Monday 4 February 2013

Mtangazaji atiwa mbaroni kwa dawa za kulevya




MAMLAKA ya Mapato Kenya(KRA),inamshikilia mwandishi wa habari wa Tanzania kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin kiasi cha kilo 5.436 zenye thamani ya karibu Sh234 milioni.
Mtanzania huyo ambaye aliwahi kuwa mtangazaji katika kituo kimoja cha redio nchini, alikamatwa akiwa anataka kusafirisha dawa hizo kwenda China.
“Mamlaka ya Mapato Kenya inataka kutaarifu maendeleo ya sakata la kukamatwa kwa kilo 5.436 za heroin zilizokamatwa Januari 23 mwaka 2013 saa 4:40 usiku.”
“Imethibitika kuwa kilichokamatwa ni dawa aina ya heroin yenye thamani ya Sh13 milioni za Kenya…kwamba mtuhumiwa… (Jina tunalo kwa kuwa hajafikishwa mahakamani) hakuwa mwanafunzi lakini ni mtangazaji wa redio nchini Tanzania.”
Ametambulika kuwa mtangazaji wa kituo kimoja cha redio kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye thamani ya Sh234 milioni.
Mtuhumiwa huyo  alikamatwa  katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kenyatta akiwa katika jaribio la kuelekea nchi za Ulaya na kwamba kukamatwa kwake kulifanikiwa kutokana na mtego ulioandaliwa na maofisa wa usalama uwanjani hapo.
Taarifa zinasema kuwa, mtuhumiwa huyo alijitambulisha kama mwanafunzi anayesoma Sweden, lakini hata hivyo ilikuja kubainika kuwa alikuwa na kibali cha ukazi alichokipata Novemba 28 na kilitazamiwa kuisha muda wake Novemba 28,2014.
Naibu Kamishna wa KRA, Kenned Onyonyi alisema kuwa maofisa wa usalama wanaendelea na uchunguzi zaidi na taarifa zaidi zitatolewa baadaye.
Habari zinasema kuwa, mtuhumiwa huyo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na raia mmoja wa Sweden, ambaye alimtambulisha kwa maofisa usalama kwamba amekuwa  akisafiri mara kwa mara katika nchi za Ghana, Kenya na Mauritius.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa, mtuhumiwa huyo  amewahi kufanya kazi na Clouds fm akiwa kama mtangazaji mwanafunzi katika kipindi cha Leo tena na baadaye aliachana na kampuni hiyo na kujiunga na gazeti hili akiandika habari za burudani. Aliachana na gazeti hilo na kuendelea na maisha yake ya kawaida.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Godfrey Nzowa alisema kuwa  hawajapata taarifa za kukamatwa kwa Mtanzania huyo, bali wamezisoma tu kwenye baadhi ya vyombo vya habari.
“Kuna utaratibu ambao inabidi watujulishe kwani kuna tume ya kuratibu dawa za kulevya  hivyo tunasubiri atuambie kuhusu tukio hilo,”alisema Nzowa.
HABARI ZAIDI BOFYA HAPA

MWANANCHI

No comments:

Post a Comment