Monday, 17 September 2012

MICHANGO YAMFIKIA MJANE WA MWANGOSI

Ndugu zangu,
Leo jioni nilifunga safari kwenda kumwona mjane wa marehemu Daud Mwangosi. Anakoishi ni maeneo ya Mwanyingo hapa Iringa.
Mjane amerudi juzi jioni kutoka msibani Tukuyu. Itika, jina la mjane wa marehemu, anawashukuru kutoka ndani ya moyo wake, wale wote waliomchangia na wanaoendelea kumchangia fedha kama pole ya msiba mkubwa uliomkuta.
"Mungu ndiye atakayewalipa"- Anasema Itika Mwangosi, mjane wa marehemu.
Amerudi kutoka msibani hakiwa hana cha kuanzia. Leo pekee tumefanya jitihada ya ziada kuhakikisha maji hayakatwi kutokana na bili iliyochelewa kulipwa kutokana na msiba wa ghafla wa Daud Mwangosi . Kutokana na michango yenu, kesho Jumatatu familia italipa deni la maji lisilozidi shilingi laki moja na nusu.
Nilichokiona kwa mjane wa Daud Mwangosi ni uhalisia wa hali aliyo nayo sasa. Anafikiria jinsi atakavyomudu kuishi na kuitunza familia. Alifarijika sana aliposikia amechangiwa kiasi cha fedha kinachozidi shilingi milioni tano hadi sasa. Anaamini, kuwa ataweza kupata pa kuanzia ikiwamo kutumia ofisi ya marehemu Mwangosi kwa shughuli za biashara ndogo aliyoifikiria. Anafikiri pia kufuga kuku, maana nyumba anayoishi ina eneo kubwa.
Na katika kumsaidia kumwongoza kwenye shughuli hizi za ujasiri amali, Mama Mfugale, mmoja wa wajasiri amali maarufu hapa Iringa amejitolea kumpa ushauri na kumwelekeza mjane wa marehemu namna ya kwenda mbele. Na katika siku chache zijazo, mjane wa marehemu atafungua akaunti NBC ambapo pia fedha mlizomchangia zitaingizwa humo ifikapo mwisho wa mwezi huu.
Dada Janet Mwenda Talawa hivi majuzi aliwasiliana nami na alikuja na ushauri wa mjane wa marehemu apewe mafunzo ya ku-edit mikanda ya video ili aweze kuitumia vema studio aliyoachiwa na marehemu mumewe kwa shughuli za namna hiyo. Nilifikisha wazo hilo, na mjane wa marehemu ameonyesha utayari wa kujifunza.
Mwana wa kwanza wa marehemu Mwangosi aitwaye Nehemia, tayari amesharipoti shuleni Malangali, huko anasoma kidato cha nne, anajiandaa na mitihani ya mwisho mwezi Oktoba. Na mtoto Hertsegovina ( Pichani) yeye yuko darasa la saba. Kesho kutwa anaanza mitihani ya kumaliza elimu ya msingi.
"Usimfikirie sana baba yako kwa sasa, fikiri kuhusu mitihani yako. Hata baba yako alitaka sana msome na mfike mbali"- Itika, mjane wa marehemu Daud anamwambia mwanawe aliyekaa kando yangu.
Naam, kama mzazi, unaingiwa na huzuni kubwa unapomsikia mzazi mwenzako aliyeondokewa ghafla na mwenziwake akiyatamka maneno hayo kwa mwanawe.
Kumsaidia mjane wa marehemu kwa sasa , ni kama hicho kilichofanywa na waliojitolea kutoa senti zao. Ndio, ni michango yenu ndiyo ambayo leo imemwezesha mjane wa marehemu awe na hakika ya kupata maji nyumbani kwake, na ndio itakayomsaidia kupata pa kusimamia kwa kuanzisha biashara, ili asije kukatiwa maji tena, na umeme pia. Na watoto nao wawe na hakika ya mlo wao. Ni matumaini yetu.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
0788 111 765
http://mjengwablog.com

No comments:

Post a Comment