Wednesday 3 August 2011

ATCL hoi bin taabani: Serikali

Tuesday, 02 August 2011 19:47

NDEGE zote zilizonunuliwa miaka 37 wakati wa kuanzishwa kwa Shirika la Ndege Tanzania(ATCL), hazifanyi kazi, Bunge lilielezwa jana.Akijibu swali la nyongeza kutoka kwa David Kafulila (NCCR-Mageuzi- Kigoma Kusini), Waziri wa Uchukuzi,
Omari Nundu alisema shirika hilo lilianzishwa mwaka 1973 na kupewa ndege 11 kama kianzio, lakini kwa sasa hakuna hata moja inayofanya kazi. Katika swali lake,
Kafulila alitaka kujua kuna ndege ngapi zinazofanya kazi na akahoji ni kwa nini kwa muda mrefu Tanzania inashindwa kuwa hata na ndege moja kama ilivyo kwa nchi ndogo kama Burundi.Awali, katika swali la msingi,
Rukia Ahmed (Viti Maalum-CUF) alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kusafisha menejimenti pamoja na shirika hilo. Mbunge huyo pia alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kufufua Shirika la ndege la Tanzania kutokana na shirika hilo kuonekana kuelekea kufa.Naibu Waziri wa Uchukuzi, Athuman Mfutakamba alisema Serikali inatambua na kutafuta namna bora ya kulifufua shirika hilo ili liweze kuwa imara kama ambavyo Watanzania wanatarajia.
 Alisema kuwa Serikali iko katika mchakato wa kuteua menejimenti na bodi mpya ambayo itakuwa na uwezo wa kusimamia Kampuni ya Ndege ya Tanzania ili iweze kufikia malengo. Naibu Waziri alisema kwa sasa Serikali inatarajia kuipatia kampuni vitendea kazi na mtaji wa kujiendesha ili iweze kuendeshwa kwa biashara bila ya kutegemea ruzuku kutoka serikalini.
Alisema serikali iko mbioni kumpata mbia mahiri na mwenye uwezo wa kubadilisha ATCL iweze kutoa huduma za hali ya juu kwa ufanisi mkubwa sambamba na kampuni zingine nchini. Kwa mujibu wa Naibu Waziri, ndege iliyokuwa kwenye metengenezo nchini Afrika ya Kusini, inatarajia kurudi nchini Agosti 8 kwa kuwa sasa iko tayari kwa ajili ya kutoa huduma.

mwananchi 

No comments:

Post a Comment