KLABU ya Yanga imewatupia
virago beki wake wa kulia na nahodha, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’ na Abuu Ubwa,
imefahamika.
Habari za kuaminika
kutoka ndani ya klabu hiyo yenye maskani yake makutano ya mitaa ya Twiga na
Jangwani, Kariakoo, jijini Dar es
Salaam zinasema, nyota hao wameachwa kutokana na
kushuka viwango.
Chanzo cha uhakika
kimedokeza kuwa kushuka kwao kiwango kuliwafanya washindwe kutoa mchango
uliotarajiwa kutoka kwao katika msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Tanzania
Bara iliyofikia tamati Mei 6.
Yanga chini ya Kocha wake
Mserbia, Kostadin Papic ilimaliza ligi hiyo kwa kushindwa kutetea ubingwa wake,
ikimaliza nafasi ya tatu nyuma ya Simba na Azam FC.
Chanzo hicho kimedokeza
kuwa, kuachwa kwa nyota hao, ni sehemu ya mkakati wa kukisuka upya kikosi cha
timu hiyo kuelekea vita ya kutetea ubingwa wa Kombe la Kagame na msimu mpya wa
Ligi Kuu.
Mbali ya kiwango, pia
kiongozi huyo amedokeza kuwa, walikerwa na utovu wa nidhamu wa ndani na nje ya
uwanja wa Nsajigwa aliyekuwa nahodha wa timu ya soka ya Tanzania,
Taifa Stars.
“Tumedhamiria kuwa na
kikosi bora, sio bora kikosi kwenye ligi kuu ijayo na michuano mingine, hivyo
hatuwezi kuwa na wachezaji walioshuka viwango,pia nidhamu mbovu,”
alisema kiongozi huyo.
Alidokeza kuwa, kwa sasa
wanaendelea na mchakato wa kusaka nyota bora ambao wataziba nafasi za wale
watakaoachwa kwa lengo la kujenga kikosi bora cha ushindani.
Mbali ya Nsajigwa na
Ubwa, nyota wengine walio kwenye hatari ya kutemwa,ni Shamte Ally, Bakari
Mbegu na Kiggi Makasy kutokana na sababu kadhaa, ikiwemo kushuka viwango.
Kuachwa kwa Nsajigwa
kunakuja huku kukiwa na habari za Yanga kuanza kusaka saini za nyota kadhaa
wakiwemo Uhuru Seleman, Juma Jabu na Juma Nyoso kwa lengo la kuimarisha kikosi
cha msimu ujao.
Shadrack, ni kati ya
mabeki shupavu nchini akijaaliwa uwezo wa pumzi kiasi cha kupanda kwenda
kusaidia mashambulizi na kushuka kuzuia, akifananishwa na lori aina ya Fuso
ambalo hutumika kubeba mizigo.
Kabla ya kutua Yanga
mwaka 2006 akitokea timu ya Moro United, Nsajigwa aliwahi kuichezea Prisons
ya Mbeya kwa mafanikio kama ilivyokuwa kwa rafiki yake, kipa Ivo
Mapunda aliyehama naye Moro Utd hadi Yanga.
Katika mechi ya mwisho ya
kufunga Ligi Kuu dhidi ya Simba iliyopigwa Mei 6 kwenye Uwanja wa Taifa,
jijini Dar es Salaam, Nsajigwa alionekana kupwaya, akisababisha penalti tatu
kutokana na kucheza rafu dhidi ya Emmanuel Okwi.
No comments:
Post a Comment