Send to a friend |
Thursday, 25 August 2011 08:37 |
BUNGE jana lilisitisha kwa muda shughuli zake za kawaida kujadili hatua ya Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo kumrejesha kazini Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo kabla ya Bunge kujadili Ripoti ya uchunguzi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Luhanjo kukutana na waandishi wa habari Dar es Salaam juzi na kuutangazia umma kwamba kutokana na matokeo ya uchunguzi huo kutomtia hatiani anaamuru Jairo arejee ofisini mara moja. “Kutokana na matokeo haya ya uchunguzi wa awali, mimi kama Mamlaka ya Nidhamu ya Katibu Mkuu Nishati na Madini, sitaweza kuendelea na hatua ya pili ya kumpa taarifa ya tuhuma. Ninaamuru David Jairo arejee kazini kuanzia siku ya Jumatano.” Hata hivyo, uamuzi huo wa Luhanjo jana uliamsha hasira za wabunge bila kujali itikadi zao za kisiasa ambao ambao walitaka Bunge lisitishe kujadili shughuli zozote kutokana na hatua hiyo ya Katibu Mkuu Kiongozi wakisema ni kudharau Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge. Hoja ya Zitto Hoja hiyo iliwasilishwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) muda mfupi kabla ya kuanza kwa kipindi cha maswali na majibu. Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni alitoa hoja kutaka Bunge lisitishe kujadili hoja zote za Serikali hadi hapo ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali iliyomsafisha Jairo itakapofikishwa bungeni na kujadiliwa. Zitto alianzisha moto huo mnamo saa 3:17 asubuhi ikiwa ni dakika moja tu baada ya Naibu Spika, Job Ndugai kutangaza taratibu za safari ya wabunge kwenda Zanzibar kwa ajili ya mazishi ya Mbunge Mussa Khamis Silima aliyefariki juzi. Alitumia kanuni ya 51 kulieleza Bunge kuwa kitendo kilichofanywa na Luhanjo kilikiuka haki, maadili na madaraka ya Bunge na hivyo akataka wabunge wenzake wamuunge mkono ili wagome kufanya shughuli zozote za Serikali hadi hapo ripoti ya CAG kuhusu tuhuma dhidi ya Jairo itakapowasilishwa rasmi bungeni. “Mheshimiwa Naibu Spika, jana kupitia vyombo vya habari tulimsikia Katibu Mkuu Kiongozi kupitia vyombo vya habari akieleza kuwa tuhuma zilizokuwa zikimkabili Jairo si za kweli na kwamba anatakiwa kurudi kazini kuanzia leo (jana),’’ alisema Zitto na kuongeza: “Mheshimiwa Naibu Spika unafahamu ya kwamba, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizungumza ndani ya Bunge hili ya kwamba angekuwa ni yeye angeshamchukulia hatua Ndugu Jairo kuhusu vitendo alivyofanya, hivyo basi naomba nitoe hoja kwamba Bunge lisitishe hoja yoyote ya Serikali mpaka itakapoleta bungeni taarifa ya CAG kuhusiana na uchunguzi huo.” Baada ya kutoa hoja hiyo, Zitto aliungwa mkono na wabunge zaidi ya nusu waliokuwamo ndani ya ukumbi, hali ambayo ilimlazimisha Naibu Spika wa Bunge, Ndugai, kuitisha Kamati ya Uongozi kwa dharura kujadili suala hilo. Hoja ya Lukuvi Baada ya hoja ya Zitto, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisimama kupinga hoja hiyo akisema Mbunge huyo hakufuata taratibu zilizotakiwa ambazo ni kuwasilisha kusudio kabla ya kutoa hoja rasmi. “Mheshimiwa Naibu Spika, najua jambo hili lina public interest (masilahi ya umma), lakini kanuni zinasema kuwa mbunge anayetaka kuwasilisha jambo lolote linalohusiana na shughuli za Bunge atafanya hivyo wakati unaofaa na uliowekwa na kanuni na atakuwa amemwarifu Spika mapema kuhusu kusudio lake, hivyo ulitakiwa kuwasilishiwa mapema ili uweze kuamua,’’ alisema Lukuvi. Akijibu hoja hiyo, Ndugai alisema: “Wakati nasoma matangazo mbalimbali kuhusiana na kifo cha Mbunge, nilipata taarifa kutoka kwa Zitto kuhusu kunitaarifu juu ya jambo hilo, hivyo basi, hoja iliyotolewa na Zitto imetolewa kwa wakati na ilifuata utaratibu unaotakiwa.’’ Uamuzi wa Kamati ya Uongozi Baada ya kikao cha dharura cha Kamati ya Uongozi ya Bunge, ilipotimu saa 3:58, kabla ya kumalizika kwa maswali na majibu, Ndugai alirejea ukumbini na kutoa taarifa kuwa kikao hicho kiliongozwa Spika wa Bunge, Anne Makinda na kukubaliana na hoja ya Zitto. “Kikao kilihudhuriwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda na alikiendesha yeye mwenyewe. Kamati imepima hoja iliyotolewa na Zitto na kuona ni hoja inayohitaji kusikilizwa na Bunge na hakuna kipingamizi chochote,” alisema Ndugai na kushangiliwa kwa nguvu na wabunge. Baada ya hapo Naibu Spika alimpa nafasi mtoa hoja, Zitto kuanza kujadili hoja hiyo na Mbunge huyo alisema jambo hilo lilikuwa ni la aibu kubwa mbele ya wabunge na taifa kwa ujumla. “Jambo hili lilianzia bungeni na hivyo ripoti hiyo ilipaswa kuanzia humu bungeni. Kitendo cha Katibu Mkuu Kiongozi ni dharau kwa Bunge na kwa kuwa Waziri Mkuu alisema anamsubiri Rais, amemdharau na ninasema kama ningekuwa mimi ni Waziri Mkuu ningejiuzulu nafasi yangu mara moja,’ ’alisema Zitto. Zainabu Vullu Mbunge wa pili kuchangia hoja hiyo alikuwa Zainabu Vullu (Viti Maalumu - CCM), alisema kitendo hicho kinaudhi na kuwataka wabunge kuungana akisema madaraka yao yalikuwa yameingiliwa. “Nianze kwa kuangalia Katiba kifungu namba 63 cha katiba Ibara ya Pili ambayo inasema sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndiyo chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka kwa niaba ya wananchi kusimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa katiba,” alisema Vullu na kuongeza: “Suala lile liliibuliwa ndani ya Bunge hili na baada ya kuibuliwa, Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye naye ni mbunge mwenzetu lilimgusa. Ni matarajio yetu baada ya utafiti na uchunguzi uliofanyika suala hili lingerudi kwetu tukalijadili na kuona nini kilichotokea na kuhabarisha wananchi wetu ni jinsi gani ya matumizi ya fedha za nchi hii ambazo jasho la wananchi zilivyotumika.” Alisema kutokana na taarifa ya Luhanjo, bunge ni kama limedhalilishwa na kwamba halikupewa haki yake kwani wabunge wote wameonekana kama watu wasiojua wajibu wao. Sendeka Mjadala wa hoja hiyo ulihitimishwa na mchangiaji wa tatu, Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka ambaye alikuja na hoja jingine ya kuomba Bunge lipitishe azimio la kuunda Kamati Teule kuchunguza suala hilo. Hoja hiyo, kama ilivyokuwa ile ya Zitto pia iliungwa mkono na wabunge karibu wote. Sendeka alisema kitendo cha Luhanjo kutangaza ripoti hiyo ni kupoka nafasi ya Bunge na kwamba Waziri Mkuu amedharauliwa kwa kiasi kikubwa. “Ninaomba kutumia kanuni ya 117 kuliomba Bunge lako tukufu sasa liamue kuunda kamati teule itakayoangalia pamoja na mambo mengine, kuingiliwa kwa uhuru wa Bunge, lakini mchakato mzima uliosababisha fedha zote zile zikusanywe na kugawanywa na kuitishwa kama fedha za harusi wakati tunajua kwamba kila waziri anapewa kasma ya maandalizi ya bajeti inayokuja,” alisema Sendeka na kuongeza: “Wote (watumishi) waliokuja waliweza kuja na mafuta kutoka katika ofisi zao naomba Bunge hili, Mheshimiwa Naibu Spika liniunge mkono kwa kutoa hoja kwa mujibu wa kanuni ya 117, fasili ya kwanza ya pili mpaka ya nne ambayo inaweka masharti ya kuundwa kwa kamati teule na hii itasaidia sana kuitendea haki hoja hii na kulinda hadhi ya Bunge lako tukufu.” Msimamo wa Bunge Baada ya Sendeka kutoa hoja hiyo, Ndugai alisimama na kusema: “Sasa hoja hiyo Mheshimiwa Ole - Sendeka ameiboresha kwa kutoa hoja ya kuunda tume teule ambayo waheshimiwa wabunge mmeiunga mkono kwa wingi sana kwa kutumia kanuni ya 117 ambayo inasema kamati teule inaweza kuundwa na Bunge kwa madhumuni maalumu kwa hoja mahsusi