Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal
ametoa mhadhara kuhusu changamoto za kisayansi katika maadhimisho ya
miaka 50 ya Idara ya Sayansi za Kimataifa kwa kifupi ISP ya Chuo Kikuu
cha Uppsala kilichopo Uswidi ambapo amefafanua kuwa, mchango wa
wanasayansi kutoka katika chuo hiki una manufaa makubwa katika kukuza
teknolojia katika sayansi kwa nchi za Afrika.
Makamu
wa Rais ambaye alikuwa mhadhiri wa somo la Fizikia katika Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam kabla ya kuingia katika siasa, amealikwa na
wanasayansi wa kariba yake katika maadhimisho haya yaliyo na lengo la
kutanua uwanda wa tafiti katika nchi za Afrika na hasa Tanzania, ambayo
kwa sasa imeanzisha chuo kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson
Mandela kilichopo Arusha.
Katika
ziara hii ambayo Makamu wa Rais ameambatana na Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, Waziri wa nchi
Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Telezya Huvisa, Naibu Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim pamoja
na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela
Profesa Burton Mwamilwa.
Ujumbe
wa Makamu wa Rais ulifika hapa na kupata nafasi ya kuzungumza na
Watanzania waliopo Uppsala ambao wengi walitaka kujua kama Tanzania
imejipanga vema kukabiliana na tatizo la umeme nchini. Makamu wa Rais
ambaye katika ziara hii amekuwa akikutana na wanasayansi mbalimbali wa
Sweden na hasa waliobobea katika sekta ya nishati aliwaeleza Watanzania
waliokuwa katika mkutano naye kuwa; kama taifa tuna kila sababu ya
kukubali kuwa tulifanya makosa huko nyuma kwa kutotambua utanuaji wa
vyanzo vya umeme wa uhakika hali inayotuumiza sasa lakini pia akawaambia
kuwa serikali imejipanga vema kuhakikisha kuwa tatizo la umeme
linapata tiba katika kipindi kifupi na pia kuwa na umeme wa uhakika
katika miaka miwili ijayo.
Maeneo
makubwa ambayo Makamu wa Rais amekuwa akiwasikiliza kwa ukaribu
wanasayansi wa Uppsala na Sweden ni kuhusu vyanzo mbalimbali vya
uzalishaji wa umeme vikiwemo vile vya upepo na maji ya bahari huku pia
ikiwa Tanzania imeshasaini mkataba wa uzalishaji wa umeme wa makaa yam
awe na kampuni ya kutoka China, mkataba uliosainiwa wiki mbili
zilizopita katika ya NDC na kampuni ya China ambazo zitashirikiana
katika miradi mikubwa katika ukanda wa Mtwara.
Eneo
jingine ambalo Makamu wa Rais amekuja kulihamasisha ni juu ya uhusiano
wa chuo hiki kikongwe katika uwanja wa Sayansi na namna chuo hiki
kitakavyozidisha ushirikiano wake katika kusomesha wataalamu wa Tanzania
katika ngazi za Shahada za Uzamivu na mchango mkubwa ukiwa kukipatia
uwezo Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela kilichopo
Arusha.
Katika
ziara hii ya kitaaluma aliyoalikwa Makamu wa Rais inayochukua siku
mbili, Makamu wa Rais pia atakutana na Waziri wa Mambo ya Jamii wa
Uswidi Ulf Kristersson na Waziri wa Mahusiano na Maendeleo Gunilla
Carlsson. Katika ratiba hiyo pia Makamu wa Rais atatembelea Taasisi ya
Mazingira ya Uswidi sambamba na kuzungumzia mafanikio ya Kilimo Kwanza
kwa wadau wa maendeleo wa Uswidi.
No comments:
Post a Comment