Thursday, 16 August 2012

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAKANUSHA UVUMI JUU YA KUHAMISHWA KWA WAMASAI SERENGETI

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Khamis Suedi Kagasheki amekanusha uvumi unaosambazwa na Shirika moja kupitia mtandao wake wa AVAAZ.org kuwa watanzania wa Jamii ya Kimasai wapatao 48,000 watahamishwa kutoka eneo lao (la Serengeti) kupisha Wafalme kutoka Mashariki ya Kati ili walitumie eneo hilo kwa uwindaji wa Simba na Chui.

Taarifa hiyo iliyosambazwa na mtandao huo imewataka watu kutoka duniani kote kujiorodhesha ili wafikie angalao 150,000 ili kumshinikiza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuacha kusaini mkataba ambao utafanya uhamisho huo utekelezwe.

Waziri Kagasheki amesisitiza kuwa uvumi huo siyo kweli na hauna msingi wowote kutokana na sababu zifuatazo:

Kwanza, hatua kama hii haiwezi kuchukuliwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Hifadhi ya Serengeti maana hakuna watu wanoishi ndani ya hifadhi hiyo. Pia kitendo hicho hakijapangwa kufanyika katika Wilaya ya Serengeti iliyoko mkoani Mara.

Pili, hata kama taarifa hiyo ilimaanisha Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, bado siyo kweli maana wilaya hiyo haina idadi ya Wamasai wanaofikia jumla ya 48,000.

Tatu, ndani ya ya Hifadhi ya Serengeti hakuna eneo lolote ambalo limetengwa kwa ajili ya wafalme wa Mashariki ya Kati ili waweze kulitumia kwa uwindaji wa Simba na Chui.

Nne, habari hizo siyo kweli maana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hahusiki kabisa na ugawaji wa vitalu vya uwindaji popote pale nchini. Hii ni kazi ya Wizara ya Maliasili na Utalii, na Wizara haijafanya hivyo katika eneo tajwa.

Pamoja na ufafanuzi huo Waziri Kagasheki amewaasa watu waliojiorodhesha, na wanaotarajia kujiorodhesha, kuwa wamepotoshwa, hivyo wanatakiwa wasisaini kubariki kitu mbacho hawakijui wala hakipo.

[MWISHO]

George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
Tarehe 15 Agosti 2012
Simu: +255 784 468047.

No comments:

Post a Comment