Tuesday 17 September 2013

Ratiba ya mastaa wa kibongo na kuuza unga


Na Gladness Mallya
IMEBAINIKA kwamba ukifuatilia ratiba za maisha ya anasa ya kila siku ya mastaa wa Kibongo, lazima utajiuliza kwa nini wasiuze au kusafirisha madawa ya kulevya ‘unga’? Ijumaa Wikienda lina ripoti ya kushangaza.
Masogange.
Uchunguzi wa gazeti hili uliopewa sapoti na baadhi ya mastaa hao, ulibaini kwamba suala la kupenda kujirusha kuliko kazi ndiyo chanzo cha kufanywa ‘punda’ wa kusafirisha unga na matokeo yake kunaswa na kuingia kwenye matatizo makubwa.
Uchunguzi huo ulibaini kuwa kuna baadhi ya mastaa hao, ratiba zao za kujirusha na kula bata ndefu zimewabana kiasi cha kushindwa kuendeleza vipaji vyao katika sanaa.
Ratiba za baadhi ya mastaa hao za kujirusha ni kama ifuatavyo;

Odama.

JUMATANO
Ilibainika kuwa Jumatano, baadhi ya mastaa hao hupenda kwenda kujirusha kwenye kumbi za starehe hasa katika Klabu ya Bilicanas, Posta ambako mara nyingi kunakuwa na bendi inayomwaga burudani huku wakishushia na pombe.
Ilibainika kuwa mastaa hao huondoka kwenye kumbi hizo za starehe karibia kunakucha (majogoo) huku wakiwa ‘tilalila’ na kwenda kulala.

Aunt Lulu.

ALHAMISI
Data zilizopatika kwa kumsoma msanii mmoja baada ya mwingine zilibaini kwamba, kwa kuwa huchelewa kulala Jumatano huku wakiwa na uchovu, Alhamisi huamka saa 10:00 jioni kisha kuchati kidogo na marafiki kabla ya usiku kwenda kujirusha hasa New Maisha Club kunakokuwa na burudani ya bendi.
Ilibainika kwamba wakiwa humo hujiachia kwa ‘masebene’ na kugonga pombe kama ilivyokuwa jana yake hadi majogoo.

Baby Madaha.

IJUMAA
Uchunguzi ulibaini kuwa siku ya Ijumaa, baadhi ya mastaa hao huamka tena saa 10:00 jioni na kinachoonekana ni kati ya siku ‘bize’ kwa mambo ya starehe hivyo wanakuwa na mialiko mingi.
Ilibainika kuwa baadhi yao huhudhuria mialiko ya sherehe za harusi, send-off, kitchen party, birthday na nyinginezo kabla ya baadaye kumalizia kwa kwenda kwenye ‘live’ bendi.
Mara nyingi hupenda kuhudhuria kwenye shoo kama hizo katika Kumbi za Thai Village, Masaki, Nyumbani Lounge, Ada Estate, Kinondoni au Club 24, Mikocheni ambako huko nako hukesha hadi majogoo.

Melisa.

JUMAMOSI
Uchunguzi wetu ulibaini kwamba Jumamosi, baadhi ya mastaa hao huamka saa 10:00 jioni kama kawa kisha kunyoosha miguu hadi baa ambapo giza likiingia huzama tena kwenye burudani ya bendi.
Wengi hupatikana katika kumbi zinazoungurumisha muziki wa bendi za dansi. Huko nako huwa wanakula bata ndefu hadi majogoo kisha kurejea nyumbani kulala.
Jack Patrick.

JUMAPILI
Kama kawaida, baadhi ya mastaa hao huamka saa 10:00 jioni kisha kwenda kujipumzisha ufukweni hasa Coco na kuendelea kujirusha. Usiku mnene ‘hujimuvuzisha’ kwenye klabu za starehe ambapo ama msanii wa Bongo Fleva anazindua wimbo au kunakuwa na shoo ya kawaida ya muziki.
Kumbi za starehe zinazokuwa ‘bize’ na mastaa huku kukiwa na shoo usiku wa Jumapili ni pamoja na Bilicanas na New Maisha Club ambako huko nako huondoka majogoo kwenda kulala.

JUMATATU
Ilifahamika kuwa siku ya Jumatatu baadhi ya mastaa hao huamka saa 7:00 mchana kisha kwenda saluni na baadaye kufanya ‘window shopping’ katika maduka ya nguo, supermarket na sehemu nyingine.
Baada ya hapo muda wa jioni, baadhi ya mastaa hao hupendelea kwenda kuogelea (swimming) kisha kuibuka Coco Beach kupata mihogo ya kuchoma, mishikaki, ‘shisha’, pombe na starehe nyingine za kiutu uzima.

JUMANNE
Mara nyingi uchunguzi wetu ulibaini kuwa siku ya Jumanne hutumiwa na wasanii hao kupumzika kutokana na uchovu wa wiki nzima kabla ya ratiba kujirudiana tena kuanzia Jumatano.

WENYEWE WANASEMAJE?
Gazeti hili lilizungumza na baadhi ya mastaa wachache wa kike kuhusu suala la kujirusha ambapo kila mmoja alifungukia ratiba yake.

BABY MADAHA
“Mimi naweza kujiachia kila siku lakini mara nyingi natoka siku tano na ratiba zinaendelea kama kawa maana huwa nalala mchana na nikitoka narudi saa 9:00 usiku.”

MIRIAM JOLWA ‘JINI KABULA’
“Siku hizi natoka mara mojamoja siyo kama zamani lakini nikiwa na kampani huwa narudi kulala saa 10:00 usiku.”

TAMRINA POSHI ‘AMANDA’
“Mimi huwa natoka kwenye ishu maalum tu.”
JACQUELINE PATRIC
“Naweza nisitoke wiki nzima lakini nikijisikia pia naweza kutoka wiki nzima na mambo mengine yanaendelea.”

WATOTO WA MBWA (TIKO, MARY & THEKLA)
“Siku hizi huwa tunatoka siku maalum, siyo kama zamani.”

YOBNESH YUSUF ‘BATULI’
“Inategemea, kama nimealikwa sehemu narudi saa 10:00 usiku au asubuhi maana kazi zetu siyo za kila siku.”

LULU MATHIAS  ‘AUNTY LULU’
“Huwa natoka siku ya Ijumaa narudi saa 8:00 usiku naamka 4:00 asubuhi. Pia natoka Jumapili kwa sababu Jumatatu nakuwa off.”

KWA NINI WASIUZE UNGA?
Uchambuzi wa kina ulibaini kuwa mbali na starehe hizo, pia kuna masuala ya mapenzi ambayo nayo huwa ni gharama na pia hutumia muda wao mwingi.
Ilibumburuka kuwa kwa staili hiyo ya maisha ya anasa huku baadhi wakisahau kwenda studio kurekodi na mazoezi ya shoo (kwa wanamuziki) na kutoonekana lokesheni wakishuti filamu.
Ilifahamika kwamba kwa ratiba hizo, anapotokea kigogo (mfanyabiashara wa madawa ya kulevya) na ‘kumsomesha’ msanii kuwa kuna dili la unga lazima akubali kuwa punda ili apate fedha za harakaharaka za kutanulia asiachwe na watoto wa mjini.
Listi inazidi kuongezeka kila kukicha ya mastaa mbalimbali ambao wanadaiwa kunaswa na unga wakiwemo Agness Gelard ‘Masogange’ na shosti yake, Mellisa Edward, Sandra Khan ‘Binti Kiziwi’, Saadah Ally, Aisha Bui, Mkwanda na Mbwana Matumla, Joseph Kaniki na wengi
neo.

No comments:

Post a Comment