Naibu mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Jack Zoka, akiongea na waandishi wa habari.
Amekanusha Usalama wa Taifa, TISS, kuhusishwa na utekaji nyara wa Dr. Ulimboka.
Katika siku za hivi karibuni, kumejitokeza taarifa zenye tuhuma kadhaa dhidi ya Idara ya Usalama wa Taifa. Taarifa hizo zimekuwa zikitolewa kwenye vyombo vya habari zikiihusisha Idara hii na matukio ambayo yanaidhalilisha na kuzua maswali mengi kwa wananchi. Kati ya tuhuma hizo ni tukio la kutekwa kwa Dr. STEPHEN ULIMBOKA, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari na madai ya kufanywa kwa mipango ya kuwadhuru baadhi ya Viongozi wa Vyama vya Upinzani. Gazeti moja la kila wiki limekuwa likurudia tuhuma hizo mara kwa mara kwa madai kwamba ni habari za uchunguzi na kuihusisha Idara.
Idara inataka kuwahakikishia wananchi kwamba taarifa hizo ni za UZUSHI NA UONGO ambazo zina nia ya kuharibu jina na sifa ya Idara. Taarifa hizo zimekuwa zikiunganishaunganisha vipande vya taarifa mbalimbali ili kukidhi malengo yaliyokusudiwa na wanaolitumia gazeti hilo. Idara haikuhusika wala haihusiki na matukio yoyote yaliyotajwa katika tuhuma hizo. Hivyo tunawaomba wananchi wazipuuze taarifa hizo.
Matukio yaliyotajwa katika tuhuma hizo yanachunguzwa na Jeshi la Polisi ambacho ndicho Chombo Chenye Dhamana, na kwa Maslahi ya Taifa si vizuri kuachia upotoshaji huo uendelee.
Aidha, tunapenda kuwahakikishia Watanzania kuwa uzushi na tuhuma zinazotolewa dhidi ya Idara hazitatuvunja moyo bali zitatuunganisha na hivyo kutuimarisha katika azma yetu ya kuhakikisha nchi yetu inaendelea kubaki salama kwa kushirikiana na wanachi na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama.
Imetolewa na Idara ya Usalama wa Taifa,
Makao Makuu,
DAR ES SALAAM
26 Julai, 2012.
No comments:
Post a Comment