Monday, 3 September 2012

POLISI WAUA MWANDISHI IRINGA


MWANGOSI AKISHAMBULIWA KWA MATEKE NA VIRUNGU KABLA YA KIFO CHAKE

*Polisi walimpiga bomu na kumsambaratisha
*Utumbo wazagaa, wananchi wataharuki
*Vilio kila kona, simanzi yatawala Iringa
MWANDISHI wa habari wa Channel Ten, Daud Mwangosi, ameuawa kwa bomu. Taarifa zilizopatikana kutoka Mjini Iringa zinasema kuwa, Mwangosi aliuawa alipokuwa akipiga picha za polisi waliokuwa wakidhibiti maandamano ya wafuasi wa Chama cha demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mjini Mufindi jana jioni.
Taarifa hizo zinasema kuwa, baada ya kudaiwa kupigwa bomu hilo, Mwangosi alisambaratishwa na mwili wake kuwa vipande vipande huku utumbo ukizagaa eneo la tukio. Kutokana na tukio hilo, taarifa zinasema kuwa, wananchi waliokuwa eneo la tukio walitaharuki na kuanza kulia, baada ya kutoridhishwa na jinsi alivyouawa mwandishi huyo wa habari.
Pamoja na hayo, taarifa hizo zinasema kuwa, jana asubuhi, kabla ya polisi kuanza kudhibiti maandamano hayo, Mwangosi alikwenda kufanya mahojiano na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, ili kupata uhakika wa maandamano ya Chadema yaliyopangwa kufanyika Mjini Mufindi jana hiyo hiyo.

Wakati akiwa katika mahojiano hayo, inasemekana kamanda huyo wa polisi alikasirika na kumtaka aeleze anauliza maswali hayo kama nani, jambo ambalo lilimfanya mwandishi huyo wa habari kuondoka ofisini kwa ofisa huyo wa polisi bila majibu ya uwepo wa mkutano huo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, wakati Mwangosi akizungumza na Kamanda Kamuhanda, alikuwa na ratiba ya mikutano ya chama hicho ingawa kulikuwa na taarifa kwamba, polisi wamezuia mikutano yoyote hadi Sensa ya Watu na Makazi itakapokamilika.

Kamanda Kamuhanda alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi simu yake ilikuwa ikiita bila majibu.

Kuuawa kwa mwandishi huyo, ni mwendelezo wa vifo ambavyo vimekuwa vikidaiwa kusababishwa na askari polisi pindi wanapokuwa wakizuia maandamano ya wafuasi wa CHADEMA.

Wiki iliyopita, askari polisi waliua mwananchi mmoja mkazi wa Morogoro wakati walipokuwa wakidhibiti maandamano ya wafuasi wa chama hicho, waliokuwa wakitaka kuandamana.

Pamoja na polisi kutanda kila kona ya Mji wa Morogoro, wananchi hao waliandamana hadi Viwanja vya Uwanja wa Ndege ambako viongozi wa CHADEMA walihutubia mkutano wa hadhara.

Mwanzoni mwa mwaka jana, polisi walidaiwa kuua wananchi watatu Mjini Arusha wakati walipokuwa wakidhibiti maandamano ya wafuasi wa chama hicho.

Wakati hayo yakiendelea, jana awali Jeshi la Polisi, Mkoa wa Iringa, lilipiga marufuku mikutano ya CHADEMA, kupitia Oparesheni yao ya M4C, ili kupisha Sensa ya Watu na Makazi inayotarajia kukamilika Septemba 8 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, alisema zuio hilo la mikutano ya CHADEMA, litaendelea mpaka watakapotoa maagizo mengine juu ya mikutano hiyo.

“Ni kweli jana saa mbili tuliwapa barua ya kuruhusu shughuli zao ila baada ya kuongezwa kwa kazi ya Sensa ya Watu na Makazi nimepokea agizo la kusitisha mikutano hii.

“Mimi ninakaribia kustaafu na kazi yangu ninaipenda, hivyo siwezi kuruhusu suala la maandamano kinyume na maagizo yaliyopo,” alisema Kamanda Kamuhanda.

Wakati Kamanda Kamuhanda akisema hayo, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Willbrod Slaa, alisema msisimko wa mabadiliko ya kisiasa yanayoendelea hivi sasa nchini, hayataweza kusimamishwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi, hata kama wataamua kuwaua viongozi wote wa chama hicho.

Dk. Slaa aliyasema hayo jana mjini hapa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya hatua ya Jeshi la Polisi kuzuia mikutano yao, huku jeshi hilo likiapa kuzuia mikutano hiyo kwa gharama yoyote.

Katibu Mkuu huyo alisema, chama chake kilipata taarifa za kusitisha mikutano jana ambapo alilazimika kuwasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP ), Said Mwema, ili kupata ufafanuzi kutokana na kukiukwa kwa makubaliano ya awali, ambayo yaliwataka kusitisha mikutano yao kwa siku tano kisha waendelee na ratiba yao.

“Kwa nia njema nilimpigia IGP Mwema ili kuweza kujadiliana juu ya jambo hili, lakini hakupokea simu mpaka nilipomtumia ujumbe mkali akaniambia, angepiga saa mbili usiku pia hakufanya hivyo na nilipomtafuta, alisema zuio linaendelea.

“Nikamuuliza kama Watanzania wameelekezwa wawatafute waandikishaji wa Sensa kwa namba za simu wawe sababu ya kuzuia shughuli zetu halali, Mwema hakuwa na jibu,” alisema Dk. Slaa.

Alisisitiza kuwa, hata baada ya kushindwa kutolea maelezo ya hoja hiyo, IGP Mwema alisema hilo ni agizo na ni lazima, litekelezwe kwa sababu ni amri iliyotolewa kisheria.

Dk. Slaa alisema, hata alipomuuliza Mkuu huyo wa Polisi nchini ni sheria gani inayozuia hali hiyo, hakuweza kumjibu huku akisisitiza amri yake ifuatwe.

“Sisi hatuna bunduki, hatuna mabomu wala majeshi, lakini Serikali ya CCM na Polisi wanapaswa kutambua haya tunayoyafanya ni sawa na gharika kuyazuia ni ngumu hata kama watatuuwa viongozi wote watambue mioyo ya Watanzania, itaendelea kulilia mabadiliko haya,” alisema Dk. Slaa.

Alisema sheria ya Sensa inabainisha wazi kuwa, kama kutakuwa na zuio lolote juu ya shughuli hiyo, mhusika atahesabika kuwa ni mhalifu kazi ambayo mahakama imeshafanya kwa kuwahukumu baadhi ya watu waliochana karatasi za dodoso.

Wakati huo huo, Mkuu wa Operesheni ya M4C Benson Kigaila alieleza kuwa, mikakati hiyo ya kuzuia mikutano ya CHADEMA ni mipango ya CCM kutokana na baadhi ya wabunge wao kuomba hilo katika Bunge lililopita.

Alisema kwamba, Agosti 4 mwaka huu walipokuwa wakijiandaa kufanya mikutano yao katika Mkoa wa Morogoro, Jeshi la Polisi lilizusha sababu mbalimbali alizoeleza hazikuwa na msingi na kwamba, hata walipotumia busara ya kukubaliana bado waliendelea kubuni hila chafu za kuzuia.

“Hawakutosheka na zuio la Agosti 4, wakaja na zengwe la Agosti 27 kuwa barabara ni ndogo na kwamba siku hiyo ni ya kazi, baada ya hapo wakaja na sensa, tumewasikiliza leo tena wanatuambia bado kuna zuio hili haliwezekani,” alisema Kigaila.

Mkuu huyo wa Oparesheni alisema chama chao kilitii matakwa ya Jeshi la Polisi, kwa lengo la kuuonyesha umma ni namna gani jeshi hilo linatumika na kwamba sasa wamefika mwisho wa kusikiliza matakwa ya jeshi hilo yasiyo katika sheria.

No comments:

Post a Comment