Tuesday, 11 October 2011

HIKI NDICHO KILICHOIMALIZA STARS MOROCCO

 KOCHA WA TAIFA JAN POULSEN
Andrew Kingamkono, Marrakech
KIPIGO cha Taifa Stars cha mabao 3-1 kutoka kwa Morocco juzi usiku kulichangiwa kwa kiasi kikubwa na maamuzi ambayo si sahihi ya kocha Jan Poulsen.Taifa Stars ilimaliza mchezo wake kwa kufunga mabao hayo, mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Menara mjini Marrakechna. Stars ilipoteza kabisa matumaini ya kufuzu.Ilipoteza mechi hiyo ya pili kwa Morocco na ilifungwa na Afrika ya Kati 2-1. Mapema ilitoka sare ya 1-1 na suluhu na Algeria.

Ilishinda mchezo mmoja na Afrika ya Kati mjini Dar es Salaam. Ilimaliza mechi zake ikiwa na pointi tano. Morocco ndiyo iliyofuzu kutoka Kundi D.Poulsen aliyejua wazi kuwa katika mchezo huo alikuwa na majukumu mawili makubwa kwanza kulinda na pili kuhakikisha anashambulia ili kuiongoza Stars kupata matokeo mazuri na hatimaye kufuzu.

Mdernmark huyo atajilaumu mwenyewe kwa uamuzi wake kubadilisha kikosi saa chake kabla ya mchezo kitu ambacho kwa namna moja au nyingine kiliifanya Taifa Stars kutojua nini cha kufanya uwanjani.

Kosa kubwa alililofanya kocha huyo kumuondoa kwenye kikosi kinachoonza Nassor Masoud aliyekuwa acheze namba saba kwa lengo la kusaidiana Erasto Nyoni.

Katika mazoezi ya mwisho upande wa kulia aliamua kumtumia Chollo na Nyoni lengo ikiwa ni kuhakikisha Morocco hawapiti kupitia pembeni kama alivyofanikiwa kwa upande wa kushoto ambako alicheza Danny Mrwanda na Idrissa Rajabu.

Jumapili asubuhi kwenye kutaja kikosi cha mwisho alimweka nje Chollo na kuamua kumtumia Mohamed Abdallah Machupa winga ya kulia ndipo tatizo lilipoanza.

Machupa ni mchezaji mzuri, lakini kwa umri wake alishindwa kwenda na kasi ya mchezo ya Wamorocco hivyo hakashindwa kushuka kumsaidia Nyoni katika kulinda.Kutokana na upungufu huo, Nyoni alichoka haraka katika kipindi hicho na kocha Poulsen aligundua hilo, lakini akafanya kosa jingine kubwa la kiimaamuzi.

Aliyeshindwa kutimiza jukumu lake ni Machuppa si Nyoni hivyo alipaswa kumpumzisha Machuppa ili aingie Chollo asaidie kwenye ulinzi na Erasto kulinda matokeo ya sare, lakini bado akamtoa Nyoni.Kiuchezaji mabeki si watu wa kutolewa katikati ya mchezo kwani ni lazima atauvuruga ukuta na mipango yote ya ulinzi, ndicho kilichoteka kwani Morocco wakahamia kwa Cholo na kupitisha mashambulizi na mabao yote mawili yalitokea upande huo.

Mrwanda aligundua hilo hivyo alijaribu kuua winga yake naye kuwa beki hadi hapo mfumo uliharibika na Stars walikuwa hawajui wanacheza kitu gani zaidi ya kukimbiza 'vivuli' vyao uwanjani.

Wakati timu ikiwa imeshachanganyikiwa, Poulsen alifanya kosa jingine; ni kweli Samata hakuwa kwenye kiwango chake lakini kwa kasi ya mchezo alikuwa na msaada zaidi kuliko alivyoingia John Boko ambaye mwenyewe ni mzito na hana maamuzi ya haraka.

Jambo lingine ambalo limechangia Taifa Stars kufungwa ni kukosekana na beki wa mwisho namba tano ambaye ni mtulivu mwenye uwezo wa kuwatuma na kupanga wenzake.

Juma Nyoso na Aggrey Morris wao ni watu wa kucheza namba nne ndiyo aina yao ya uchezaji na hata ukiangalia jinsi wanavyokaba wanakuwa wote hivyo akipotea moja, mwingine anashindwa kujipanga.

Kwa aina yao ya uchezaji Stars kila siku itakuwa ikifungwa mabao kupitia katikati kutokana na wao kushindwa kujipanga.Ukiangalia bao la kwanza la Marouane Chamackh ni wazi alikuwa peke yake na kuruka juu wakati Aggrey na Nyosi wameshapotea.

*Ndoto yafutika
Ndoto ya Tanzania ilizima kabisa mbele ya wenyeji Morocco waliokuwa wameahidiwa dola 100,000 kwa kila mchezaji endapo wangeshinda wakishangiliwa kwa nguvu na mashabiki wao waliopamba uwanja kwa rangi nyekundu na nyeupe.

Pamoja na Morocco kufanikiwa kupata bao la kuongoza dakika 20 kupitia mshambuliaji wake, Chamackh aliyeunganisha kwa kichwa krosi ya Oussama Assaidi aliyekuwa mwimba kwa ngome ya Stars.

Kiungo Abdil Kassim alisawazisha bao hilo dakika 38 kwa shuti kali la umbali wa mita 25 na kuufanya uwanja wote kuwa kimya kabisa huku timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare 1-1.

Mwanzoni mwa kipindi cha pili kocha Jan Poulsen aliamua kumtoa beki Erasto Nyoni na kumwingiza Nassor Masoud 'Cholo' ili kumkabili Assaidi aliyeonekana kuwa hatari kutokea winga ya kushoto.

Wakati Stars ikionekana kujipanga na kutulia mwamuzi alionekana kufanya maamuzi mengi ya utata na kuwapendelea wenyeji kwa kiasi furahani.

Mwamuzi huyo aliamuru kupige adhabu nje ya eneo la hatari la Taifa Stars dakika ya 67 iliyopigwa na kiungo wa Queens Park Rangers, Adel Taarabt aliyefunga bao la pili kwa wenyeji kwa shuti lake kwenda moja kwa moja wavuni baada ya beki ya Stars kushindwa kuruka ili kuokoa mpira huo.

Kuingia kwa bao hilo kuliamsha shangwe kwa mashabiki wa Morocco na kuirudisha timu yao kwenye mchezo na kuanza kucheza pasi na kutawala.

Uwezo mkubwa ulioonyesha na kipa Juma Kaseja ulinusuru Stars kupata kipigo kikubwa, lakini dakika ya 90 mchezaji Mbark Boussoufa alitumia vizuri udhaifu wa beki ya Stars kwa kuunganisha krosi kwa shuti la chini lililokwenda moja kwa moja wavuni na kuipa Morocco bao la tatu.

Katika mchezo huo, kocha Poulsen alifanya mabadiliko kadhaa, lakini hayakuwa na faida kwa timu yake kwani aliwapumzisha Mbwana Samata, Mohamed Rajabu 'Machupa' na kuiwaingiza John Boko na Mrisho Ngassa.

Nahodha wa Tanzania, Henry Joseph anakiri kuwa mchezo ulikuwa mgumu na timu haikucheza kwa kiwango chake.

"Tulishindwa kucheza mchezo wetu mara zote tunapoteza mwelekeo na kushindwa kujipanga kwa ujumla tulikosa mipango," alisema Henry.


chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment