadhifa tofauti za
juu kwenye hoteli kubwa za kitalii jijini Dar es Salaam wakati hawana
ujuzi wa taaluma ya kazi husika.
Uchunguzi wa Tanzania Daima umebaini kuwa wafanyakazi hao huletwa na
ndugu zao wenye madaraka makubwa katika hoteli hizo bila kujali taaluma
zao, na wakati mwingine hufanya kazi za kawaida ambazo kisheria
zinatakiwa kufanywa na wafanyakazi wazawa.
Gazeti hili limenasa orodha ya wafanyakazi wa moja ya hoteli kubwa
maarufu zilizopo eneo la Kunduchi, yenye wafanyakazi wa kigeni 29 ambao
takriban wote ni raia wa India ukiacha watendaji wachache wa juu kabisa.
Taarifa kutoka ndani ya hoteli hiyo ni kwamba wafanyakazi hao wengi
wao hawana ujuzi kabisa na kazi walizoajiriwa kufanya, hivyo baada ya
kuingia hufundishwa na wale wachache wazawa ambao hata hivyo
hawathaminiwi.
Ili kukwepa mkono wa sheria za nchi kuhusu wageni kufanya kazi
zinazoweza kufanywa na Watanzania wazalendo, baadhi ya wafanyakazi hao
wasio na ujuzi (vihiyo), wamekuwa wakitumia majina tofauti hotelini hapo
badala ya yale yaliyoko kwenye pasi zao za kusafiria au nyaraka za
Idara ya Uhamiaji.
Baadhi ya wafanyakazi wazalendo wa hotelini hapo, walilidokeza gazeti
hili kuwa mchezo huo umekuwa ukifanywa kwa ushirikiano wa watendaji
wasio waaminifu ndani ya Idara ya Uhamiaji na wamiliki wa hoteli hiyo.
“Tumelalamika sana juu ya mchezo huu unaotunyima ajira, maana kazi
wanazofanya hawana ujuzi nazo, tunawafundisha sisi, lakini wanaajiriwa
wao na kulipana mishahara mikubwa; watu wa Uhamiaji tukiwaambia wanakuja
wanazungumza na wamiliki mambo yanaishia hapo na kama haitoshi
wanatutaja majina kwa wamiliki tunafukuzwa kazi kwa kutoa siri za
ofisi,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao wazalendo.
Katika orodha ya wafanyakazi wa kigeni 29 wa hoteli hiyo ambayo gazeti
hili lina nakala yake, kazi zilizoainishwa nyingi ni za kawaida kama
ufundi, udaktari, umeneja stoo, uhasibu na nyinginezo ambazo kimsingi
wako Watanzania wengi wenye ujuzi wa kuzifanya.
“Yaani hapa ukiingia humu ndani utashangaa kuona watu wanavyoweza
kwenda kwao kuleta ndugu, wake, waume na jamaa zao na kuwajaza kazini
kwenye vitengo nyeti wakati hawafanyi lolote. Tunaye Store Controller,
lakini ukisoma kibali chake cha kazi anatambulishwa kama Operation
Manager,” kilisema chanzo chetu.
Vile vile katika orodha hiyo yuko mfanyakazi mmoja anatajwa kama
injinia, lakini wafanyakazi wenzake wanasema hajui lolote, hatua
inayowafanya kuiomba serikali kuingilia kati kuzikagua hoteli hizo ili
kubaini kama wahusika wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria za nchi na
vibali vyao.
Nafasi za juu ambazo zinashikiliwa na wafanyakazi wazalendo hotelini
hapo ni mbili, moja ikiwa ya Meneja Rasilimali Watu, ambaye hata hivyo
anatajwa kutokuwa na kauli kwani wafanyakazi wazalendo wanapomlalamikia
hawapi majibu ya kujitosheleza akidai kuwa yeye analetewa wafanyakazi na
wakubwa zake. Mwingine mwenye wadhifa mkubwa ni Meneja Ulinzi.
Juhudi za kuwatafuta wasemaji wa hoteli hiyo, waziri mwenye dhamana na
kazi pamoja na Idara ya Uhamiaji zinaendelea kutokana na jana kuwa siku
ya wikiendi na hivyo watendaji hao kuwa mapumzikoni.
CHANZO:TANZANIADAIMA
|
No comments:
Post a Comment