Monday 8 November 2010

MAMBO JUU YA MAMBO KITI CHA SPIKA

CHENGE

KINYANGANYIRO CHA USPIKA: Chenge aushambulia uongozi wa Spika Sitta

MMOJA wa wanachama wa CCM walioomba nafasi ya kuliongoza Bunge la Jamhuri, Andrew Chenge jana alitumia muda mwingi kuuponda uongozi wa Spika Samuel Sitta huku akisita kuweka bayana alikopata fedha zilizoibuliwa kwenye uchunguzi wa kashfa ya ununuzi wa rada.

Chenge, ambaye alijiuzulu wadhifa wake wa Waziri wa Miundombinu kutokana na kuhusishwa kwenye kashfa hiyo iliyochunguzwa na Taasisi ya Makosa Makubwa ya Jinai (SFO) ya Uingereza, aliitisha mkutano na waandishi wa habari jana kuelezea nia yake ya kugombea uspika wa Bunge la Jamhuri na kufafanua "makandokando yanayolizunguka jina langu".

Wakati alikuwa na wakati mgumu kujibu maswali kuhusu tuhuma zinazomkabili, Chenge alitumia mkutano huo kueleza kile alichokiita udhaifu wa uongozi wa Bunge la Tisa, akisema kwa miaka mitano iliyopita kulikuwa na ombwe la uongozi.

"Na hili ndilo lilinisukumu kugombea nafasi ya Spika wa Bunge," alisema Chenge ambaye taarifa aliyowaandalia waandishi iliandikwa kwa mkono bila ya kuchapishwa.

Bila ya kumtaja jina kiongozi wa Bunge, Chenge alidai uongozi uliopita ulikuwa wa kinafiki; wa majungu; uzandiki na kila aina ya mbinu za kuwapaka watu matope kwa lengo la kujijengea umaarufu binafsi.

Alidai kuwa uongozi uliopita ulitumia mwingi kuruhusu hoja binafsi ambazo hazikuwa na maslahi kwa taifa, kitu ambacho alisema kilimfanya aaumue kuingia kwenye kinyang'anyiro cha uspika.

Chenge aliorodhesha kazi za Spika wa Bunge, akisema kuwa anatakiwa awe kama refa ambaye anasimamia kanuni za mchezo na kuitumia dhana ya wengi wape, ambayo alisema haikuheshimiwa na uongozi uliopita.

Alisema katika bunge lililo kwenye utawala wa kidemokrasia, huwa kuna wabunge kutoka chama tawala na wa upinzani na kwamba wale wa chama tawala wana haki ya kuikosoa serikali yao kwa lengo la kuboresha utendaji wake kwa kuzingatia kanuni.

Alisema wabunge kutoka vyama vya upinzani huikosoa serikali kwa lengo la kuidhoofisha na ikiwezekana hata kuiondoa madarakani.

"Kilichotokea wabunge wote wa chama tawala na upinzani waliungana dhidi ya serikali... hii si sahihi," alisema Chenge. "Chama tawala kimepewa fursa ya kutoa maagizo kwa serikali... chama kilichopata ridhaa ya wananchi kupitia kura zao, lazima kipewew fursa ya kwanza ya kutekeleza programu zake bila ya kuathiri haki za wachache kutoa maoni yao."

Alisema hiyo haikufanyika kutokana na uongozi uliopita kuwa na udhaifu.

"Uongozi wa namna hiyo ni wa kuogopa kama ugonjwa wa Ukimwi," alisema mwanasheria huyo mkuu wa zamani wa serikali.

"Nikiwa spika nitatoa nafasi kubwa kwa wabunge walio wengi ambao ni wa CCM na kuipa nafasi serikali kuwasilisha miswada yake ya sheria na kutekeleza programu zake za maendeleo kwa mujibu wa kanuni."

Samuel Sitta alikuwa Spika wa Bunge la Tisa ambalo limeingia kwenye historia kama Bunge lililokuwa na mijadala mikali na huru iliyosababisha mabadiliko makubwa ndani na nje ya Bunge, ikiwa ni pamoja na ubadilishaji wa kanuni za Bunge na uchunguzi wa kashfa mbalimbali.

Bunge hilo pia lilijadili kwa kina tuhuma mbalimbali za ufisadi, ikiwemo ya zabuni ya uzalishaji umeme wa dharura iliyokwenda kwa kampuni ya Richmond Development na kusababisha Edward Lowassa kujizulu wadhifa wake wa waziri mkuu.

Chenge pia alifafanua makandokando yanayozunguka jina lake akisema ni maneno ya hisia dhidi yake.
Alitaja makandokando hayo kuwa ni kuisababishia taifa hasara kubwa kutokana na mikataba mibovu, kuchunguzwa na SFO na kuhusika kwenye ununuzi wa rada.

"Wengine wanasema sijui rada. Kwa ufahamu wangu jalada la rada lilikwishafungwa na SFO," alisema akizungumzia kuhusishwa kwenye kashfa ya ununuzi wa rada ambayo uchunguzi uliofanywa na taasisi hiyo ya Uingereza ulibaini kuwa waziri huyo wa zamani alikuwa na Sh1.2 bilioni kwenye akaunti yake iliyokuwa kwenye benki moja mjini Jersey.

