Wednesday 2 May 2012

JK AYEYUSHA WAZO LA KUPANDA MISHAHARA YA WAFANYAKAZI


 Send to a friend

0digg
Rais Jakaya Kikwete
Waandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete ameshindwa kutangaza hadharani kima cha chini cha mshahara cha Sh315,000 kwa mwezi kilichoombwa kwa mara nyingine na  Shirikisho la Chama cha Wafanyakazi Tanzania (Tucta).Badala yake, Kikwete akiwahutubia wafanyakazi  jijini Tanga jana alisema  Serikali itaendelea kuboresha maisha ya wafanyakazi kwa kuongeza mishahara kwa kadri itakavyokuwa na uwezo.
Hatua hiyo ilikuja baada ya Katibu Mkuu wa Tucta, Nicolaus Mgaya kumwomba Rais Kikwete atangaze kima cha chini cha mshahara kuwa Sh 315,000 kwa mwezi.
“ Mheshimiwa Rais pamoja na kwamba kima hiki cha chini tulikiomba tangu mwaka 2007  bila mafanikio, tunaomba leo utangaze kiasi hicho kuwa kima cha chini, ingawa kwa sasa hakitakuwa kinatosha,” alisema Mgaya.
Hata hivyo Kikwete alisema itaendelea kuimarisha na kusimamia vyanzo vya mapato ya Serikali ili kuboresha mishahara ya wafanyakazi.
Akizungumza kwa simu kuhusu hilo, Mgaya alisema wanasubiri bajeti ya mwaka 2012/13 kuona wataongezwa kiasi gani cha mshahara.
“ Tuna imani kwamba atatuongeza ingawa hajatamka kuongeza kiasi kile alichoomba sasa hatujui kama atatupa kiasi gani,” alisema Mgaya.
Alipongeza hotuba ya Kikwete kwa kuonyesha mwelekeo unaoonyesha kuwa ana dhamira ya dhati katika kukomesha ufisadi unaofanywa na baadhi ya watendaji wa Serikali.
Wakati huohuo  Mratibu wa sherehe za Mei Mosi mkoani Mbeya, Suma Kabiga amesema Serikali imeshindwa kudhibiti mfumko wa bei hali inayosababisha ugumu wa maisha kwa wafanyakazi.
Kabiga akisoma risala ya wafanyakazi mkoani humo alisema mfumko wa bei unawaathiri wafanyakazi kwa sababu mishahara ni ile ile ya zamani isiyopanda.
Habari kutoka Dodoma zilisema Tucta imesema mishahara wanayolipwa wafanyakazi ya Sh 150,000 kwa Serikali
na 65,000 kwa sekta binafsi ni kinyume na haki za binadamu kwa kuwa haitoshi hata kuishi kwa siku 30 na kutaka Serikali kuangalia upya suala hilo ili kuleta utulivu na amani sehemu za kazi.

Hayo yalibainishwa jana mjini Dodoma na Katibu wa Tucta mkoani hapo, Everest Mwalongo wakati wa maadhimisho ya sherehe ya Mei Mosi kwa mkoa huo  yaliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri mjini hapa.

Mwalongo alisema mshahara wanaolipwa watumishi wa Serikali kwa kima cha chini wa Sh150,000 na ule wa sekta binafsi wa Sh 65,000 hautoshelezi kwa maisha ya sasa hatua inayofanya watumishi kuishi kwa kukopa jambo linaloathiri utendaji wa kazi.

Wakati huohuo Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Mashambani na Kilimo (TPAWU) Mkoa wa Dar es Salaam, John Adrian ameiomba Serikali kufanya  maboresho ya maslahi ya wafanyakazi ili waweze kumudu maisha.
Adrian aliitaka Serikali kufanyia kazi madai yao ambayo ni pamoja na kuongeza kiwango cha chini cha mshahara hadi Sh350,000 badala ya Sh150,000 na 65,000 kwa sekta binafsi.
Alisema kuwa mshahara wa sasa ni mdogo ambao hauendani na mfumuko wa bei uliopo.
Risala hiyo ilisomwa mbele ya Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mwantumu Mahiza.

Akizungumza, kwenye hafla hiyo, Mahiza aliwataka wafanyakazi hao kutumia nguvu na bidii katika uwajibikaji kama ambavyo wanatumia nguvu hiyo katika kudai haki zao.

“Kama kweli tunataka kupambana na ukali wa maisha pamoja na mfumko wa bei hatuna budi kila mmoja kwa nafasi yake kuwajibika badala ya kuendelea kulalamika kama ambavyo wengi wamezoea,”alisema Mahiza

Aliongeza kuwa Serikali iko katika mpango wa kutekeleza hatua kwa hatua mapendekezo ya wafanyakazi kwa lengo la kuboresha utendaji wake na kuleta tija katika maendeleo ya nchi.

No comments:

Post a Comment