Friday, 24 August 2012

Mramba azidi kumkandamiza Mkapa mahakamani



ALIYEKUWA Waziri wa Fedha Basil Mramba, jana aliendelea kumkandamiza aliyekuwa bosi wake na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, akimhusisha moja kwa moja na kutolewa kwa msamaha wa kodi kwa kampuni ya Alex Stewart Government Business Assayers.

Mramba aliyaeleza hayo jana wakati akijitetea dhidi ya tuhuma zinazomkabili za matumizi mabaya ya ofisi za umma na kuisababishia Serikali hasara ya Sh11.7 bilioni na kwamba alitoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo ili kutekeleza matakwa ya mkataba.

Alidai kuwa kifungu cha 4.3.1  kilichopo kwenye  mkataba huo ulioingiwa kati ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Alex Stewart Government Business Assayers kinasema malipo yoyote  yatakayolipwa na mkataba huo hayatotozwa kodi. 
“Mimi nilichofanya ni kutekeleza  matakwa ya mkataba huu kwa sababu Waziri wa Fedha  pekee ndiye mwenye mamlaka  ya kutekeleza mkataba huo,” alidai Mramba.

Mramba alikiri kuruhusu gavana wa BoT kuilipa kampuni ya Alex Stewart,  Dola za Marekani 1 milioni kama malipo ya awali, kwa ajili ya kufanya maandalizi ya ukaguzi wa migodi ya madini, na kwamba fedha nyingine zingelipwa kwa awamu. 
Mramba alisema aliruhusu malipo hayo kufanyika kutokana na kuwapo kwa barua  ya Mei 13, 2003, kutoka kwa Katibu Mkuu wa Rais, Patrick Mombo  kwenda kwa Katibu Mkuu wa Nishati na Madini kuhusu mkaguzi wa dhahabu ikisema “Rais amekubali Waziri wa Fedha na BoT watafute njia ya kuilipa kampuni ya Alex Stewart Government Business Assayers”. 
“Maagizo yote mimi niliyachukulia  kama ni ya Rais, alikuwa akiagiza watendaji wake kutekeleza majukumu yote,”alisema Mramba na kuongeza kuwa kwa kuzingatia makubaliano hayo alitafuta fedha hizo kupitia bungeni katika Bajeti ya Serikali ya 2003/04.

Kuhusu mkataba, Mramba alisema kuwa anachofahamu yeye sheria ya BoT inampa mamlaka Gavana kuingia mikataba na kuisaini na kwamba mikataba yote aliyoingia na watu wengine ni lazima kodi isamehewe. 
Mramba aliiambia mahakama hiyo kuwa, kampuni ya Alex Stewart Government Business Assayers ilikuwa ikitaka malipo bila kodi na kwamba, wao walikubali kutomtoza kodi kutokana na ushauri kutoka kwa wataalamu akiwamo gavana kuwa wamsamehe kodi vinginevyo wangemlipa zaidi.   
Hata hivyo, alisema mkataba baina ya BoT na kampuni hiyo haukuwahi kupitia katika kikao cha Baraza la Mawaziri. “Sikudhani kama angeweza kutiliana nao saini kwenye mkataba huo,  bila Baraza la Mawaziri kuridhia,”alisema Mramba. 
Ushauri wa TRA

Mramba alibainisha kuwa Bethar Soka  ambaye alikuwa kwenye kamati iliyofanya mchakato wa kuitafuta kampuni hiyo ya ukaguzi wa dhahabu, aliomba kupata kauli ya TRA  kama kampuni ya Alex Stewart Government Bussines Assayers isamehewe kodi ama la, Mei 26, 2003. 

Alidai kuwa baada ya  Soka kupeleka ombi hilo Mei 26, 2003, TRA katika majibu yao ya Juni 24, 2003 walisema kuwa hawapendekezi mkaguzi huyo wa dhahabu asamehewe kodi na kwamba barua hiyo ilipelekwa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha wakati BoT na kampuni ya Alex Stewart Government Business Assayers iliingia mkataba  Juni 14, 2003.

“Inaonyesha barua hiyo ya TRA ilichelewa  kwa siku 10, baada ya mkataba kusainiwa,  hata hivyo, ushauri huu wa TRA hatukuuhitaji  hata kama ungekuja  haungekuwa na manufaa,” aliongeza kudai Mramba. 

Baada ya maelezo hayo, mmoja wa wanaosikiliza kesi hiyo, Hakimu Saul Kinemela, alimuuliza Mramba, Wizara ya Fedha  iliomba ushauri  huo TRA kwa kazi gani? 

Akijibu swali hilo, Mramba alisema, "Siyo Wizara ya Fedha iliomba ushauri TRA, bali Soka aliomba ushauri huo kama mwanakamati iliyokuwa ikifanya mchakato wa kutafuta kampuni hiyo na  kwamba  Soka yeye  alikuwa ni mtumishi wa wizara yake. 

Alibainisha kuwa  Soka  asingeweza  kumshauri  Waziri,  anayeweza kumshauri ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu. 

Mbali na Mramba, wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja. 
Jaji John Utamwa aliiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 12, mwaka huu itakapoendelea na utetezi. 
Utetezi wa awali

Mramba (71) alianza kujitetea, Agosti 22, mwaka huu  ambapo alidai kuwa Serikali iliiteua BoT ifanye kazi ya kutafuta  kampuni inayoweza kufanya kazi hiyo hivyo ikaingia mkataba na kampuni iliyochaguliwa  ya Alex Stewart Government Bussines Assayers. 

Waziri huyo wa zamani aliongeza kudai kuwa aliyeagiza BOT kufanya kazi hiyo ya kumtafuta mkaguzi wa dhahabu ni Rais wa Awamu ya Tatu, Mkapa na kwamba wakati huo yeye akiwa Waziri wa Wizara ya Fedha alipewa jukumu la kuhakikisha gharama za kumlipa mkaguzi huyo zinapatikana ndani ya Serikali au BoT ama pengine popote.

Alifafanua kuwa kati yake yeye na gavana  hakuna aliyekuwa na mamlaka  juu ya mwingine na kwamba gavana alikuwa  na wajibu wa kufanya mchakato wa kumtafuta mkaguzi wa dhahabu. 

Mramba alisisitiza kudai kuwa yeye hakuhusika kwenye mchakato huo kwa kumtafuta wala kumleta hapa nchini  wala kumtuma mwakilishi  yeyote  kumwakilisha kwenye kamati iliyoteuliwa  kufanya mchakato huo bali alipewa agizo la kumlipa. 

“Mimi kama waziri sikuwa na mtu wangu kwenye ile kamati, lakini Wizara ilituma mwakilishi, ambaye alikuwa mwanasheria Bethar Soka wakati wa kuhoji kampuni mbili  ili wachague na kwenye kujadili vipengele vya mkataba,”alisema. 

Inadaiwa kuwa, kati ya Agosti mwaka 2002 na Juni 14, mwaka 2004, jijini Dar es Salaam, washtakiwa wakiwa watumishi wa umma, walitumia vibaya madaraka yao na kuisababishia Serikali hasara ya Sh11.7 bilioni. 

Ilidaiwa kuwa washtakiwa hao waliipatia msamaha wa kodi isivyo halali, Kampuni ya M/S Alex Stewart ya Uingerez

Chanzo.mwananchi

No comments:

Post a Comment