ATAKA WIZARA YAKE IONDOLEWE KAMATI YA LOWASSA
Habel Chidawali, Dodoma
WAZIRI
wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amependekeza kuwa
wizara yake iondolewe chini ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya
Nje, Ulinzi na Usalama inayoongozwa na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward
Lowassa na iundiwe kamati yake.
Sitta
alitoa kauli hiyo bungeni, mjini Dodoma juzi usiku wakati akihitimisha
hoja za Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa
fedha 2012/13.
Mkongwe
huyo wa siasa alieleza kuwa moja ya sababu za kupendekeza hivyo ni
Kamati hiyo ya Mambo ya Nje kukabiliwa na majukumu mengi hata wakati
mwingine kushindwa kuitendea haki wizara yake.
Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama inayoongozwa na
Lowassa, ambaye mara kadhaa ametajwa kuwa ni mwiba kwa Wizara za Mambo
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na ile ya Ushirikiano
wa Afrika Mashariki inayoongozwa na Sitta.
Iliripotiwa
kwenye vyombo vya habari hivi karibuni kuwa Lowassa akiwa kwenye vikao
vya kamati yake alitaka kukwamisha bajeti za wizara hizo mbili akidai
maelezo ya ufafanuzi kuhusu matumizi ya mwaka uliopita pamoja na masuala
kadhaa ya kiutawala.
Kufuatia
hali hiyo, kamati ililazimika kumwita Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe mbele ya kamati ili kutoa
maelezo ambapo alifanya hivyo na kukubaliana na kamati hiyo.
Kauli
ya Sitta inatafsiriwa kuwa ni dalili za kumkimbia Lowassa kutokana na
misuguano ya kisiasa ya muda mrefu ndani ya chama chao CCM na Serikali,
ambayo imekuwa ikielekezwa katika kuwania nafasi ya juu ya uongozi ndani
ya Taifa.
Lowassa
alijiuzulu uwaziri Mkuu, Mwaka 2008, kutokana na kuibuka kwa kashfa ya
Kampuni ya Kufua Umeme ya Richmond baada ya Bunge lililokuwa chini ya
uongozi wa Spika Sitta kuunda kamati teule kuchunguza kashfa hiyo.
Ingawa
Sitta hakutaja moja kwa moja nini hasa atakachofanya, lakini inaonyesha
kuwa hakubaliani na Kamati ya Lowassa kuisimamia wizara yake, huku
akiwapoza wabunge kuwa anafanya hivyo ili kuipunguzia mzigo kamati hiyo.
Akijenga
hoja ya kuundiwa kamati yake, Sitta alitoa sababu kuwa Kamati ya Mambo
ya Nje inashughulikia masuala mengi ya msingi hivyo inashindwa kuwa
karibu na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
“Napendekeza
kuwa iundwe Kamati ya Kudumu ya Bunge itakayoshughulika na masuala ya
Afrika Mashariki tu, kwani hii iliyopo sasa imekuwa na mambo mengi
sana,’’ alisema Sitta na kuongeza:
“Unaweza
kuona kuwa hawa wanaangalia Mambo ya Nje, wanaangalia Ulinzi na
Usalama, sasa kuwapa na Afrika Mashariki ni mzigo mzito sana.’’
Hata
hivyo, haijulikani kama kamati aliyopendekeza Sitta itaundwa kwa Kanuni
ipi kwa kuwa kwa mujibu wa Kanuni za Bunge hakuna kamati hiyo na karibu
kamati zote zimekuwa zikihudumia zaidi ya wizara moja.
Maelezo ya Lowassa
Lowassa
alipoulizwa na gazeti hili jana juu ya pendekezo la Sitta, alisema
kuwa, haoni kama kuna tatizo endapo kamati hiyo ikiundwa kwa ajili ya
kuisaidia wizara hiyo.
“Kimsingi
mimi sikuwepo, lakini kama alisema yawezekana alilenga kutoa nafasi kwa
Wizara hiyo kupata chombo cha kuisemea kwa karibu.”...
No comments:
Post a Comment