Thursday 20 December 2012

KATIBU IKULU ASOTEA MAFAO HAZINA MIAKA 30!


KATIBU wa Kwanza wa Rais (Ikulu- Habari), Paul Sozigwa bado anasotea mafao yake tangu alipostaafu utumishi wa Serikali takriban miaka 30 iliyopita, Mwananchi imeelezwa.

Sozigwa ambaye alistaafu utumishi serikalini mwaka 1983, baada ya kutumikia katika nyadhifa mbalimbali, amesema licha ya utumishi huo, hajalipwa mafao yake hadi sasa.
Mbali na kuwa Katibu wa Ikulu, nyadhifa nyingine alizoshika ni Mkurugenzi wa Kwanza wa Redio Tanzania (RTD), Ofisa Wilaya (DO), Wilaya Kisarawe katika Serikali ya Kikoloni na Katibu Mkuu, Wizara ya Habari na Utangazaji.

Ndani ya CCM, Sozigwa amepata kushika nafasi mbalimbali, zikiwamo za Mjumbe Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec), Kamati Kuu (CC) na Mwenyekiti Tume ya Taifa ya Udhibiti na Nidhamu na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani.

Sozigwa alisema tangu alipostaafu kazi serikalini, amekuwa akifuatilia mafao yake Hazina bila mafanikio na mara zote amekuwa akizungushwa kwa maneno ya kuridhisha yasiyotekelezeka.

Hivi karibuni, mwandishi wetu alimwona Sozigwa akiteremka kwenye daladala katika Kituo cha Magomeni Mapipa, Dar es Salaam akiwa na bahasha ya khaki mkononi na katika kusalimiana, alisema alikuwa ametoka Hazina kufuatilia mafao hayo.

“Natoka Hazina kufuatilia faili langu. Nazunguka, sijakata tamaa, lakini najua kuwa ipo siku nitapata haki yangu,” alisema Sozigwa, huku akilazimisha tabasamu kabla ya kukunja tena uso huku akinyanyua mguu kupiga hatua nyingine.
“Kuna wakati unaambiwa limeonekana linashughulikiwa na mara nyingine jibu kutoka kwa makarani ni kuwa halionekani.”
Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa hakupatikana jana kuzungumzia madai hayo lakini Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi), Celina Kombani alisema kuwa Serikali haina taarifa za Sozigwa kusotea mafao yake.
“Mimi sina taarifa hizo... alete taarifa na vielelezo vyake, sasa kama analalamikia huko tutashindwa kumsaidia,” alisema Kombani.

CCM kimepoteza mwelekeo
Akizungumzia mwenendo wa CCM, Sozigwa alisema anavyokiangalia, kinakwenda harijojo kutokana na baadhi ya watu kukigeuza kuwa kikundi cha watu fulani badala ya mali ya umma.

“Hali sasa si shwari kwani chama kimekuwa cha kikundi cha watu na siyo wananchi jambo ambalo linachangiwa na kupuuzwa kwa mfumo na misingi ya Tanu na Afro Shiraz ambavyo ndivyo vimezaa CCM,” alisema.

Alisema hivi sasa watu hawajui mipaka ya kazi zao hali ambayo inazua malumbano zaidi kuliko kuwatumikia wananchi. Anatoa mfano wakati akiwa Tume ya Taifa ya CCM, Udhibiti na Nidhamu, alisema kuwa ilikuwa na mtandao wa kiintelijensia.

“Mtu aliitwa, alielezwa na kuonyeshwa ushahidi kuhusu tuhuma zake na wapo ambao waliwajibishwa kabla ya vikao vya chama na wengine walionywana kuachwa kuendelea na shughuli zao, sasa mfumo umekufa,” alisema.

Hata hivyo, alisema iwapo Sekretarieti ya Halmashauri Kuu Taifa ambayo imechaguliwa hivi karibuni inarudi kwa watu kama alivyosema Katibu Mkuu, Kinana (Abdulrahman) litakuwa jambo jema.
Habari zaidi soma ndani, Jarida la Siasa.

MWANANCHI

No comments:

Post a Comment