Sunday 5 August 2012

SITTA ATAFUTA KUMKIMBIA LOWASSA




ATAKA WIZARA YAKE IONDOLEWE KAMATI YA LOWASSA
Habel Chidawali, Dodoma
WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amependekeza kuwa wizara yake iondolewe chini ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama inayoongozwa na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa na iundiwe kamati yake.

Sitta alitoa kauli hiyo bungeni, mjini Dodoma juzi usiku wakati akihitimisha hoja za Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2012/13.

Mkongwe huyo wa siasa alieleza kuwa moja ya sababu za kupendekeza hivyo ni Kamati hiyo ya Mambo ya Nje kukabiliwa na majukumu mengi hata wakati mwingine kushindwa kuitendea haki wizara yake.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama inayoongozwa na Lowassa, ambaye mara kadhaa ametajwa kuwa ni mwiba kwa Wizara za Mambo ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na ile ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki inayoongozwa na Sitta.

Iliripotiwa kwenye vyombo vya habari hivi karibuni kuwa Lowassa akiwa kwenye vikao vya kamati yake alitaka kukwamisha bajeti za wizara hizo mbili akidai maelezo ya ufafanuzi kuhusu matumizi ya mwaka uliopita pamoja na masuala kadhaa ya kiutawala.

Kufuatia hali hiyo, kamati ililazimika kumwita Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe mbele ya kamati ili kutoa maelezo ambapo alifanya hivyo na kukubaliana na kamati hiyo.

Kauli ya Sitta inatafsiriwa kuwa ni dalili za kumkimbia Lowassa kutokana na misuguano ya kisiasa ya muda mrefu ndani ya chama chao CCM na Serikali, ambayo imekuwa ikielekezwa katika kuwania nafasi ya juu ya uongozi ndani ya Taifa.

Lowassa alijiuzulu uwaziri Mkuu, Mwaka 2008, kutokana na kuibuka kwa kashfa ya Kampuni ya Kufua Umeme ya Richmond baada ya Bunge lililokuwa chini ya uongozi wa Spika Sitta kuunda kamati teule kuchunguza kashfa hiyo.

Ingawa Sitta hakutaja moja kwa moja nini hasa atakachofanya, lakini inaonyesha kuwa hakubaliani na Kamati ya Lowassa kuisimamia wizara yake, huku akiwapoza wabunge kuwa anafanya hivyo ili kuipunguzia mzigo kamati hiyo.

Akijenga hoja ya kuundiwa kamati yake, Sitta alitoa sababu kuwa Kamati ya Mambo ya Nje inashughulikia masuala mengi ya msingi hivyo inashindwa kuwa karibu na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

“Napendekeza kuwa iundwe Kamati ya Kudumu ya Bunge itakayoshughulika na masuala ya Afrika Mashariki tu, kwani hii iliyopo sasa imekuwa na mambo mengi sana,’’ alisema Sitta na kuongeza:

“Unaweza kuona kuwa hawa wanaangalia Mambo ya Nje, wanaangalia Ulinzi na Usalama, sasa kuwapa na Afrika Mashariki ni mzigo mzito sana.’’

Hata hivyo, haijulikani kama kamati aliyopendekeza Sitta itaundwa kwa Kanuni ipi kwa kuwa kwa mujibu wa Kanuni za Bunge hakuna kamati hiyo na karibu kamati zote zimekuwa zikihudumia zaidi ya wizara moja.

Maelezo ya Lowassa
Lowassa alipoulizwa na gazeti hili jana juu ya pendekezo la Sitta, alisema kuwa, haoni kama kuna tatizo endapo kamati hiyo ikiundwa kwa ajili ya kuisaidia wizara hiyo.

“Kimsingi mimi sikuwepo, lakini kama alisema yawezekana alilenga kutoa nafasi kwa Wizara hiyo kupata chombo cha kuisemea kwa karibu.”... 
 

No comments:

Post a Comment