Saturday, 10 September 2011

BABU AIBUKA TENA



 
Na Mwandishi Wetu
Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Masapile ‘Babu’  (pichani) ameibuka tena hivi karibuni na kuweka wazi yanayoujaza moyo wake.

Akiongea na vyombo vya habari hivi karibuni kutokea kijijini Samunge, Loliondo, Babu alisema kuwa, ameongea na Mungu na ameambiwa kwamba, wagonjwa wanaokunywa tiba ya kikombe chake, hawatakiwi kunywa dawa nyingine yoyote ya ugonjwa uliowafanya wapate dawa yake.
Hapa alimaanisha kwamba, endapo mgonjwa anaugua TB, akipata kikombe chake hatatakiwa kunywa dawa nyingine kwa lengo la kuponya ugonjwa huo.
Kwa mantiki hii, Babu anakwenda pembeni ya matamshi yake ya kwanza ambapo aliwahi kuripotiwa akisema, wagonjwa wasiache kunywa dawa za hospitali hata kama watapata kikombe kwake.

Aidha, Babu Masapile alikwenda mbele zaidi pale aliposema kwamba, baadhi ya madaktari nchini wanamuonea wivu ndiyo maana wanasema dawa yake haiponyi.
Babu akahoji: “Mbona Wakenywa wanapona wengi sana na wanaongea vizuri kuhusu mimi?”
 
Akaendelea: “Tatizo Watanzania wengi hawana imani, na mtu akikosa imani dawa yangu haifanyi kazi.”
Aidha, Babu alisema kwamba, kwa sasa anapokea wagonjwa kiasi cha 40 mpaka 50 kwa siku moja, akasema tiba yake bado inatibu.

Hii ni mara ya tatu Babu kudai ameongea na Mungu. Mara ya kwanza ni pale alipoanza kutoa tiba mwaka 2007, akaja kuongea na Mungu mwaka 2010 ambapo alisema amepewa maelekezo mapya.

chanzo:GPL

1 comment:

  1. huyu mzee bonge la kauzu kwanini asihamie kenya basi?

    ReplyDelete