Wednesday, 26 September 2012
KIKWETE-ANAYETAKA KUONDOKA CCM RUKSA
NI WALE WANAOTISHIA BAADA YA KUTOSWA, AWASHANGAA WANAOTISHIANA SILAHA KWA AJILI YA UONGOZI
Na: Midraji Ibrahim na Habel Chidawali, Mwananchi
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amewatolea uvivu wagombea wa nafasi mbalimbali ambao majina yao yamekatwa, akisema wanaotaka kukihama chama hicho kwa sababu wametoswa, waondoke haraka. Licha ya kuwatakia safari njema, Rais Kikwete aliwatupia lawama baadhi ya wanaCCM ambao wameripotiwa kuendesha malumbano na kugeuza uchaguzi huo kama uwanja wa vita. Akifungua kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) jana, Rais Kikwete alisema kumekuwapo na taarifa mbalimbali ambazo zimemfikia pia kwamba baadhi ya wanachama wanatishia kukihama chama hicho kama majina yao yatakatwa.
“Wako wenye ndimi mbili ambao wanasema kuwa wasipoteuliwa wanaweza kuondoka. Ah! Mimi nasema watangulie huko maana inaonyesha kuwa walishaandaa maeneo ya kwenda,” alisema Rais Kikwete huku akishangiliwa na wajumbe wa Nec. Alisema CCM kinayo taarifa kuhusu watu kugombana na hata kutoleana silaha, jambo alilosema linashangaza, huku akihoji kuna nini katika uongozi tena Nec? “Uchaguzi usigeuzwe uwanja wa fujo.
Wengine wanatoleana silaha kama majembe, ngumi na silaha nyingine, hivi wanagombana nini huko? Uchaguzi usigeuzwe kuwa ni uwanja wa vita.” alisema. Hivi karibuni, baadhi ya makada wa chama hicho wamekuwa wakitoa kauli mbalimbali za kukitishia chama hicho akiwemo Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono ambaye alikaririwa akisema kama jina lake halitapitishwa, patachimbika. Mbunge huyo alisema hayo siku chache baada ya jina lake kutupwa na Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi iliyokuwa ikipitia na kuteua wagombea watatu kwa ajili ya kuwania nafasi ya mwenyekiti wa jumuiya hiyo.
"Hapatatosha CCM," alisema Mkono alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu kutoswa kwake katika mchujo wa awamu hiyo ya awali. Ingawa Rais Kikwete hakutaja majina, Mbunge wa Nzega Dk Khamis Kigwangallah na Hussein Bashe nao waliripotiwa kutoleana maneno makali hata kuonyeshana bastola, huku Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja na Mbunge wa Kahama, James Lembeli wakiendesha malumbano kwa muda mrefu. Inadaiwa kuwa majina hayo yote na ya vigogo wengine yamekatwa na jana baadhi yao walikuwa wanadai kuwa CCM kinataka kuzalisha upinzani ambao utakisababishia kushindwa katika safari yake kisiasa hasa katika mfumo huu wa vyama vingi. Licha ya makaripio hayo, Rais Kikwete alibainisha kuwa CCM kinasemwa na watu kuwa kinakithiri rushwa katika chaguzi zake hivyo akawataka wagombea kubadilika kabla ya kukamatwa na Takukuru. “Zipo taarifa ingawa hatujazithibitisha kwamba wapo baadhi ya wagombea wanamwaga fedha sijawahi kuona… Takukuru wapo wanaendelea na kazi. Chama chetu kinasemwa tujipe fursa ya kubadilika, tusisubiri kukamatwa na kuanza kuilaumu PCCB.”
Kuhusu uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali, Rais Kikwete alisema katika uchaguzi huo, wamejitokeza watu wengi tena vijana wasomi na kwamba Kamati ya Usalama na Maadili na Kamati Kuu, zimewapandisha na kuwakata waliotumikia chama muda mrefu. “Kama hukuteuliwa kuna mawili, ama nafasi zimejaa au hufai una upungufu kidogo na huo ni utaratibu wa chama siyo kuoneana,” alisema Rais Kikwete huku akishangiliwa.
Alisema katika uteuzi huo vijana watapewa nafasi zaidi kutokana na ukweli kuwa, chama bila ya vijana hakiwezi kuwa imara kwa sababu ndiyo nguvu ya ushindi. “Hao watakaoachwa watambue kuwa tunafanya hivyo kwa ajili ya kutengeneza timu ya ushindi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2014 na Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa Bara na Visiwani, hivyo kuachwa jina lako isiwe nongwa,” alisema na kuongeza: “Lazima tukipe chama chetu watu wa kushinda… Lazima tutambue sasa tunaunda timu ya ushindi wa chama siyo ushindi wa mtu.” Hata hivyo, Rais Kikwete alitoa angalizo kuwa anajua kikao cha Halmashauri Kuu kingekuwa na mjadala mzito, lakini lazima wakipe chama watu wa kushinda. Majina manne Kamati Kuu ya CCM, inadaiwa kupendekeza majina ya wagombea wanne kwenye jumuiya zake, tofauti na kanuni ya chama hicho ya nafasi moja kuwaniwa na watu watatu. Kikao chake kilichomalizika juzi usiku, kinadaiwa kubadili kanuni ya kupendekeza wagombea watatu kwa nafasi moja na kwamba, hivi sasa mapendekezo hasa kwenye jumuiya ni wagombea wanne.
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zilidai kuwa, hatua hiyo inalenga kutoa ushindani kwa wagombea. Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipotakiwa kuzungumzia suala hilo hakukanusha wala kukubali zaidi ya kusema kwamba hata kama utaratibu huo umetumika siyo mara ya kwanza kwa chama hicho. Alisema kama Jumuiya ya Vijana wanaojitokeza lengo lao linakuwa kupata uzoefu na kwamba, idadi ya majina inategemeana na busara za kikao kinavyoona ili kutoa nafasi kwa wagombea kujipima.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment