Wednesday 1 February 2012

sakata la posho:jk amkana pinda na makinda

ASEMA ALIWATAKA WATUMIE BUSARA,  SPIKA ASISITIZA ALIRUHUSU, WANANCHI WACHACHAMAA

Waandishi Wetu
SIKU moja baada ya Waziri Mkuu Mkuu, Mizengo Pinda kusema tayari Rais Jakaya Kikwete amesaini kuidhinisha ongezeko la posho za vikao (sitting allowance) kwa wabunge kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000 kwa siku, Ikulu imetoa taarifa kukanusha madai hayo.Wakati Ikulu ikitoa taarifa hiyo, jana Spika wa Bunge, Anne Makinda aliitisha mkutano wa waandishi wa habari na kusema: “Siyo kwamba tutaanza kutoa, tulishaanza kutoa na Rais (Jakaya Kikwete), ameshatoa kibali chake na mbunge atalipwa katika vikao tu, si kila siku na tena baada ya kukaa kwenye vikao na kusaini.”
Lakini katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu imesema: “Maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuhusu suala hili yako wazi kabisa na hakuna mahali ambako Rais Kikwete amebariki posho hizi.”
“Kwanza, Mheshimiwa Rais Kikwete anakubali haja ya kuangalia upya posho kwa wabunge lakini amewataka wabunge kutumia hekima na busara katika kulitafakari suala hili. Pili, Mheshimiwa Rais Kikwete amewataka wabunge kutumia Kikao cha sasa cha Bunge kulizungumza upya suala hilo.”

Juzi, Pinda aliwaambia wabunge ndani ya kikao cha utangulizi kuwa tayari Rais Kikwete alikuwa ameidhinisha ongezeko la posho za vikao kutoka Sh70,000 hadi Sh200, 000. Baada ya Waziri Mkuu kusema hivyo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema) alisimama na kudai kuwa taarifa alizonazo ni kwamba Rais Kikwete alikuwa hajasaini kuidhinisha posho hizo.

Kauli ya Zitto ilisababisha Mbunge wa Kondoa Kaskazini (CCM), Juma Mkamia kusimama na kuhoji iwapo Zitto ni miongoni mwa wasemaji wa Rais kabla ya Pinda kusimama na kuthibitisha kusainiwa posho hizo akisema, siyo ajabu  kwani hata watumishi wa Serikali wanalipwa kati ya Sh50,000 na Sh200,000.

Hata hivyo, Zitto alitetea msimamo wake kwamba alitarajia baada ya kusainiwa kwa posho hizo na Rais, angepewa masharti mapya ya kazi za ubunge. Wengine walioshambuliwa katika kikao hicho ni Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba na Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Khamis Kigwangwallah kwa kupinga posho hadharani.Wanaodhaiwa kuwashambulia wabunge hawa wanaopinga posho ni Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo, Mbunge wa Sikonge,  Said Nkumba, Nkamia na Mbunge wa Gando (CUF),  Khalifa Suleiman Khalifa.

Jana baada ya kuripotiwa kwa habari hiyo wananchi kutoka kila kona ya nchi walipinga huku wasomi wakitahadharisha kuwa kitendo hicho kinaweza kuligawa taifa.

Wananchi wa kada mbalimbali waliotuma maoni yao kwenye mtandao wa gazeti hili na wasomi ambao walihojiwa walisema kwamba kitendo hicho ni hatari hasa katika kipindi hiki cha mgomo wa madaktari.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Profesa Gaudence Mpangala alisema nyongeza hiyo inaleta utata na kwamba inaonyesha wazi kuwa nchi inanyemelewa na dalili za kuwepo kwa matabaka... “Hii inaonyesha kuwa wapo wanaopendelewa na wengine wanaminywa, jambo hili kiutawala si zuri hata kidogo linaweza kuleta migomo na maandamano nchi nzima.”

Alisema Serikali inatakiwa kuzitazama sekta nyingine huku akitolea mfano mgomo wa madaktari na kuongeza: “Yaani baada ya kutatua hali hii ya mgomo wao ndiyo wanapandisha posho za wabunge. Gharama za maisha ziko juu sana, hilo lazima Serikali ilitambue.”

Mhadhiri mwingine mwandamizi wa chuo hicho, Dk Kitila Mkumbo alisema kauli ya Waziri Mkuu Pinda imetoa majibu sahihi kwamba Serikali ina fedha za kutosha za kuwalipa madaktari.”

“Pinda alikaririwa akisema kuwa Serikali haina fedha za kuwalipa madaktari, lakini hizo za kuwalipa wabunge zimepatikana, sijui hapa inakuwaje?,” alihoji Dk Mkumbo.

Alisema kiwango cha fedha za nyongeza hizo za posho ambacho watalipwa wabunge katika kikao cha Bunge la Juni, zinaweza kuwalipa madaktari waliogoma nchi nzima.

“Mwezi wa sita wabunge hukaa bungeni miezi miwili, sasa ukipiga hesabu za haraka haraka kiwango cha posho watakazolipwa kinatosha kabisa kumaliza kero ya madaktari,” alisema Dk Mkumbo.

Kwa upande wake, Mhadhiri mwingine wa UDSM , Dk Benson Bana alielezea kushangazwa kwake na kitendo cha Serikali kupandisha kiwango cha posho licha ya kuwa suala hilo limepigwa kelele na wananchi... “Posho za vikao (Sitting allowances) siyo kipaumbele chetu, posho hizi hazina uhusiano na utendaji wa mbunge.”

Alisema suala hilo licha ya kutia wasiwasi, linaibua maswali mengi kwa kuwa walimu na madaktari nao wanataka kulipwa vizuri ikiwa ni pamoja na nyongeza ya posho.

“Ningewaelewa kama wangeongeza mishahara ya wabunge lakini siyo posho…, posho ambazo wanalipwa katika saa za kazi, haiingii akilini hata kidogo.” alisema Dk Bana.

Naye Profesa Tolly Mbwete wa Chuo Kikuu Huria (OUT), alisema nyongeza hiyo ya posho inatakiwa kufanyika katika sekta zote ili kupunguza malalamiko ya watu wa kada mbalimbali. “Binafsi naona suala hili linatakiwa kutazamwa katika sekta zote kuliko kujikita kwa wabunge tu.”
Mwanasheria wa kujitegemea, Profesa Abdallah Safari alisema posho hizo hazina mashiko kwa kuwa wanaolipwa wanakuwa katika majukumu yao ya kazi ambayo huwafanya walipwe mshahara mwisho wa mwezi.

Spika atetea
Spika Makinda, jana aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake kwamba wabunge wameshaanza kulipwa posho mpya za Sh200,000 kwa kila kikao kuanzia Bunge lililopita akisema ni baada ya idhini ya Rais.
Alisema posho hiyo iko katika waraka wa Serikali  kuhusu posho uliotolewa Julai mwaka juzi akisema wenyeviti wanapata Sh200,000, wajumbe Sh150,000 na wengine Sh100,000.
Kitendo cha kuongezeka kwa posho za wabunge kinaiweka Serikali katika wakati mgumu kutokana na watu wa kada mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, wanasiasa, wanaharakati na wasomi kuzipinga.
Hata hivyo, Makinda alisema ni jambo la kawaida kwa wananchi kuhoji uhalali wa posho za wabunge wakati mishahara ya wengine haihojiwi.
“Mtu mwingine akipata mshahara unakuwa wake na familia yake lakini, kwa mbunge si hivyo kwa kuwa kuna watu wengi ambao wamekuwa wakihitaji misaada kutoka kwa wabunge na hivyo si jambo la kawaida zinapoongezwa posho,’’ alisema na kuongeza:
“Wabunge wengine wanaondoka na mshahara wa Sh45,000 kwa mwezi wengine Sh100,000, wanachopata ni kidogo sana kwa kwa sababu utendaji wake wa kazi ni mgumu.”
Makinda aliyekuwa ameongozana na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah pamoja na maofisa wengine wa Bunge alisema wabunge wengine wamekuwa wanakopa hadi mafuta ya kuja bungeni na kwamba si matajiri kama baadhi ya watu wanavyofikiri.
Alisema wapo wabunge ambao hufariki dunia muda mfupi mara baada ya kumaliza kipindi chao cha ubunge kutokana na ugumu wa maisha.
“Anamaliza ubunge Februari anakufa, kiinua mgongo chake  ameshakopa leo ikifika mwaka 2015 hana kitu unadhani inakuwaje hapo?”

mwananchi

No comments:

Post a Comment