WABUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wameigomea Serikali wakitaka isilipe kabisa fidia ya Sh94 bilioni dhidi ya Kampuni ya Dowans, iliyorithi mkataba wa kifisadi wa Richmond au deni hilo lipunguzwe.
Tayari sakata hilo limekwishaitikisa Serikali ya CCM huku kukiwa na shinikizo kubwa la wanaharakati wa mashirika 11 ambao wamefungua kesi Mahakama Kuu kukata rufaa, kupinga malipo hayo.
Hata hivyo, joto hilo la Dowans lililipanda zaidi jana katika siku ya mwisho ya kikao cha wabunge wote wa CCM ambao walikutana kwa siku mbili tangu juzi chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete.
Kwa mujibu wa duru za ndani za kikao hicho nyeti cha chama ambacho kimefanyika siku chache kabla ya mkutano wa Bunge la 10, asilimia kubwa ya wabunge walitoa msimamo dhahiri wakitaka deni hilo lisilipwe huku wengine wakitaka lipunguzwe.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye ni mkuu wa shughuli za Serikali bungeni anayetarajiwa kukumbana na sakata hilo katika Bunge linaloanza Februari 8, alithibitisha mapendekezo hayo mawili na kuongeza, "Serikali imekubaliana na ushauri wa kamati."
"Serikali imekubali kamati ya wabunge wa CCM kuhusu Dowans kuona kama inaweza ama kupunguza au kuliondoa kabisa deni hili ili kupunguzia mzigo Watanzania," alifafanua Waziri Mkuu Pinda wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alifafanua kwamba, uamuzi huo umekuja baada ya kamati hiyo kuishauri Serikali kuhusu deni hilo.
Waziri Mkuu aliongeza kwamba, Dowans ina historia ndefu ambayo ni kuanzia Richmond na kuongeza kwamba, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), inaweza kuzamia katika hilo kuona kama kuna mianya ya rushwa na kuongeza, "Ingawa hadi sasa sijapata taarifa zozote za namna hiyo."
Pinda maarufu kama mtoto wa mkulima, aliweka bayana kwamba wakati wa mjadala kuhusu kuilipa au kutoilipa Dowans au kupunguza deni, walijitokeza wabunge wa CCM ambao kitaaluma ni wanasheria walikubali kujitolea kuisadia Serikali katika hilo.
kuhusu Dowans kurudishwa bungeni, Waziri Mkuu alisema hayo ni maoni ya watu ambao wana uhuru wa kufanya hivyo huku akisisitiza, kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni ingawa katika hilo kulirudisha bungeni itakuwa ni kujadili sheria juu ya sheria na kwamba litaangaliwa kwa makini.
Pinda aliongeza katika kulifanyia kazi vema sakata hilo, "'ndiyo maana kamati imeshauri Serikali isikilize ushauri wa kisheria na jaji atoe ushauri wake."
Kuhusu kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema kwamba fedha hizo lazima zilipwe na hakuna jinsi, Pinda alisema tatizo lililokuwepo awali ni kwamba kila mtu alipoulizwa na chombo cha habari aliweza kutoa kauli kwani kama asingesema vyombo vingeandika Serikali yagoma kuzungumzia Dowans.
Pinda akizungumzia mvutano wa hoja kati ya mawziri, alisema ndiyo maana imefanyika semina hiyo kwa lengo la kuondoa tofauti na kuwezesha mawaziri kuweza kuzungumza mambo bila kutofautiana.
Lakini, duru za ndani zaidi kutoka kikao hicho zilisema wabunge wengi wa CCM wakiongozwa na Waziri wa Afrika Mashariki Samuel Sitta na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe, ambao kitaaluma ni wanasheria ndiyo walibadili upepo wa kisiasa ndani ya kikao hicho.
Mawaziri hao kwa mujibu wa duru hizo, waliwezesha wabunge wa CCM kutoa azimio hilo wakati wa mada ya hali ya umeme nchini iliyowasilishwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima ambaye alipendekeza kwa wabunge kutoa mawazo jinsi Serikali inavyoweza kuepuka kubeba mzigo huo.
Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho zilisema kuwa mjadala mzima wa masuala ya nishati ya umeme yalijikita katika suala la Dowans na kwamba wabunge wote wapatao 10 waliochangia mada hiyo walipendekeza Serikali kutolipa fedha hizo.
Miongoni mwa wabunge waliochangia mada hiyo mbele ya Rais Kikwete na Waziri Mkuu, Pinda aliyekuwa Mwenyekiti wa kikao hicho ni Waziri Sitta, , Dk Mwakyembe na Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka.
Duru zaidi zilifafanua kwamba, hata Rais Kikwete alipozumgumzia suala hilo alitamka wazi kwamba linalomuumiza sana, huku akiweka bayana amekuwa akijadiliana na Waziri Mkuu kuona kama linaweza kuepukwa.
Taarifa hizo zilimnukuu Naibu Waziri Malima akiwaambia wabunge kwamba, fedha hizo ni nyingi, lakini wizara haikuwa na la kufanya kutokana na ushauri waliopewa na AG Werema kwamba hakuna jinsi wanavyoweza kukwepa kulipa.
Kauli hiyo ya Malima inatotafautiana na ile ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja ambaye aliutangazia umma kwamba Serikali inajipanga kuilipa Dowans kiasi hicho cha fedha, hatua ambayo imekuwa ikipigiwa kelele na wananchi wengi.
Ngeleja hakuhudhuria semina hiyo ya wabunge wa CCM na haikufahamika mara moja sababu za kutokuhudhuria kwake.
Mara baada ya Rais Kikwete kufunga rasmi semina hiyo ya wabunge wa CCM, baadhi yao walionekana wakimpa mkono Malima, huku baadhi yao wakimpongeza kwa kile walichosema kuwa ni ujasiri wa kusema kweli.
Katika maazimio yao, wabunge wa CCM walisema suala hilo lirejeshwe serikalini na kufanyiwa uchunguzi upya na kwamba lifanyike kila linalowezekana kuhakikisha fedha hizo hazilipwi.
Uchunguzi uliopendekezwa na wabunge ni ule unaohusu uhusiano baina ya kampuni ya awali ya Richmond na Dowans, pamoja na jinsi kampuni hizo mbili zilivyoingia mkataba wa kuzalisha umeme.
Kadhalika, wabunge hao wa CCM wanataka kupatikana kwa mwenendo wa kesi hiyo kwani wengi wao katika kuchangia kwao walionekana kutilia mashaka.
Taarifa kutoka ndani ya semina hiyo ya siku tatu zinadai kuwa Rais Kikwete alisema anakubaliana na mawazo ya wabunge kwamba fedha hizo ni nyingi sana, huku akitamka bayana kwamba hilo ni, “suala linalomuumiza sana .”
Awali, ilielezwa baada ya hoja za kisheria za Dk Mwakyembe alisimama mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrodi Mkono, aliyejitolea akisema ataisaidia Serikali kuhakikisha ama deni hilo linapunguzwa au halilipwi.
Tangu kutangazwa kwa uamuzi wa ICC wa Noovemba mwaka jana, sakata hilo la Dowans limeibua mjadala mzito katika CCM na Baraza la Mawaziri.
SOURCE:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment