Friday 10 February 2012

MGOMO WA MADAKTARI: Vigogo nje

 Send to a friend
Thursday, 09 February 2012 21:01
0diggsdigg
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni
KATIBU MKUU, MGANGA MKUU WIZARA YA AFYA WANG’OLEWA, VYOMBO VYA DOLA VYAWACHUNGUZA KWA UFISADI, MADAKTARI WAREJEA KAZINI
Waandishi Wetu
WAKATI madaktari nchini wakiafiki kusitisha mgomo wao na kukubali kurejea kazini leo, sakata hilo limeacha jeraha kubwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa,  kwa kusimamishwa kazi.

Hatua hiyo ilitangazwa jana na Waziri Mkuu , Mizengo  Pinda alipokutana na madaktari hao  katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), huku akiweka bayana kuwa hatima ya Waziri wa Wizara hiyo,  Dk Haji Mponda na Naibu wake,  Dk Lucy Nkya, inabaki mikono mwa Rais Jakaya Kikwete.
 Pinda, alisema watendaji hao wa ngazi ya juu ya Wizara ya Afya, wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa vyombo vya dola, dhidi ya tuhuma mbalimbali zinazohusishwa na utendaji wao.

Katika mkutano huo, Waziri Mkuu aliweka wazi sababu kuu tatu za Serikali  kuwasimamisha kazi  vigogo hao wa wizara.

Pinda aliyelazimika kuacha kikao cha Bunge mjini Dodoma na kurejea Dar es Salaam juzi kushughulikia mgomo huo, alisema sababu ya kwanza ya kuwasimamisha watendaji hao, ni  tuhuma za kuingiza nchini robo tatu ya vifaa bandia vya vipimo vya Ukimwi kutoka Korea Kusini.


Alitaja sababu zingine  kuwa  ni tuhuma za  kuanzisha kampuni ya kusambaza nguo kwa madaktari na kuiingiza kinyemela kampuni ya kufanya usafi ndani ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbil.Pinda alisema tuhuma hizo ni nzito zinazoidhalilisha Serikali na kamwe haitakuwa busara kuzifumbia macho huku Serikali ikiendelea kudhalilika.


“Nimeamua kuwasimamisha kazi  Katibu Mkuu na Mganga Mkuu wa Serikali, ili kuweza kupisha uchunguzi  maana hizi tuhuma zinafedhehesha taifa."
Aliongeza; “Kwa upande wa Waziri   na Naibu Waziri  wa Afya, nimeshapeleka ushauri kwa Rais kutokana na yeye  kuwa mwenye dhamana, siwezi kuliongelea hili hapa ila yule aliyewateua, atafanya maamuzi, najua kitakachofuata mnakijua,” alisema Pinda huku madaktari wakilipuka kwa shangwe na kuimba nyimbo ya mshikamano.

Alisema malalamiko ya madaktari  ni makubwa na kwamba, yana msingi wa kusikilizwa na kusihi  kamati iliyoundwa kuorodhesha kila kitu ili Serikali iweze kuyafanyia kazi.
Alisema baada ya madaktari mabingwa kumweleza hali ilivyo katika hospitali hiyo ya  Muhimbili, ndipo  aliweza kujua kwa undani  matatizo yao makubwa.

Mganga Mkuu wa Serikali,Dk Deo Mtasiwa,
Alisema Watanzania wana imani kubwa kwa madaktari hao kurejea kazini na Serikali kuanza kuyafanyia kazi madai yao zikiwemo posho.

 Utekelezaji
Pinda alisema  baada Serikali kusikia kilio cha madaktari hao imeamua kuongeza posho zao  kufikia Sh 25,000  hadi  35,000.

Alisema suala la maboresho ya mishahara litashughulikiwa katika  bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2012/13.
“Serikali imeamua kuongeza posho kutoka Sh 10,000 za awali hadi 25,000 na 35,000  kiwango hiki  kitaendana na madaraja ya madaktari kama mtu alikuwa akilipwa  Sh 3,000, atalipwa Sh 10,000, aliyekuwa analipwa Sh 5,000 atalipwa Sh 15,000 huku waliokuwa wakilipwa kuanzia Sh 20,000 itaongezeka hadi 35,000,”alifafanua  Pinda.

Madaktari wasitisha mgomo
Akitangaza kumalizika kwa mgomo huo,  Mwenyekiti wa Kamati ya Madaktari, Dk Stephen Ulimboka, alisema wamesitisha mgomo kwa muda kwa nchi nzima ili kutoa fursa ya majadiliano  kati yao na Serikali.


“Tunasitisha mgomo huu na kuanzia sasa madaktari wote nchini nawasihi kurejea ofisini kesho (leo) na kuendelea na kazi. Tunafikia hatua hii kwa maslahi ya Watanzania, lakini, pia tutaendelea kufanyia tathimini utekelezwaji wa madai yetu,”alisema Dk Ulimboka.

Mwenyekiti huyo,  alisema madaktari hao wanatarajia kukutana Machi 3 mwaka huu kufanya tathmini juu ya utekelezwaji wa madai yao na kwamba,  kama Serikali itashindwa kutekeleza wao wataamua cha kufanya.

Mwenyekiti huyo alitumia fursa hiyo kuitaka Serikali iwaachie bila masharti wanaharakati waliokamatwa jana, kwa kile alichosema, hatua hiyo itavuruga utatuzi wa mgogoro huo uliodumua kwa muda wa siku 17.
 Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Primus Saidia, alimtaka  Waziri Mkuu Pinda kusoma Biblia Kitabu cha Yoshua Bin Sira Sura ya 38 mstari wa 1-15 ambayo, inamtafsiri daktari kuwa ni mkuu kati ya wakuu wote.

“Biblia inasema hivyo, lakini hata kiapo cha madaktari mnachotaka tukitii mnapaswa kukumbuka kuwa kina sehemu mbili, sehemu ya kuapa kwa daktari, lakini pia ipo sehemu ambayo daktari anapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa,"alisema.

Saidia alisema kitabu hicho ambacho kipo katika Agano la Kale, kinaelezea vizuri pia namna daktari anavyotakiwa kuenziwa na  kuhemishiwa.

“Kiapo kinamtaka daktari kuhakikisha anafanya kazi ya kuokoa maisha ya watu, lakini pia kwa upande wa pili, kinataka Serikali na watu wake kuhakikisha daktari anaishi kwa raha maishani mwake,”alisema.
Aliongeza, “Daktari hawezi kuwa na raha kama hatafika kazini, hawezi kuwa na raha kama atalipwa mshahara  mdogo, kama atacheleweshewa posho kwa siku 40  na kama atashindwa kumtibu mgonjwa kwa kukosa vifaa na dawa,”alisema.

Wafurahia Nyoni kung’olewa
 Muda mfupi baada ya Pinda kuwasimamisha vigogo hao wawili wa Serikali, wafanyakazi katika Hosptali ya MNH walishangilia kwa nguvu na kuipongeza Serikali kwa hatua hiyo.

Wafanyakazi ambao  wengi wao ni wauguzi, walipiga vigelele huku baadhi yao wakidai aliwambia hawezi kukukutana wala kuzungumza nao sababu wao ni wachafu.  “Alisema sisi ni wachafu tena ni afadhali hakuja,  tungempopoa mawe,”alisikika mmoja wa wauguzi akipaza sauti.  Mwenyekiti wa Chama cha Wauguzi Taifa (Tanna) Tawi la Muhimbili, Paul Magesa alielezea hatua ya kusimamishwa katibu huyo kama hatua muhimu katika kusafisha wizara hiyo.

 Alimtuhumu wazi kuwa, amekuwa sehemu ya kukwamisha  pendekezo la uundwaji wa Kurugenzi ya Wauguzi wizarani hapo.  “Sisi tumekuwa na madai yetu kwa muda mrefu, na kubwa ni  la kutaka iundwe  Kurugenzi ya Wauguzi, tulishajiandikisha tukaambiwa kuna taratibu za kufuatwa, lakini ghafla tukaona Kurugenzi nyingine zinazundwa,”alisema Magesa na kuongeza “ni bora walivyotimuliwa.”

 Bungeni Dodoma
Mjini Dodoma, Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii iliyokuwa ikishughulikia mgomo huo, imekabidhi ripoti yake kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda na inadaiwa kuelezwa kuwa baadhi ya watendaji hao walishinikiza kampuni za kufanya usafi, MNH na kupitishwa kwa sare ya madereva wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI).

“Wale madaktari tumekaa nao kila mmoja wetu (wabunge), alikuwa akibubujikwa machozi ukisikiliza shida zao... huyu (jina tunalo) anadaiwa licha ya Bodi ya Zabuni kupitisha sare kwa madereva wa MOI, alikwenda akashinikiza wapitishe kitambaa walichokataa,” alidokeza mmoja wajumbe wa kamati hiyo.

Kamati hiyo imependekeza kuchunguzwa watendaji hao iwapo wana hisa za moja kwa moja kwenye kampuni hizo, au wamewekwa kwa hisa zao kwa watu wengine.

Baada ya kamati hiyo kuwasilisha taarifa yake kwa Kamati ya Bunge ya Uongozi juzi usiku, iliamua kumwagiza Spika Makinda, kuwasiliana na Rais Jakaya Kikwete ili kuwaondoa au kuwahamisha Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Mponda, Naibu wake, Dk Nkya, Katibu Mkuu wa Wizara, Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Mtasiwa.


Pia, inadaiwa wakuu wa Idara Wizara ya Afya, wanachukua mikopo bila kurejesha.

Akitoa taarifa kwa wabunge jana asubuhi, Makinda, alisema walipokea taarifa ya Kauli ya Serikali na kwenda kufuatilia undani wa mgomo huo na kwamba, imefanya kazi kubwa kwa muda mfupi.

“Kamati ya Uongozi pamoja na Kamati ya Huduma za Jamii, tumefanya shughuli ya kujadili taarifa hiyo tukiwa tumepata maelezo ya wenzetu waliofika kule, wameongea na madaktari, wamekagua Hospitali ya Muhimbili, wameongea na watu mbalimbali na wakapata undani wa hali halisi. Kwa hiyo ushauri wao tumeujadili jana usiku mpaka tumemaliza kikao kama saa 6:00 usiku,” alisema.

Makinda alisema baada ya saa 6:00 usiku kwa sababu mambo yenyewe yalikuwa ya haraka, aliagizwa kuwasiliana na viongozi wakuu, Rais na Waziri Mkuu.

“Kwa hiyo tumeongea na Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu wote wanakubaliana na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati na kwamba mpaka sasa hivi hayupo kwa sababu Kamati ilichokuwa inaomba ni kwamba kwanza tuombe kwa dhati kabisa na Bunge hili madaktari warudi kwenye stations (vituo)  zao,” alisema.

Spika Makinda alisema mawasiliano mabaya yaliyokuwapo kati ya madaktari na wizara yangechukuliwa hatua jana na madai yao mengine ambayo ni ya dharura na haraka, Serikali ilikuwa ikiyashughulikia.

Kwa zaidi ya wiki mbili sasa madaktari nchini wamekuwa katika mgomo mkubwa wakishinikiza kutekelezewa madai yao ya msingi.

mwananchi

No comments:

Post a Comment