POLISI YAWATUHUMU UAMSHO, YATANGAZA KUWASAKA POPOTE, VURUGU ZAENDELEA
Na: Salma Said,MWANANCHI
MACHAFUKO yanayoambatana na ghasia,
yamechukua sura mpya, baada ya askari mmoja wa Kikosi cha Kutuliza
Ghasia (FFU), CPL Said Abdulrahman kuuawa kwa mapanga na watu wanaodaiwa
kuwa wafuasi wa kikundi cha Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki).
Tukio hilo limekuja ikiwa ni siku moja
baada ya kikundi cha watu hao kufanya ghasia wakitaka kiongozi wao,
Sheikh Farid Hadi Ahmed aliyetoweka katika mazingira ya kutatanisha
arudishwe wakiamini kuwa, polisi walimteka.
Habari zilizopatikana jana zilidai kuwa mauaji hayo yalifanyika eneo la
Bububu katika mji wa Unguja Visiwani Zanzibar. Kamishna wa Polisi
Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema Mjini Unguja jana kuwa, askari
aliyeuawa ni mwenye namba F.2105 wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU),
cha Mkoa wa Mjini Magharibi.
"Wafuasi wa Uamsho wamempiga mapanga kichwani na mikononi wakati akirudi
kutoka kazini saa 6:30 usiku eneo la Bububu.
Tuelewe kwamba aliyeuawa ni askari
polisi, ni raia wa Tanzania na ni muumini wa dini ni lazima tuhakikishe
waliofanya unyama huu wanakamatwa," alisema na kuongeza:
"Tutawasaka kwa udi na uvumba na kufikishwa mahakamani kwa mauaji na
sheria za nchi zitachukua mkondo wake,” alisisitiza Kamishna huyo.
Vurugu zaendelea
Pamoja na tamko hilo, hadi jana jioni vurugu hizo ziliendelea kwa vijana
hao kuchukua misalaba makaburini, viti na meza na kuviweka barabarani
kisha kuvichoma moto.
Mwandishi wa habari hizi na wenzake
kadhaa, walinusurika kuvamiwa na wafuasi wa Uamsho wakati wanatokea eneo
la Kwerekwe, baada ya kundi la watu kuwazunguka na kuziba barabara kwa
magogo, kisha kuchoma matairi ya gari.
"Tumefukuzwa kwa mawe na hao ubayaubaya
na nusura niligonge gari. Jamaa walituzunguka katikati, wametuwekea
magogo na huku wametuwashia matairi ili tusipite. Kidogo leo tufe
billahi!" alisema mwandishi huyo.
Kutokana na vurugu hizo, polisi iliwaita
viongozi watano wa Uamsho na kuhojiana nao kuhusu suala hilo, na hadi
tunakwenda mitamboni hakukuwa na taarifa zaidi kuhusu hali hiyo.
Akizungumzia tukio la kutoweka kwa
kiongozi wa Uamsho, Sheikh Farid Hadi Ahmed, Kamishna alisema: "Ilikuwa
saa 6:30 mchana wa juzi tulipokea taarifa kutoka kwa Sheikh Msellem Ally
kwamba kiongozi mwenzao wa Jumuiya ya Uamsho ametekwa na haonekani
tangu jioni ya Oktoba 16.
"Baada ya taarifa hii, uchunguzi ulianza na mmoja wa watu waliohojiwa ni
Said Omar Said ambaye ni ndugu wa Sheikh Farid ambaye ni dereva na
ndiye aliyekuwa naye walipokwenda katika eneo la Mazizini kununua umeme
kutokana na maelezo ya dereva huyo."
Kamishna Mussa alisema kwa mujibu wa
Said, Sheikh Farid alimwamuru dereva huyo kwenda nyumbani kupeleka umeme
wakati yeye akizungumza na watu walikuwamo ndani ya gari aina ya Noah
ambalo hata hivyo nambari zake za usajili hazikufahamika.
Alisema ilipotimu saa 6:30 mchana juzi wakati taarifa hizo zinapelekwa
kituoni, wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho walikuwa wanaendelea kujikusanya
katika msikiti wa Mbuyuni na kuanzisha fujo kwa kuwasha moto kwenye jaa
lililokuwa karibu na msikiti huo.
"Baadaye fujo hizo zilisambaa katika
maeneo mengine ya mjini kwa kufanyika uharibifu wa mali za Serikali,
Chama Cha Mapinduzi na wananchi wa kawaida,” alisema.
Alisema katika vurugu hizo watu hao walichoma moto magari kadhaa, ambapo
gari la Serikali lilivunjwa kioo kidogo cha pembeni, gari la Zimamoto
kuvunjwa kioo cha mbele pamoja kuvunja duka la pombe na kuiba mali
zilizokuwamo ndani.
Kamishna Mussa alisema, mpaka sasa, watu
10 wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika katika vurugu hizo.
Kauli ya SMZ
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, SMZ, imewataka wananchi kuendelea na
shughuli zao kama kawaida kwa maelezo kuwa vyombo vya ulinzi na usalama
vimeimarisha ulinzi katika maeneo yote ya Zanzibar.
Taarifa ya Serikali iliyotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed imesema Zanzibar bado ni shwari na
inaendelea kuwa katika hali ya amani na utulivu.
Akizungumzia tukio la vurugu zilizotokea
juzi, Aboud alisema kwamba vikundi vya vijana vinavyosadikiwa kuwa ni
wafuasi wa Sheikh Farid vilifanya vurugu katika mitaa ya Darajani,
Michenzani, Mwembeladu, Magomeni na Amani wakidai kwamba kiongozi wao
ametekwa.
Alisema Serikali imewasiliana na vyombo vya dola wakiwamo Polisi, Jeshi
la Wananchi wa Tanzania, Idara ya Usalama wa Taifa, Vikosi vya Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar, KMKM, JKU, Chuo cha Mafunzo, Zimamoto na Valantia
na vyote vimeeleza kuwa havielewi chochote kuhusu Sheikh Farid.
Aboud alisema wakati Jeshi la Polisi
likiendelea na upelelezi wao, wananchi wanapaswa kutulia na kutoa
taarifa kuhusu tukio hilo kwa vituo vya polisi au kupitia Masheha, Ofisi
za Wilaya na Mikoa katika maeneo yao.
Waziri Aboud alisema kuwa Serikali
inawasihi wananchi kuacha kujiingiza katika fujo na vurugu kwani kufanya
hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria na Serikali haitavumilia vitendo
hivyo.
CCM, CUF walaani
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wa CCM, wamelaani ghasia
zilizofanywa na kikundi cha Uamsho katika mitaa mbalimbali juzi.
Akizungumza kwa niaba ya wawakilishi wa
CCM kwenye Ukumbi wa Baraza hilo lililopo Bweni, Hamza Hassan Juma
alisema wakati umefika kwa hatua kali za kisheria kuchukuliwa kabla ya
hali haijawa mbaya zaidi.
"Isifike mahali Zanzibar ikageuka taifa la machafuko na kuwafanya
wananchi kushindwa kuishi kwa amani," alisema huku akimtaka Mkuu wa
Polisi, IGP Said Mwema kusimama kidete kumaliza hali hiyo.
Wawakilishi hao wa CCM, waliitaka Serikali kuwalipa fidia wote
walioathirika na ghasia hizo na vikosi vya usalama SMZ kusaidia kuweka
ulinzi wakati wote katika mji wa Zanzibar.
Juma alifika mbali zaidi na kusema kuwa,
Jumiki si chama cha siasa, hivyo kuiomba Serikali kuifuta kwa maelezo
kwamba imekosa mwelekeo kwa kuchochea vitendo vya uvunjifu wa amani.
Wajumbe hao waligoma kuingia Barazani jana ikiwa ishara ya kuonyesha
msimamo wao kulaani hali hiyo.
Kwa upande wake, Chama cha Wananchi CUF
kimeelezea kusikitishwa na matukio ya vurugu Visiwani Zanzibar.
"Kutokana na vitendo hivyo, Chama cha Wananchi kinalaani kwa nguvu zote
matukio hayo ambayo yamesababisha uvunjifu wa amani, na kusababisha
hofu na taharuki kwa raia pamoja na wageni wanaotembelea Zanzibar”,
ilisema taarifa ya CUF iliyotolewa Zanzibar jana.
CUF katika taarifa hiyo, pia walieleza
kushtushwa na habari za kutoweka kwa Sheikh Farid Hadi Ahmed katika
mazingira ya kutatanisha, hivyo kuitaka SMZ kuzidisha juhudi za
kumtafuta.
Kwa upande mwingine, CUF inawataka
wanachama wake, wapenzi na wananchi wote kutojiingiza na kutofanya
vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani ya nchi yetu.
No comments:
Post a Comment