ASEMA ALIWATAKA WATUMIE BUSARA, SPIKA ASISITIZA ALIRUHUSU, WANANCHI WACHACHAMAA
Waandishi Wetu
SIKU
moja baada ya Waziri Mkuu Mkuu, Mizengo Pinda kusema tayari Rais Jakaya
Kikwete amesaini kuidhinisha ongezeko la posho za vikao (sitting
allowance) kwa wabunge kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000 kwa siku, Ikulu
imetoa taarifa kukanusha madai hayo.Wakati Ikulu ikitoa taarifa hiyo,
jana Spika wa Bunge, Anne Makinda aliitisha mkutano wa waandishi wa
habari na kusema: “Siyo kwamba tutaanza kutoa, tulishaanza kutoa na Rais
(Jakaya Kikwete), ameshatoa kibali chake na mbunge atalipwa katika
vikao tu, si kila siku na tena baada ya kukaa kwenye vikao na kusaini.”
Lakini
katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais, Ikulu imesema: “Maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuhusu suala hili
yako wazi kabisa na hakuna mahali ambako Rais Kikwete amebariki posho
hizi.”
“Kwanza, Mheshimiwa Rais Kikwete anakubali haja ya
kuangalia upya posho kwa wabunge lakini amewataka wabunge kutumia hekima
na busara katika kulitafakari suala hili. Pili, Mheshimiwa Rais Kikwete
amewataka wabunge kutumia Kikao cha sasa cha Bunge kulizungumza upya
suala hilo.”
Juzi, Pinda aliwaambia wabunge ndani ya kikao cha
utangulizi kuwa tayari Rais Kikwete alikuwa ameidhinisha ongezeko la
posho za vikao kutoka Sh70,000 hadi Sh200, 000. Baada ya Waziri Mkuu
kusema hivyo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema)
alisimama na kudai kuwa taarifa alizonazo ni kwamba Rais Kikwete alikuwa
hajasaini kuidhinisha posho hizo.
Kauli ya Zitto ilisababisha
Mbunge wa Kondoa Kaskazini (CCM), Juma Mkamia kusimama na kuhoji iwapo
Zitto ni miongoni mwa wasemaji wa Rais kabla ya Pinda kusimama na
kuthibitisha kusainiwa posho hizo akisema, siyo ajabu kwani hata
watumishi wa Serikali wanalipwa kati ya Sh50,000 na Sh200,000.
Hata
hivyo, Zitto alitetea msimamo wake kwamba alitarajia baada ya kusainiwa
kwa posho hizo na Rais, angepewa masharti mapya ya kazi za ubunge.
Wengine walioshambuliwa katika kikao hicho ni Mbunge wa Bumbuli (CCM),
January Makamba na Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Khamis Kigwangwallah kwa
kupinga posho hadharani.Wanaodhaiwa kuwashambulia wabunge hawa
wanaopinga posho ni Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo, Mbunge wa
Sikonge, Said Nkumba, Nkamia na Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa
Suleiman Khalifa.
Jana baada ya kuripotiwa kwa habari hiyo
wananchi kutoka kila kona ya nchi walipinga huku wasomi wakitahadharisha
kuwa kitendo hicho kinaweza kuligawa taifa.
Wananchi wa kada
mbalimbali waliotuma maoni yao kwenye mtandao wa gazeti hili na wasomi
ambao walihojiwa walisema kwamba kitendo hicho ni hatari hasa katika
kipindi hiki cha mgomo wa madaktari.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo
Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Profesa Gaudence Mpangala alisema nyongeza
hiyo inaleta utata na kwamba inaonyesha wazi kuwa nchi inanyemelewa na
dalili za kuwepo kwa matabaka... “Hii inaonyesha kuwa wapo
wanaopendelewa na wengine wanaminywa, jambo hili kiutawala si zuri hata
kidogo linaweza kuleta migomo na maandamano nchi nzima.”
Alisema
Serikali inatakiwa kuzitazama sekta nyingine huku akitolea mfano mgomo
wa madaktari na kuongeza: “Yaani baada ya kutatua hali hii ya mgomo wao
ndiyo wanapandisha posho za wabunge. Gharama za maisha ziko juu sana,
hilo lazima Serikali ilitambue.”
Mhadhiri mwingine mwandamizi wa
chuo hicho, Dk Kitila Mkumbo alisema kauli ya Waziri Mkuu Pinda imetoa
majibu sahihi kwamba Serikali ina fedha za kutosha za kuwalipa
madaktari.”
“Pinda alikaririwa akisema kuwa Serikali haina fedha
za kuwalipa madaktari, lakini hizo za kuwalipa wabunge zimepatikana,
sijui hapa inakuwaje?,” alihoji Dk Mkumbo.
Alisema kiwango cha
fedha za nyongeza hizo za posho ambacho watalipwa wabunge katika kikao
cha Bunge la Juni, zinaweza kuwalipa madaktari waliogoma nchi nzima.
“Mwezi
wa sita wabunge hukaa bungeni miezi miwili, sasa ukipiga hesabu za
haraka haraka kiwango cha posho watakazolipwa kinatosha kabisa kumaliza
kero ya madaktari,” alisema Dk Mkumbo.
Kwa upande wake, Mhadhiri
mwingine wa UDSM , Dk Benson Bana alielezea kushangazwa kwake na kitendo
cha Serikali kupandisha kiwango cha posho licha ya kuwa suala hilo
limepigwa kelele na wananchi... “Posho za vikao (Sitting allowances)
siyo kipaumbele chetu, posho hizi hazina uhusiano na utendaji wa
mbunge.”
Alisema suala hilo licha ya kutia wasiwasi, linaibua
maswali mengi kwa kuwa walimu na madaktari nao wanataka kulipwa vizuri
ikiwa ni pamoja na nyongeza ya posho.
“Ningewaelewa kama
wangeongeza mishahara ya wabunge lakini siyo posho…, posho ambazo
wanalipwa katika saa za kazi, haiingii akilini hata kidogo.” alisema Dk
Bana.
Naye Profesa Tolly Mbwete wa Chuo Kikuu Huria (OUT),
alisema nyongeza hiyo ya posho inatakiwa kufanyika katika sekta zote ili
kupunguza malalamiko ya watu wa kada mbalimbali. “Binafsi naona suala
hili linatakiwa kutazamwa katika sekta zote kuliko kujikita kwa wabunge
tu.”
Mwanasheria wa kujitegemea, Profesa Abdallah Safari alisema
posho hizo hazina mashiko kwa kuwa wanaolipwa wanakuwa katika majukumu
yao ya kazi ambayo huwafanya walipwe mshahara mwisho wa mwezi.
Spika atetea
Spika
Makinda, jana aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake kwamba
wabunge wameshaanza kulipwa posho mpya za Sh200,000 kwa kila kikao
kuanzia Bunge lililopita akisema ni baada ya idhini ya Rais.
Alisema
posho hiyo iko katika waraka wa Serikali kuhusu posho uliotolewa Julai
mwaka juzi akisema wenyeviti wanapata Sh200,000, wajumbe Sh150,000
na wengine Sh100,000.
Kitendo cha kuongezeka kwa posho za wabunge
kinaiweka Serikali katika wakati mgumu kutokana na watu wa kada
mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, wanasiasa, wanaharakati na wasomi
kuzipinga.
Hata hivyo, Makinda alisema ni jambo la kawaida kwa
wananchi kuhoji uhalali wa posho za wabunge wakati mishahara ya wengine
haihojiwi.
“Mtu mwingine akipata mshahara unakuwa wake na familia
yake lakini, kwa mbunge si hivyo kwa kuwa kuna watu wengi ambao wamekuwa
wakihitaji misaada kutoka kwa wabunge na hivyo si jambo la kawaida
zinapoongezwa posho,’’ alisema na kuongeza:
“Wabunge wengine
wanaondoka na mshahara wa Sh45,000 kwa mwezi wengine Sh100,000,
wanachopata ni kidogo sana kwa kwa sababu utendaji wake wa kazi ni
mgumu.”
Makinda aliyekuwa ameongozana na Katibu wa Bunge, Dk
Thomas Kashililah pamoja na maofisa wengine wa Bunge alisema wabunge
wengine wamekuwa wanakopa hadi mafuta ya kuja bungeni na kwamba si
matajiri kama baadhi ya watu wanavyofikiri.
Alisema wapo wabunge ambao hufariki dunia muda mfupi mara baada ya kumaliza kipindi chao cha ubunge kutokana na ugumu wa maisha.
“Anamaliza ubunge Februari anakufa, kiinua mgongo chake ameshakopa leo ikifika mwaka 2015 hana kitu unadhani inakuwaje hapo?”
mwananchi
No comments:
Post a Comment