Tuesday, 2 October 2012

Wanafunzi 20 wauawa na Boko Haram


Abubakar Shekahu kiongozi wa kundi la Boko Haram
Takriban wanafunzi 20 wameuawa kwa kupigwa risasi katika eneo la Mubi, Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.
Polisi wamefahamisha BBC kuwa shambulizi hilo limetokea katika dahalia ya wanafunzo(Hostel) mbali kidogo na chuo cha ufundi anuwai cha Mubi.
Mhadhiri mmoja amefahamisha BBC kuwa wanafunzi 40 wameuawa lakini bado taarifa hizo hazijathibitishwa.
Mauaji haya yanakuja siku chache baada ya operesheni kali kufanywa dhidi ya kundi la wapiganaji wa kiisilamu la Boko Haram mjini humo.
Aidha mhadhiri ambaye hakutaka kutajwa, aliambia BBC kwamba wanafunzi waliamrishwa kupanga foleni na kusema majina yao mmoja baada ya mwingine kabla ya kuuawa.
Haijulikani kwa nini baadhi waliuawa na wengine kuachwa, baadhi ya wale waliouawa ni waisilamu.
"kila mtu anaogopa na wamejifungia vyumbani," alisema mhadhiri huyo.
Aliongeza kuwa wanafunzi sasa wameanza kuuhama mji huo. Inasemekana wameweka majani ya rangi ya kijani kibichi kwenye magari yao kama ishara kuwa hawaungi mkono upande wowote.
Wapiganaji wa Boko Haram wanaopigana wakitaka sheria za kiisilamu kutumika, wamewaua zaidi ya watu 1,000 Kaskazini mwa Nigeria.

BBC

No comments:

Post a Comment