itakayotolewa na kuafikiwa.” “Mimi ninakubaliana na jambo hili na kwa jinsi hiyo, kufuatana na kanuni hiyo ya 117 Bunge hili litaunda tume teule kwa ajili ya kulichunguza jambo hili kwa sababu Bunge ni mhimili, haliwezi kudharaulika kiraisi na tunaiheshimu na kuipenda sana Serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete na Waziri mkuu wake Mizengo Pinda.” “Si rahisi kwa Bunge kuonekana Waziri Mkuu akidharaulika likanyamaza! Haiwezekani, kama dharau inaweza kutokea hukohuko si ndani ya Bunge hili.” Baada ya uamuzi huo, Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono alijaribu kupinga uamuzi huo akitaka jambo hilo liende kwa utaratibu ili Bunge lisije likaingilia taratibu za mihimili mingine. Alihoji kwa kitendo cha kutompatia nafasi Jairo ili ajieleze lakini Ndugai alisema jambo hilo alishalifunga lakini akamtoa shaka mbunge kuhusu haki: “Kama ni kuhojiwa basi ataitwa akahojiwe huko asipotendewa haki hiyo utaleta hoja yako.’. Jairo apokewa kishujaa Wakati wabunge wakimng'ang'ania, Jairo alipokewa kwa mbwembwe aliporipoti ofisini kwake Dar es Salaam huku baadhi ya wafanyakazi wakisukuma gari lake na kuimba: “Baba, baba baba huyooo, karibu baba, karibu baba, umeshinda vita karibu nyumbani.’ Akizungumza baada ya kuingia ofisini, Jairo alisema: “Nimesamehe kwa upendo mkubwa. Siwezi kulipiza kisasi, wala sitachukua hatua zozote kwa kuwa mimi ni Mkristo nimerudi kwa amani, tuchape kazi tujenge nidhamu,” alisema. Mara baada ya kufika ofisini kwake, Jairo akionekana mwenye uso uliojaa furaha huku akilengwa na machozi alisimama mbele ya kiti chake akiwa kimya akitazama chini na kisha alitoka na kuelekea ofisini kwa Waziri wake, William Ngeleja. “Nimejipanga kuchapa kazi kwa bidii na kudumisha ushirikiano uliokuwapo tangu awali, nashukuru haki imetendeka na sitawashtaki wale walionituhumu,’’ alisema Jairo na kuongeza kwamba watu wajielekeze kwenye mambo ya maendeleo kuliko kufuatilia mtu mmojammoja, kwa kuingiza maslahi binafsi. Waziri Ngeleja alisema ameshukuru kwamba Jairo amerudi baada ya misukosuko ya hapa na pale. LHRC wapinga Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimepinga hatua ya Serikali kumsafisha Jairo na kisha kumtaka arejee kazini, kikisema hatua hiyo imedhalilisha Bunge. “Taarifa ya kusafishwa kwa Jairo inaashiria mambo matatu, kwanza inaonyesha kuna mkakati wa kuwalinda viongozi pale wanapofanya makosa. Pili, taarifa hiyo imelidhalilisha Bunge ambalo ndilo lilifichua kashfa hiyo, Beatrice Shelukindo ndiye aliyefichua hayo. Tatu, taarifa hiyo imemdhalilisha Waziri Mkuu na kumfanya aonekane kutokuwa makini na kauli zake hasa pale aliposema kuwa angeweza kumchukulia hatua Jairo lakini anasubiri taarifa ya Rais.” Policy Forum yakosoa Mratibu asasi ya kiraia ya Policy Forum, Semkae Kilonzo alisema Serikali imechukua uamuzi huo bila ya kuzingatia uzito wa jambo husika. Alisema umefika wakati iache kufanya kazi kwa mazoea na iheshimu mamlaka ya mihimili mingine. Alisema Katiba ya sasa katika Ibara ya 63, kifungu kidogo cha 1 hadi 3 inaeleza bayana, mamlaka ya Bunge na kusisitiza kuna haja ya mhimili huo kupewa meno zaidi kwa mujibu wa sheria ili ushauri na maoni yake yaweze kutekelezeka. “Wabunge walishaeleza maoni yao kuhusu sakata hilo lakini serikali imechukua hatua bila ya kuzingatia uzito wa jambo lenyewe, cha msingi hapa ni bunge liongezewe meno zaidi ili kazi zake ziweze kuheshimika na kutekelezeka,” alisema Kilonzo. mwananchi |
SIKU moja baada ya Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, kumrejesha kazini Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, Rais Jakaya Kikwete, amemsimamisha tena kazi ili kupisha uchunguzi zaidi -Chanzo MWANANCHI
ReplyDelete