"Nawaomba wanahabari muwe na ujasiri wa kwenda kwenye ofisi husika, Takukuru na DPP, wakanushe au kuthibitisha ufahamu wangu..., msipokuwa na huo ujasiri mkome kulihusisha jina langu na kile kinachoitwa rushwa ya ununuzi wa rada," alisema Chenge.

Chenge ambaye alijaribu kuzungumza kwa ujasiri kuhusu kashfa zake, alijikuta akikabiliana na maswali mengi kuhusu tuhuma mbalimbali zinazomkabili na akaishia kuvituhumu baadhi ya vyombo vya habari akidai vinaipeleka nchi kubaya.

"Baadhi ya media (vyombo vya habari) vinalipeleka taifa letu pabaya..., tunachonganisha ndugu kwa mifarakano, mara kuwapachika majina kama mafisadi," alilalamika Chenge.

Kuhusu sehemu alikopata kiwango hicho kikubwa cha fedha wakati akiwa mtumishi wa umma, Chenge alijibu: "Kuhusu wapi nimepata fedha hizo, siwezi kueleza kwa sababu na mimi nina haki zangu kikatiba. Ndiyo maana tunajaza fomu za maadili."

"Kiutaratibu, mtu mwadilifu anapoomba uongozi wa umma huwa anapaswa kutamka mali zake kwa kuwa miongoni mwa sifa zinazombainisha kuwa kiongozi bora ni pamoja na kutokuwa mlarushwa, mwenye kuheshimu mali za umma, muwazi na mkweli.

"Hizi ni fedha za Trust (mfuko). Katika Trust kuna wadhamini na mimi ni mmoja wao kwa upande mmoja na upande mwingine yupo mke wangu Tina Chenge. Kama kuna mtu kasema nimeuza ng'ombe wa ukoo huyo ni yeye."

Chenge alikuwa akizungumzia kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba ambaye baada ya akaunti ya Chenge kukutwa na kiasi hicho cha fedha katika uchunguzi wa SFO, alinukuliwa na gazeti hili akisema "hata mimi sielewi labda kama kauza ng'ombe wao wote wa ukoo".

Chenge alijitetea kuwa fedha hizo zina malengo ambayo ni kusaidia yatima na wasiojiweza, lakini akisita kutaja jina la mfuko wenyewe, mahali ulipo na yeye aliwekeza kiasi gani zaidi ya kusema, "na mimi niliweka fedha zangu humo".

Kuhusu tuhuma za kuiingiza nchi kwenye mikataba mibovu wakati akiwa Mwanasheria Mkuu, mbunge huyo wa Bariadi Mashariki alisema kazi ya Mwanasheria Mkuu ni kuangalia kama mikataba imetimiza masharti ya sheria za nchi na kama imepata baraka za Baraza la Mawazira na kuongeza kusema "hata waziri mwenye dhamana na sekta fulani hawezi kusaini mkataba bila kupata baraka za Baraza la Mawaziri".

Chenge alitwisha mzigo huo wa kusaini mikataba kwa baraza la mawaziri, wataalamu na hata marais akisema kuwa kutaratibu mikataba haiwezi kusainiwa bila kupita ngazi hizo kwa ajili ya kupata vibali.

Alitoa mfano wa mkataba uzalishaji umeme wa baina ya serikali na kampuni binafsi ya Independent Power Limited (IPTL), akisema ulipata baraka za baraza hilo.

"Baraza la mawaziri liliidhinisha mkataba wa IPTL; kingine ni matatizo ya kitaalamu... kama labda Tanzania ilihitaji megawati 40 kwa dola 100, hilo si suala la kisheria."

Kuhusu maoni yake dhidi kesi yake ya uendeshaji gari kizembe uliosababisha vifo vya watu wawili, Chenge alihoji: "Nani kati yenu ana uhakika akitoka hapa atafika nyumbani salama?

"Ile ni ajali tu, hata mimi sikupenda itokee na inaweza kumtokea mtu yeyote. Ila sipendi kuingia kwa undani kwani tayari jambo hilo liko mahakamani, lakini nasema hicho si kikwazo kwangu."

Baadhi ya vyombo vya habari jana viliripoti mkakati wa kundi la watuhumiwa wa ufisadi ndani ya CCM ambalo linadaiwa kutaka kuhakikisha jina la Sitta halipiti katika ngazi ya kamati kuu ya chama hicho tawala kwa hofu kwamba likipita mbunge huyo wa Urambo Mashariki atafanikiwa kurejea kwenye kiti chake.

Leo ni mwisho wa wanachama wa CCM kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo na uteuzi wa wagombea watatu watakaopelekwa kwenye mkutabno wa wabunge wa chama hicho ili kupigiwa kura utafanyika Novemba 12.

Mbali na Sitta na Chenge, wengine waliochukua fomu kuwania nafasi hiyo ya juu kwenye muhimili huo wa nchi ni pamoja na Anna Makinda, ambaye ni Naibu Spika w a Bunge la Tisa, Anna Abdallah, Kate Kamba na Jobu Ndugai ambaye alikuwa mwenyekiti wa Bunge lililomaliza muda wake.


CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment