Waziri
wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Khamis Suedi Kagasheki amekanusha
uvumi unaosambazwa na Shirika moja kupitia mtandao wake wa AVAAZ.org
kuwa watanzania wa Jamii ya Kimasai wapatao 48,000 watahamishwa kutoka
eneo lao (la Serengeti) kupisha Wafalme kutoka Mashariki ya Kati ili
walitumie eneo hilo kwa uwindaji wa Simba na Chui.
Taarifa
hiyo iliyosambazwa na mtandao huo imewataka watu kutoka duniani kote
kujiorodhesha ili wafikie angalao 150,000 ili kumshinikiza Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuacha kusaini mkataba ambao utafanya
uhamisho huo utekelezwe.
Waziri Kagasheki amesisitiza kuwa uvumi huo siyo kweli na hauna msingi wowote kutokana na sababu zifuatazo:
Kwanza,
hatua kama hii haiwezi kuchukuliwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
katika Hifadhi ya Serengeti maana hakuna watu wanoishi ndani ya hifadhi
hiyo. Pia kitendo hicho hakijapangwa kufanyika katika Wilaya ya
Serengeti iliyoko mkoani Mara.
Pili,
hata kama taarifa hiyo ilimaanisha Wilaya ya Serengeti mkoani Mara,
bado siyo kweli maana wilaya hiyo haina idadi ya Wamasai wanaofikia
jumla ya 48,000.
Tatu,
ndani ya ya Hifadhi ya Serengeti hakuna eneo lolote ambalo limetengwa
kwa ajili ya wafalme wa Mashariki ya Kati ili waweze kulitumia kwa
uwindaji wa Simba na Chui.
Nne,
habari hizo siyo kweli maana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
hahusiki kabisa na ugawaji wa vitalu vya uwindaji popote pale nchini.
Hii ni kazi ya Wizara ya Maliasili na Utalii, na Wizara haijafanya hivyo
katika eneo tajwa.
Pamoja
na ufafanuzi huo Waziri Kagasheki amewaasa watu waliojiorodhesha, na
wanaotarajia kujiorodhesha, kuwa wamepotoshwa, hivyo wanatakiwa
wasisaini kubariki kitu mbacho hawakijui wala hakipo.
[MWISHO]
George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
Tarehe 15 Agosti 2012
Simu: +255 784 468047.
No comments:
Post a Comment